27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe awasha moto bungeni

basheNa Bakari Kimwanga, Dodoma

WABUNGE wameendelea kuchangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, huku Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), akiitaka Serikali kutenga Sh bilioni 7.5 kwa ajili ya kuwakatia bima ya afya wajawazito kote nchini.

Amesema hatua hiyo itasaidia mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto kama ilivyo katika mkakati wa Serikali kuliko ilivyo sasa.

Bashe aliyasema hayo jana bungeni mjini Dodoma, akichangia bajeti ya wizara hiyo.

Alisema takwimu zinaonyesha wajawazito 42 hupoteza maisha kwa siku jambo ambalo ni hatari kwa Taifa.

“Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge hili tupitishe kwa kuitaka Wizara ya Fedha na Mipango impatie Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Sh bilioni 7.5 mwaka huu ili wajawazito wote wakatiwe bima ya afya kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),” alisema.

Alisema takwimu zinaonyesha Tanzania ina wanawake milioni 1.2 ambao hujifungua kila mwaka chini ya mwamvuli wa NHIF kwa wastani wa Sh 50,400 kwa kila mwanamke.

Alisema wanawake ambao wanakwenda kliniki wanajulikana kwa kuwa taarifa zao zipo, hivyo wakikatiwa bima ya afya baada ya miezi tisa anakwenda kujifungua bila kwenda na kiwembe ama ‘glovsi’.

Akizungumzia suala la ukagutuaji wa madaraka (D by D), alisema kwamba sera ya afya inasimamiwa na Wizara ya Afya, lakini inashangaza suala hilo kupelekwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

“Mimi ninachotaka kusema katika nchi yetu tuna matatizo makubwa katika sekta mbili, sekta ya afya na elimu, haiwezekani sera wanaosimamia wizara utekelezaji TAMISEMI, sasa Bunge ni vema tuangalie suala hili la D by D, ni tatizo katika nchi yetu. Ni vema tuondoe hili TAMISEMI wabaki na miundombinu tu,” alisema huku akishangiliwa na wabunge wa pande zote.

Alisema haiwezekani wizara tatu zisimamie wizara moja ikiwemo Tamisemi na Utumishi kwani haitawezekana kupatikana kwa ufanisi.

Bashe alisema kwa mwaka huu wa fedha akabidhiwe waziri hospitali zote za mkoa na si tu za rufaa, itasaidia katika usimamizi wa sera, kusimamia utendaji katika hospitali husika, itasimamia uendeshaji na Tamisemi waachiwe jukumu la kuendeleza miundombinu peke yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles