24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Baraza laipongeza Wizara ya Kilimo

MWANDISHI WETU-ARUSHA

UONGOZI wa Baraza la Kilimo Tanzania umeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa uamuzi wake wa kutangaza kutokuingilia kupanda kwa bei ya mazao ya kilimo, hasa unga na mahindi na kwamba uamuzi huo utazidi kumsaidia mkulima kuanza kunufaika na sekta ya kilimo.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Arusha na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Kilimo Tanzania, Jacqueline Mkindi, ilieleza kuwa uamuzi huo wa Serikali wa kutokupanga bei elekezi kwa mazao hayo ni hatua muhimu katika kutetea nafasi ya mkulima katika kilimo biashara na soko huru.

“Sisi Baraza la Kilimo kwa dhati kabisa tunaipongeza Serikali kwa uamuzi wake huu  wa kutetea soko huru la mazao kwa kutokupanga bei elekezi kwa wakulima wa mahindi, hii inazidi kuonyesha dhamira njema ya Serikali ya kuzidi kumsaidia mkulima wa Tanzania,” alisema Jacqueline.

Alieleza kuwa baraza hilo limeridhishwa na utendaji kazi wa viongozi wa juu wa Wizara ya Kilimo na kwamba mara kadhaa wamekuwa wakisikika wakimtetea mkulima kwa kulinda mazao yake baada ya kutoka shambani.

“Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amekaririwa akitoa msimamo wa Serikali wa kutokupanga bei elekezi kwenye unga na mahindi. Jambo hili ni jema sana, lakini pia hata Naibu wake, Hussein Bashe aliwahi pia kusema Serikali haina mpango wa kuzuia kuuza mazao nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kutokupanga bei elekezi kwa mazao ya kilimo.

“Sisi kama Baraza la Kilimo kwa niaba ya wakulima nchini, tunafarijika sana tukiskia kauli hizi zikitoka kwa viongozi wetu,” alisema Jacqueline.

Hivi karibuni akijibu swali bungeni, Bashe alisisitiza msimamo wa Serikali wa kutokuingilia na kupanga bei elekezi kwa mazao ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kuondoa marufuku ya uuzaji wa mazao nje ya nchi.

“Ni matumaini ya baraza kuwa kama sera za kutoingilia masoko zikidumishwa, baada ya miaka michache ijayo Tanzania itakuwa mzalishaji mkubwa wa chakula, hasa mahindi na mchele na kuwa mazao haya yatakuwa ni miongoni mwa mazao yatakayowakomboa wakulima kiuchumi kwani kuna soko kubwa kwa nchi zinazotuzunguka,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kilimo, Janet Bitegeko alisema kwa sasa Tanzania inazalisha zaidi ya tani milioni sita za mahindi na kwamba lengo ni kufikia tani milioni nane ifikapo mwaka 2020/21.

“Baraza tunaamini kama wakulima watapata bei nzuri kwa miaka mitatu au minne mfululizo bila kuingiliwa, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia uzalishaji wa tani milioni 15 za mahindi kwa mwaka, kwa sababu wakulima wengi zaidi watakuwa na ari kubwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles