24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BARRICK, SERIKALI VYAFIKIA MARIDHIANO

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


BAADA ya mazungumzo ya takribani miezi mitatu kati ya serikali na Barrick Gold kuhusu udanganyifu kwenye biashara ya mchanga wa dhahabu (makinikia), pande hizo mbili zimefikia maridhiano na kampuni hiyo kutoa asilimia 16 ya hisa zake kwenye kila mgodi wake nchini, asilimia 50 ya mapato yake na Dola za Marekani milioni 300 (Sh bilioni 700).

Muda mfupi baada ya makubaliano hayo jana mchana, Acacia yenye hisa asilimia 36.1 kwenye migodi hiyo, hisa zake kwenye soko la hisa za Landon zilipanda kwa asilimia 18.

Baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyekuwa akiongoza timu ya Tanzania kwenye mazungumzo hayo na Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick, Profesa John Thonton, aliyezungumza kwa niaba ya kamapuni yake yenye hisa asilimia  63.9 kwenye migodi hiyo, Rais Dk. John Magufuli, alisema baada ya kufikiwa kwa maridhiano hayo kwa sasa, Watanzania watoe ushirikiano na kampuni hiyo.

Akizungumzia mafanikio ya mazungumzo hayo jana, Profesa Kabudi alisema kampuni hiyo ya Barrick imekubali masharti yote yaliyopo katika sheria mpya ya madini yaliyotungwa na Bunge.

“Mazungumzo haya hayakuwa mepesi hata kidogo yalikuwa magumu, kuna nyakati zilituteteresha sana lakini pande zote mbili tulifika mahali tukaona ni muhimu wote tukubaliane mambo ambayo yatajenga msingi imara wa mahusino yetu ya siku za usoni.

“Lakini pia bila kufunika chini ya zulia yale yote yaliyofanyika huko nyuma matokeo yake leo tunayaona,”alisema.

Makubaliano

“Wamekubali masharti yote yaliyomo katika sheria mpya iliyotungwa na Bunge letu, wamehakikisha yanaingia katika mfumo wa fedha tuliokubaliana,”alisema Profesa Kabudi.

Pamoja na hilo, alisema pia wamefikia makubaliano kuhakikisha Serikali inapata hisa asilimia 16, kama sheria ilivyotamka huku inapokuja suala la kugawana itakuwa nusu kwa nusu.

Alisema migodi yote itaweka fedha zao zote za madini katika akaunti zilizopo hapa nchini.

“Pia tumekulibaliana ofisi zao za London na Johannesburg zitahamishiwa Tanzania na makao makuu ya kampuni hiyo yawe Mwanza ili iwe pale machimbo yanapofanyika.

“Tumekubaliana umuhimu wa kuanzisha kampuni mpya ya kusimamia na kuendesha migodi itakayoongozwa na mtendaji mkuu, mkurugenzi wa fedha na manunuzi awe mtanzania na ingawa Serikali itakuwa na asilimia 16 na 50 kwa 50, lakini wamekubali itakuwa na wawakilishi bodi ya wakurugenzi katika mgodi huo,”alisema .

Profesa Kabudi alisema wamekubaliana sehemu kubwa za kazi za huduma mbalimbali za migodini zitafanywa na kampuni za kitanzania na Watanzania.

“Tumekubaliana kuimarisha huduma za jamii katika maeneo yanayozunguka migodi kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi.

“Kila kampuni itakayoendesha kampuni ya madini inaachana na wafanyakazi wa mikataba, itawaajiri wafanyakazi wazawa na hawatakaa katika makambi na  wanafikiria kujenga barabara kutoka Mwanza hadi mgodini ili wafanyakazi warudi majumbani kwao jioni.

“Kuajiri Watanzania katika nafasi muhimu za uongozi na utaalamu au kuwafundisha, ili baadaye waweze kujaza nafasi za uongozi.

“Kutengwa kwa bajeti maalumu kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata makinikia na kujenga maabara ya kupima makinikia.

“Serikali itakuwa na umiliki wa madini mengine yote; yatakayopatikana wao watabaki na dhahabu, fedha na shaba mengine yatakayobaki ni ya Watanzania.

“Asilimia zile 16 ni kwa kila mgodi kama ambavyo sheria imesema na kesi zote mashauri yote yatafanyika hapa hapa nchini,” alisema Profesa Kabudi.

Fidia

Kuhusu fidia ya Sh trilioni 425.4 ambazo kampuni hiyo ilipaswa kuilipa Serikali ya Tanzania, Profesa Kabudi alisema eneo hilo lilichukua muda mrefu lakini wamekubali kulipa Dola za Marekani milioni 300 sawa na Sh bilioni 700 wakati mazungumzo yakiendelea.

“Jambo hili limekuwa gumu kwa sababu mambo yaliyofanyika si mazuri, hayafurahishi na yamefanyika kwa kipindi cha miaka 16.

“Tulichukua muda mrefu hivyo ili tupate nyaraka zote na risiti zote inahitaji muda, sasa wakati mazungumzo yanaendelea kuhusu jambo hili wamekubali kutoa dola milioni 300 sawa na Sh bilionil 700,”alisema Profesa Kabudi.

Mwenyekiti wa Barrick

Baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick, Profesa John Thonton alisema makubaliano hayo yataenda kuidhinishwa na bodi nchini Uingereza ambayo ina hisa asilimia 64.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi, ambayo ni muhimu kwa biashara katika karne hii ya 21.

Profesa Thornton alisema  Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano hayo na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.

Alisema wamekubaliana pande hizo mbili zitakuwa zinagawana faida asilimia 50 kwa 50.

Rais Magufuli

Kwa upande wake Rais Dk. Magufuli alimuagiza Profesa Kabudi kuunda timu zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi pamoja na migodi mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze kunufaika ipasavyo.

“Nataka machimbo yote ya dhahabu mchakato kama huu ufanyike, pia nakuagiza Profesa Kabudi biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi nako ni lazima kufuata utaratibu huu, asiyetaka aondoke atuachie madini yetu, tumepewa na Mwenyezimungu na tutaendelea kuchukua msimamo huu huu,”alisema Rais Magufuli.

Alisema  mafanikio yaliyofikiwa baada ya kuwepo majadiliano kati ya wataalamu wa Tanzania na wale wa Barrick kuhusu biashara ya madini ya dhahabu yameweka rekodi ya aina yake.

Alisema hatua hiyo inaweza kuzisukuma nchi nyingine za Afrika kuja Tanzania kujifunza namna inavyoweza kujadiliana na wawekezaji wa kigeni na hatimaye kukubaliana.

“Tumeonyesha mfano na kweli tukiamua tunaweza, haya majadiliano hayakuwa kitu rahisi lakini mwisho wa siku tumefanikiwa na naamini nchi nyingine za Afrika zitataka kuja hapa kujifunza namna tulivyofanikiwa,” alisema Rais Magufuli.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli alisema amejifunza kuwa mazungumzo daima yana faida na licha ya kuona ugumu wake lakini aliendelea kuiamini timu yake huku akiitia moyo kutorudi nyuma.

Alisema kuanzia sasa Tanzania imeweka kiwango kipya kuhusu mikataba ya madini na kwamba kiwango hicho, kilichofikiwa na kampuni ya Barrick ndicho kitatumika katika majadiliano na kampuni nyingine.

Rais Magufuli alisema makubaliano hayo yataisaidia nchi katika uzalishaji ajira zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi.

Julai 31 mwaka huu, kamati maalumu iliyoundwa Rais John Magufuli na wawakilishi kutoka Barrick Gold Corporation, ilianza mazungumzo juu ya biashara ya madini yanayochimbwa na migodi ya kampuni hiyo hapa nchini.

Msingi wa kuundwa kwa kamati hiyo ulitokana na ripoti ya pili ya kuchunguza mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia) kuitaja Kampuni ya Migodi ya Acacia kufanya kazi nchini kinyume na sheria, kutokana na kutosajiliwa na Msajili wa Kampuni (Brela).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles