25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe alia na sera ya kilimo

BENJAMIN MASESE-MWANZA

SERIKALI imesema  sera iliyopo ya sekta ya kilimo inayotumika sasa,  ndiyo cha chanzo cha wakulima kuwa masikini kutokana na kuwatumikisha  wananchi kuilisha nchi na  matajiri, huku wakiwa wanakabiliwa na changamoto kubwa.

Kutokana na hali hiyo, imesema sera imepitwa na wakati ambapo wizara  imelazimika kuanza kuipitia upya  na kuondoa  changamoto  na vikwazo kwa wakulima.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe  wakati akifungua sherehe za wakulima  na maonyesho ya kilimo (Nanenane) katika viwanja vya Nyamhongolo mkoani Mwanza.

Aliwapiga marufuku wakuu wa wilaya na mikoa kuwazuia wakulima kuuza chakula chao kwa kuhofia uwepo wa njaa.

Alisema kila mkulima, anajua namna anavyotunza  na kuilisha familia yake hivyo  kama kuna kiongozi anahofia uwepo wa njaa ni vema  akanunua mazao hayo  kwa bei anayotaka mkulima na kuyatunza ili yaweze kusubiria dhana aliyoiweka kichwani kwake, kwamba kutakuwapo na uhaba wa chakula.

“Hatuwezi kujenga viwanda wakati wakulima ni masikini wa kutupwa,  lazima tuwawezeshe kwa kutengeneza mazingira ya watu kunufaika na kilimo chao sambamba na kuwa na soko la uhakika, ndio maana leo hii kama wizara tumeanza kupitia sera ya kilimo na kuondoa changamoto  na  vikwazo vilivyokwekwa .

“Sera iliyopo imepitwa na wakati  kabisa,  inawaumiza wakulima   na kuwafanya kubaki  kila mwaka kuilisha nchi na matajiri huku wao wakibaki na umasikini wao  huku kukiwapo na utitiri wa taasisi nyingi ambazo ukichunguza zimeanzishwa kwa lengo la kuwakandamiza, hii haiwezekani kama wizara tumeanza kuangalia ni taasisi gani zinatakiwa  kufutwa na kubaki  chache.

“Fedha ambazo zilikuwa zikielekezwa kwenye utitiri wa taasisi hizo, zitaelekezwa katika mfuko maalum  ambo  wizara tunatarajia kuanzisha  na kazi ya mfuko huo ni kufidia mkulima pale inapotokea mtikisiko wa bei katika soko la dunia, kama serikali hatuna uwezo wa kuthibiti bei ya soko la dunia, mfuko huo ndio utakaokuwa na kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuwafikia wakulima,”alisema.

Alisema Serikali ilikuwa ikipokea fedha nyingi kutoka mataifa ya nje ili kuendeleza kilimo, lakini zilikuwa zikishia katika semina mafunzo kwa  watendaji, huku  asilimia 50 ya fedha zilizokuwa zikipokelewa ndizo  zinafika kwa wakulima.

Alisema  alitoa mfano, mtikisiko uliotokea katika pamba na korosho  mwaka huu, kama Serikali  isingechukua hatua ya kuzungumza na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa fedha za kununulia pamba,  basi  wangeuza kilo moja  kati ya Sh 500- 700 kulingana na bei ya soko la dunia.

Alisema  tayari vikao kati ya Serikali na BoT vya kutoa fedha za pamba vimekamilisha juzi na kuanzia leo Jumatatu fedha zitaanza kutolewa katika benki zingine kwa ajili ya kulipa wakulima wa pamba ambapo tayari bei elekezi ni Sh 1,200 kwa kilo moja.

“Ichukulieni hali  hali ya usafirishaji wa pamba kutoka mikononi mwa wakulima kama dharula maana mvua ikianza kunyesha zao hilo likiwa bado lipo majumbamni ni hasara, niwaambie baada ya kupitisha sera mpya na kuunda mfuko wa fidia kwa wakulima, hakika suala kama lililojitokeza katika korosho na pamba litakuwa historian a halitajitokeza maana Serikali tumejipanga kuchukua hatua.

“Mbali ya mfuko wa fidia, kama wizara tumebaini kuwapo na kasoro kadhaa katika bodi ya pamba hivyo kama Serikali  tunaigiza bodi ya pamba kuanza mchakato wa kuainisha mahitaji yote ya wakulima kisha tutakuja na mfuko fulani  wa uagizaji pembajeo kwa pamoja, lengo ni kupunguza hasara kwa mkulima,”alisema.

Wakati huo huo, Bashe aliwaagiza wakuu wa wilaya, mikoa na watendaji wengine wanaohusika na sekta ya kilimo kuhakikisha mwaka huu wakulima hawapandi pamba kwa kumwaga mbegu, ispokuwa  kwa kutumia kamba ikiwa lengo ni kulima kisasa na kupata mavuno mengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles