Balozi Kazungu atoa hesabu migogoro ilivyoporomosha biashara Tanzania, Kenya

0
584

Na DERICK MILTON,BARIADI

Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu amesema biashara kati ya Tanzania na Kenya imeshuka kwa kiwango kikubwa kwa nchi zote mbili katika kipindi cha hivi karibuni kutokana na uwepo wa migogoro ya kibiashara ya mara kwa mara.

Amesema kwa miaka mitano nyuma, biashara kutoka Kenya kuja Tanzania ilikuwa na thamani ya Sh bilioni 46 kwa pesa ya Kenya (takribani shilingi za Tanzania trilioni moja) huku Tanzania kwenda Kenya ikiwa na thamani ya Sh bilioni 34 hadi 35 kwa pesa ya Tanzania.

Balozi Kazungu alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery, Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi kinachomilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Kenya.

“Biashara kutoka Kenya kuja Tanzania imepungua kutoka Sh bilioni 46 kwa pesa ya Kenya hadi kufikia bilioni 28 (sawa na shilingi za Tanzania bilioni 635) na bishara kutoka Tanzania kwenda Kenya kwa pesa ya kitanzania imeshuka hadi kufikia bilioni 20 kutoka bilioni 34 na 35,” alisema Kazungu.

Balozi huyo alisema migogoro hiyo mbali na kuwa kikwazo kwa kushuka kwa biashara, pia inahatarisha uchumi wa nchi zote mbili na wananchi wake.

Alisema Kenya ndiyo kinara wa uwekezaji Tanzania kwa Afrika.

Balozi Kazungu aliwaomba wafanyabishara kwa nchi zote mbili, viongozi na wananchi kuungana katika kutatua changamoto hiyo.

“Hii migogoro midogo midogo inatakiwa kumalizwa mara moja na haraka iwezekanavyo, haipaswi kutupotezea muda na kushusha uchumi wetu, tunatakiwa kuhangaika na mambo makubwa ya kukuza uchumi wa Kenya na Tanzania,” alisema.

Kauli ya balozi huyo imekuja ikiwa imepita takribani miezi saba tangu Rais Dk. John Magufuli na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wawaagize mawaziri wa nchi hizo mbili kutatua tofauti ndogo ndogo zinazojitokeza katika biashara.

Marais hao kwa pamoja walitoa agizo hilo walipokutana na kufanya mazungumzo Februari 23, mwaka huu katika Hoteli ya Munyonyo, Kampala nchini Uganda, muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kauli za marais hao zilikuja wakati Juni mwaka jana Serikali ya Kenya ilipiga marufuku bidhaa za Tanzania kama unga wa ngano na gesi kuingizwa nchini humo pasipo kutozwa ushuru jambo ambalo ni kinyume na makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kuna mambo madogo madogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote mawaziri wa Kenya na mawaziri wa Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogo madogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa,” alikaririwa Rais Magufuli na kuungwa mkono na Rais Kenyatta.

Kwa msingi huo, maagizo hayo yaliwalenga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya, Peter Munya.

Akisisitiza juu ya kutatua changamoto hiyo, Balozi Kazungu alisema katika kipindi cha miaka minne ambacho atafanya kazi hapa nchini, atapenda kuona kiwango cha ufanyaji wa biashara kati ya Tanzania na Kenya kinaongezeka kutoka hapa kilipo.

Zaidi balozi huyo ameahidi kuleta wawekezaji katika Mkoa wa Simiyu kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo na pamba kutokana na mkoa huo kuwa kinara wa uzalishaji wa zao hilo.

Katika hatua nyingine, balozi huyo alisema uamuzi wa Rais Magufuli wa kuanzisha mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge ni sahihi na nchi ya Kenya inaunga mkono.

Balozi Kazungu alisema mradi huo utasaidia kukuza uchumi si tu wa Tanzania bali pia wa Kenya.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza na kukuza uchumi wa viwanda, hasa kwa nchi zote mbili.

“Bila ya umeme wa uhakika bidhaa zitakazozalishwa hazitakuwa na ubora,” alisema.

Awali Meneja wa kiwanda hicho Boazi Ogola, alimweleza Balozi Kazungu kuwa kumekuwapo na changamoto ya ukosefu wa elimu kwa wakulima wa pamba kulima kisasa hali ambayo inapunguza uzalishaji wa zao hilo.

Ogola alisema kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikisaidia wakulima katika kuwapatia elimu ya kilimo cha kisasa, mbegu bora na zana za kilimo cha kisasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, alimwomba balozi huyo kusaidia kuleta wawekezaji kutoka nchini Kenya kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa zao la pamba na mifugo.

“Mkoa wa Simiyu ndiyo kinara wa uzalishaji wa pamba kwa zaidi ya asilimia 50 nchini, tumekuwa na tatizo kubwa la kuongeza thamani kwa zao hilo kutokana na kutokuwepo kwa kiwanda cha bidhaa za pamba,” alisema Mtaka.

Alisema mkoa huo uko tayari kutoa eneo bure pamoja na kusaidia kuboresha miundombinu kwa mwekezaji yeyote ambaye atakuwa tayari kujenga kiwanda cha kutatua changamoto za wakulima wa pamba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here