24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

BALOZI MONGELA: WAZEE TULIPINGA BUNGENI UJIO WA VYAMA VINGI

Wiki iliyopita gazeti hili katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani lilifanya mahojiano Maalumu na  Balozi Getrude Mongela, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake, uliofanyika Beijing nchini China Septemba 15, 1995,tunaendelea na mahojiano hayo…..

MTANZANIA: Je, unafikiri tulipofika kuhusiana na ajenda mlizokwenda kuzungumzia Beijing nchi washiriki zinatekeleza?

BALOZI MONGELA:  Hapa tulipofika sihaba lakini bado safari ni ndefu kwa maana kwamba tulikotoka ni mbali, mila na desturi haziwezi zikafutika kwa mara moja, mila inayomuona mwanamke sio sawa katika baadhi ya makabila na sitaki kutaja baadhi ya makabila ambayo mwanamke hatakiwi  kuzungumza  akiwa  amesimama lazima achuchumae, hata vikao hivi vya Serikali mwanamke hatakiwi kupiga kelele kuongea mbele ya wanaume. Hata kwenye vikao vyetu hapa Tanzania yapo makabila yanaona hivyo mwanamke ni basi tu siasa hizi ndizo zinawaleta katika nafasi ya kuzungumza na kuamua mambo.

Ingawaje nah ii pia imetuonesha kuwa baadhi ya mila na desturi zilikuwa nzuri, zinamlinda mwanamke nazo tulikuwa tumezitupa. Kwa mfanobaadhi ya kabila zetu hapa Tanzania ilikuwa kama watu wanataka kwenda vitani kuna kipindi wanauliza ngoja tukaulize nyumbani, sasa wakija ukiona wamekubaliana ujue kila mtu ameshauliza mke wake na kukubaliwa na kama hawajakubali basi hawaendi vitani. Hata kuuza kitu kama ng’ombe anasema subiri kwanza nikashauriane na mwenzangu, hili lilikuwapo na kulikuwapo pia na thamani ya mwanamke akiwa mtu mzima anaweza kuheshimika na kuombwa ushauri na hasa anapofika umri wa kutozaa tena wanamwamini zaidi kwa sababu anakuwa kama mwanamme na kwa kumuamini  huko ameweza  kuhusishwa katika vikao vya uamuzi ndani ya familia, ndani ya ukoo na ndaniya jamii.

Kwahiyo sisi huku tuseme katika nchi za Afrika ilikuwa kuwa mtu mzima ilikuwa siyo balaa, ilikuwa ni heshima na imekuwa sasa katika hali ya kuheshimika kwahiyo sisi kuitwa bibi ilikuwa tunaona raha tu unafurahi, kila mtu kijijini ni mume wako, vijana wote ni waume zako, lakini sasa hivi kina bibi wengine nao wanataka kujifanya nao ni vijana, wamepoteza mila na desturi inayosema kuwa bibi ni heshima.

MTANZANIA: Ajenda ipi ambayo mliijadili wakati ule kule Beijing ambayo unafikiri hadi sasa haijafanyiwa kazi?

BALOZI MONGELA: Nafikiri kwenye upande wa uamuzi, mwanamke kushiriki katika kuamua bado kunalegalega, uamuzi katika ngazi zote ukianzia katika ngazi ya familia bado kuna ukakasi  ingawaje kuna hatua zimechukuliwa. Unapokuja kwenye ngazi za kuongoza unakuta hata kwenye vyama vyetu bado kuna ukakasi kumfanya mwanamke kuwa Mwenyekiti wa chama, kuwa Katibu wa chama kitaifa.

Nitatumia mfano wa chama changU (CCM) tuna wanawake wawili tu ambao ni Wenyeviti wa mikoa, wanawake wawili ni aibu na hili lazima niliseme wazi kwa sababu ni chama changu ni chama dume, mimi raha yangu nataka kuona  katika kikao cha  Halmashauri Kuu ya Taifa Wenyeviti wa CCM nusu wanaume au zaidi kidogo tu na idadi kubwa pia ni wanawake nitafurahi kweli.

Lakini ukija kwenye ngazi ya Serikali pia bado kuna ukakasi, watu wanafikiria kuwa hakuna watu wa kujitokeza, kwani wanaume wanajitokeaza? Si wanaonekana? Tumesoma na madigirii tunayo lakini kutokana na ukakasi uliopo, wakiteuliwa wanawake watano basi tunaonekana wameteuliwaaaaa.

Na hili suala Mama Sopha Kawawa alilikataa nikimsikia kwa masikio yangu. Siku moja Mwalimu alimteua mwanamke kuwa Balozi Mama Tatu, huyu alikuwa pia ni Mwalimu tena Mwalimu wa Sayansi. Mwalimu akamuuliza Sophia mbona Mwenyekiti  hujanipongeza? Mama Sophia akamjibu nikupongeze nini na bado endelea mpaka tutakapofika mahali  tukiona kazi umeifanya tutakupongeza.

Namimi ninaona ukiwa umeteua watu mia moja na ukateua watu watano hii inaonesha ni kama vile tunapewa sadaka. Ifike mahali ionekane haifikiriwi hata kidogo, anateuliwa mtu kwa uwezo wake na kwambahuyu ameteuliwa mtu kwa uwezo wake na sio kwa sababu ya upendeleo maalumu.

Watu waingie bungeni si kwa sababu ya upendeleo maalumu, waingie bungeni kwa sababu jamii inawaona  kinamama hawa wanaweza na sio majaribio. Sasa hapo ndio palipo na kazi ni kiasi gani hawa kinamama  ambao kwa miaka mingi wameachwa  nyuma kielimu, wameachwa nyuma katika usawa, wameachwa nyuma katika maendeleo ya uchumi ni kiasi gani utawatoa katika mstari huo na kuhakikisha wanateuliwa bila mtu kufikiri. Kwa sababu siku moja Mwalimu alisema Jamani ninapoteua mwanamke napata  mwanamke  mpaka nifikirie kama mume wake atakubali, mbona nyie wanaume hamfikiriwi kama wake zenu watakubali?

Kwahiyo hii mpaka itoke kwenye utamaduni wa kufikiri kwamba hili linamuhusu, hili litamfaa ni lazima tufanye kazi ya ziada ndio maana ya yale maamuzi 12 tuliyofanya Beijing ikiwamo elimu, afya kwa sababu wakati mwingine una afya mbovu, umezaa watoto 12 utafikiri kwenda kuwa mbunge. Kwahiyo vitu vyote hivyo ni lazima vifanyiwe kazi kwa pamoja ili mama huyu umpe uwezo.

MTANZANIA: Unafikiri  Umoja wa Wanawake (UWT) ambao uko chini ya chama chako unadhani unawajibika ipasavyo katika kumkomboa mwanamke wa Tanzania kutoka katika lindi la umaskini, kama ambavyo ilani ya CCM inavyoutaka?

BALOZI MONGELA:  Bado.

MTANZANIA: Kwanini bado?

BALOZI MONGELA: Kwa sababu ya yale makando kando yaliyowazingira wo si nje ya jamii na fikra ya jamii.

MTANZANIA: Unafikiri UWT imezingirwa na makandokando gani?

BALOZI MONGELA: Kwa sababu wanawake hatuna uwezo wakituachia peke yetu ambapo hatuna uwezo wa kiuchumi tukomboe hawa wenzetu hawa ni kutukosea haki. Kazi hii ni yetu sote wanaume na wanawake. Na nimegundua kuwa watu wengi wanafikiria masuala haya ya wanawake ni ya wanawake tu. Hapana, ni ya jamii nzima.

Hatutegemei elimu ya watotowa kike isimamiwe tu na wanawake inapaswa chama kizima kifanye hiyo kazi. Ukishawatenga wanawake kwa kuwaweka sentensi ya mwisho ni mbaya. Mimi nasema hii si kazi ya UWT  tu. UWT inafanya kazi sio ya wanawake tu, mpaka uchaguzi tunasimamia UWT. Tunapoona upungufukatika kutekeleza masuala ya Beijing sio ya UWT

MTANZANIA: Unafikiri misingi iliyojengwa na kinamama kama kina Bibi Titi Mohammed, Sophia Simba, Tabitha Siwale na hatimaye ninyi, inasimamiwa?

BALOZI MONGELA: Imesaidia, kwa sabau msingi mkubwa ambao tumeujenga ni kama kuvunja mwiko, mwanamke kwenda kwenye silaha ni kuvunja mwiko. Tunaimarisha sera za Mwanamke na Mtoto na kinababa na unaacha kukaa nyumbani. Kwahiyo kipindi cha kwanza ilikuwa ni kuvunja mwiko na tumeivunja. Na baada ya kuivunja miiko imefungua milango kwahiyo hatuwezi kuruzi nyuma ni lazima twende mbele. Kwa sababu suala la kinamamani la kidunia na la kibinadamu. Sisi tunataka tusaidiane na Rais Magufuli katika kutumbua.

MTANZANIA: Unaionaje Tanzania ya sasa katika siasa, uchumi na mshikamano kama Taifa?

BALOZI MONGELA: Katika uchumi mimi naona mwanga, tukienda kwa spidi hii naona mwanga, watu wataumia, wataumia kwa sababu kamani mwendo kasi asiye na pumzi watahema, wataumia kwa kuhema lakini ndio twende, tumechelewa. Ukiangalia sera za dunia hasa sera za Wachina wanakwenda mwendo kasi na wanataka wachomoke huo. Sasa wale wanakwenda mwendo kasi tuachwe nyuma tena? Tumeachwa nyuma nawakoloni na Mchina naye anakuja atuache nyuma, haya mambo yanawezekana? Haiwezekani. Wa kuhema na waheme, wa kutapika damu na watapike. Na katika kuhema huko sisi wanawake tunaweza. Pumzi tunayo na mapafu tunayo. Kasi gsani itakayotushinda sisi. Tuna mapafu ya mbwa.

MTANZANIA: Awamu ya kwanza ya uongozi, Mwalimu alihamasisha vijana kutokuwa legelege katika kusimamia uhuru wao wa kujieleza na uzalendo kwa Taifa, Unadhani uhuru huo upo kwa sasa?

BALOZI MONGELA: Usipotumia uhuru wako ambao umejengwa kwa muda mrefu ni uzembe. Kwa mfano uhuru tuliopewa sisi ulikuwa ni wa kufanya kazi. Kwa sababu sasa hivi watu wanapata uhuru wa chee (chee)yaani apate pesa kirahisi rahisi, kwa ulaini, huo si uhuru ni utumwa.

Kwahiyo sisi tulikuwa tunajua kila mtu lazima afanye kazi, watu walikuwa wanashikwa kama wakionekana wanazurura tu, walikuwa wakifunguliwa mashamba kule Gezaulole. Kwahiyo uhuru tuliokuwa tunaambiwa ni kwamba kila mtu afanye kazi, ujitegemee na ilitukaa kichwani ili usiwe ombaomba.  Vitu vitatu hivyo tulikuwa tunaviimba, ufanye kazi, usiwe ombaomba, ujitegemee. Na ilikuwa inaimbwa mpaka ngazi ya kijiji, kijiji kijitegemee, tumekuwa na mashindano ya siasa ni kilimo. Hii hatufanyi hata kwa watoto wetu.

MTANZANIA: Unadhani upo umuhimu wa kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya?

BALOZI MONGELA:  Haujatenguliwa uamuzi huo, uliamuliwa bungeni kwahiyo mtu asifikirie ni uamuzi wa chama, ulikuwa ni uamuzi wa Bunge kwahiyo lazima utekelezwe. Ama Bunge tena lirejee na kupitia uamuzi wake wa kwanini isiwe. Na haijatenguliwa na mtu. Full Stop.

MTANZANIA: Unazungumziaje hii hatua ya wanasiasa iliyojitokeza kuhama vyama vyao na kujiunga vyama vingine vya kisiasa?

BALOZI MONGELA: Huo ndio mchezo wa siasa, kama  sera za huyu hazikukutosha tokaaa usilete vurugu, wewe fuata hicho unachokitaka. Sasa kama juzi tumeona watu wameona CCM inafanya mambo vizuri. Nasisi pia CCM kumekua na watu wameona pia CCM haifai. Lakini ni fundisho kwa wapiga kura.

MTANZANIA: Unazungumziaje hili wimbi la watu kutekwa na baadaye wengine kukutwa wameuawa?

BALOZI MONGELA: Huo unyama kokote duniani upo, juzi Marekani katoto kamepiga risasi watu. Ndio maana sisi Beijing tulitaka amani. Na kwamba tabia za malei pia zimekuwa potofu kwahiyo unapata watu wa aina hiyo na watakuwapo, unapata wezi, unapata majambazi. Culture yetu imeharibika, huwezi kusema ni ya kisiasa. Watu wengi sasa wanakosea wanataka kuyabadilisha yawe ya kisiasa. Mimi narudi tena huko huko Beijing turudi kwenye amani.

Hebu angalieni nji jira ya Afrika Kusini imemtumbua Zuma, nilikuwapo Zuma alipomtumbua Mbeki nikashangaa. Ndio nasema tabia za dunia yetu.

MTANZANIA: Wazee kama ninyi ndio tunu yetu vijana, una ushauri gani na hali ya kisiasa ilivyo sasa?

BALOZI MONGELA:  Mzee Ali Hassan Mwinyi alituambia kila zama na kitabu chake. Mimi nilisoma nikawa Youth League na hatukuwa na vyama vingi. Nimeingia bungeni hatukuwa na vyama vingi. Vimekuja siku hizi tumeviruhusu. Ndani ya Bunge la mfumo wa chama kimoja ulikuwa unatoa hoja mpaka jasho linakutoka na hakuna atakayekunyamazisha. Tulikuwa na demokrasi kuliko sasa.

Wewe ukiwa chama fulani ukisema jambo la haki mwenzako anakwambia wewe msaliti. Sisi tulikuwa hakuna usaliti, unasimama kama Mtanzania, chama kimoja mtaachaje kukosoa, unambembeleza nani. Nikisimama Mama Mongela nilisema wazi, watu wakasema hii sio demokrasi.

Wote makofi mkapiga, hasa nyie vijana, haya ngoja tulete vyama vingi, sasa vurugu mechi. Utu uzima wangu unanionesha tuliposema chama kimoja kiongoze mkatuona wazee hatujawa democratic. Leteni vyama vingi sasa tena mnaanza kuhangaika navyo. Hivi ndio vyama vingi vilivyo. Endeleeni, demokrasi mnaenda na yale mnayoyataka.

Nendeni kwenye Hansard tuliyoifanya bungeni kuhusu kuleta vyama vingi, wazee wanavutia huku mnatuletea balaa, huku vijana wakisema hiyo sio dunia inavyokwenda. Tukaenda dunia inavyokwenda. Kama nilivyokupa mfano wa Zuma ndio dunia inavyokwenda. Nilikuwa nikishuhudia wakimfanyia vurugu Mbeki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles