33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Balozi Seif: Sitishwi na wanasiasa

Balozi Seif Ali Iddi
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi

Na Umar Mukhtar, Zanzibar

MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, amesema hakuna mwanasiasa yeyote Zanzibar mwenye ubavu wa kumpangia majukumu ya kazi za serikali zaidi ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein aliyemteua.

Balozi Seif alitoa msimamo huo jana, wakati akizindua ujenzi wa maskani ya Chama Cha Mapinduzi iitwayo Amani na Utulivu katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Balozi Seif alitumia nafasi hiyo kumjibu Naibu Waziri wa Makazi, Ujenzi, Maji na Nishati ambaye anatoka Chama cha Wananchi (CUF), Haji Mwadini Makame.

Mwadini alimshitaki Balozi Seif kwa Dk. Shein akimshutumu  kuwa amekuwa akifanya siasa na ziara za mfululizo katika jimbo lake kuliko kusimamia kazi za maendeleo katika majimbo mengine visiwani humo.

Alisema akiwa msimamizi mkuu wa kazi za Serikali, hazuiwi na mwanasiasa yeyote kufika mahali au kuzuiwa asitimize wajibu aliopewa kisheria na kikatiba katika kusimamia maendeleo na kuimarika kwa huduma za jamii, kwa sababu ya kumuogopa mwanasiasa.

Alisema Rais Dk. Shein alimteua kuwa kiranja mkuu wa shughuli za Serikali na kuratibu kazi za maendeleo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, hivyo ameapa hatakubali kuona wananchi wanakabiliwa na matizo yanayokosa utatuzi wa haraka na kuyaacha kwa kuogopa kushitakiwa kwa Rais au kulaumiwa na wanasiasa wa upinzani.

“Ndugu zangu nataka niwaeleze, nimeshitakiwa kwa Rais na Mwakilishi wa Jimbo la Nungwi ati navuruga siasa kwa kusimamia maendeleo ya jamii, namwambia yeye na washirika wake sitaacha kufanya hivyo na hana ubavu wa kunizuia katika miaka ya kazi zangu kikatiba na kisheria, kama ameshindwa kazi awaeleze wananchi, kuku wangu mwenyewe sipati tabu ya kumpiga kwa manati,” alisema Balozi Seif.

Alisema kazi ya kuwahudumia wananchi ni jukumu la Serikali ya CCM ambacho kilishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kisipofanya hivyo kitasutwa na wananchi kwa kutotimiza wajibu na majukumu waliyokabidhiwa.

Alisema utumishi wake katika Jimbo la Nungwi ulianza tangu mwaka 1966, wakati akiwa mwalimu wa shule ya msingi hadi mwaka 1968 na miongoni mwa wanafunzi aliowafundisha ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Silima Ame Peraira na Sheha wa Nungwi, Kombo Mnungwi.

“Hawa wawili ni kati ya wanafunzi wangu niliowafundisha, sikuitumikia Nungwi na Zanzibar jana au leo, nimetumia elimu yangu, nguvu, maarifa na bidii kuijenga nchi yangu bila kuchoka, nitaendelea kufanya hivyo, sitababaishwa, nimeapa kwa mujibu wa katiba kuisimamia Serikali,” alisisitiza Balozi Seif.

Alisema wananchi mahali popote wanapokuwa na matatizo ya ukosefu wa maji, umeme, kukosekana kwa pembejeo za kilimo, zana za uvuvi na ubovu wa miundombinu huenda ofisini kwake wakijua ndiye mtendaji mkuu wa kazi za kiserikali.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. hoja si kuwajibika kama kiongozi wa serikali, hoja inakuwa jimbo la nungwi tu? wao dio wenye shida peke yao? mbona anakwepa hja ya msingi?

    • Mimi napenda kutoa maoni yakngu kua kiongozi bora ni yule anaejua matatizo ya watu anaowaongoza Makamu wa Rais Zanzibar anajua nini anachokifanya kuwa yeye ni kiongozi ambae yupo karibu na wananchi anaowaongoza na pia kwa kuwa yeye ni mtendaji mkuu wa serikali anayo haki na wjibu wa kwenda popote wakati wowote saa yoyote na mara atakazo hata kuweka kambi Nunwi na si Nungwi tu hata popote katiba inamruhusu huo ni wasiwasi wa wanasiasa tena wale ambao wamejipandikiza Nunwi kuwa muda wao umekwisha uwakilishi bai bai uchaguzi ujao kosa lililotokea Nungwi halitokei twna kama wapinzani waliziba bomba za maji makusudi kwa zege huu ni ujahili na waeleweke hawana maana ati maji yametoka kwa ajili ya naibu waziri wa maji ambae ni mpinzani uongo wananchio tusidanganywe na wanasiasa uchwara

      • Mimi napenda kutoa maoni yangu kua kiongozi bora ni yule anaejua matatizo ya watu anaowaongoza Makamu wa Rais Zanzibar anajua nini anachokifanya kuwa yeye ni kiongozi ambae yupo karibu na wananchi anaowaongoza na pia kwa kuwa yeye ni mtendaji mkuu wa serikali anayo haki na wajibu wa kwenda popote wakati wowote saa yoyote na mara atakazo hata kuweka kambi Nungwi na si Nungwi tu hata popote katiba inamruhusu huo ni wasiwasi wa wanasiasa tena wale ambao wamejipandikiza Nungwi kuwa muda wao umekwisha uwakilishi bai bai uchaguzi ujao kosa lililotokea Nungwi halitokei tena kama wapinzani waliziba bomba za maji makusudi kwa zege huu ni ujahili na waeleweke hawana maana ati maji yametoka kwa ajili ya naibu waziri wa maji ambae ni mpinzani uongo wananchi tusidanganywe na wanasiasa uchwara……hebu wananchi sasa tuachane na soasa potovu tulete maendeleo katika Nchi yetu wanasiasa hawataki maendeleo kwa wananchi bali wao ni kutaka kujinufaisha na maslahi yao

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles