24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Bageni akwama kujinusuru adhabu ya kunyongwa

Kulwa Mzee

-Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Rufaa imetupilia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, SP Christopher Bageni na kubariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa na mahakama hiyo kwa sababu haikukosea kufikia uamuzi huo.

Hukumu hiyo imetolewa jana na kusomwa na Naibu Msajili Mwandamizi, Elizabeth Mkwizu, baada ya jopo la majaji watatu, Stellah Mugasha, Ferdinand Wambali na Rehema Kerefu kusikiliza hoja za pande mbili zilizowasilishwa na kuona kwamba mrufani kashindwa kuishawishi mahakama.

Bageni alipewa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuwaua kwa makusudi wafanyabiashara wanne wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi katika Msitu wa Pande, Dar es Salaam.

Akisoma uamuzi wa jopo hilo, Naibu Msajili Mwandamizi, Elizabeth alisema hakuna ubishi kwamba Bageni alikuwa ni ofisa wa polisi wa cheo cha juu na kwamba katika Msitu wa Pande alikuwepo.

Alisema hoja ya mrufani kwamba wakati wa kutiwa hatiani mahakama ilizingatia hoja mpya haina mashiko, kwa sababu hakuna kitu kipya, Mahakama ya Rufaa ni wajibu wake kuangalia kilichotokea katika ushahidi na kwa kufanya hivyo si kuleta mambo mapya.

Naibu Msajili Mwandamizi, Elizabeth alisema mahakama ilipomtia hatiani Bageni ilizingatia ushahidi wa mshtakiwa mwenzake, Koplo Rajabu Bakari na ushahidi huo uliungwa mkono na mwenendo wake baada ya tukio la mauaji.

“Koplo Rajabu alisema Bageni alikuwepo Msitu wa Pande muda wote na ndiye aliyeamuru wafanyabiashara hao wapelekwe huko.

“Wakiwa msituni, Rajabu alibakia katika gari na redio call akasikia milio ya risasi, aliifuata akakuta mtu wa mwisho anamaliziwa kupigwa risasi na Koplo Saad.

“Anasema hakusikia katika redio kwamba Bageni aliamuru wapigwe risasi, lakini aliamuru wapelekwe msituni, lakini si aliyeua.

“Ushahidi wa Koplo Rajabu uliungwa mkono na mwenendo wa Bageni baada ya tukio kwani alidanganya kwamba kulikuwa na mashambulizi ya risasi kati ya polisi na majambazi wakati baadhi ya mashahidi walisema hapakuwa na mashambulizi hayo.

 “Bageni aliamuru askari wawili waende baharini kufyatua risasi tisa na kisha alichukua maganda na kudai yalipatikana Sinza katika mashambulizi.

 “Mtu yeyote anayedai mahakama ilikosea kufikia uamuzi alitakiwa yeye athibitishe madai hayo, kwa mazingira hayo mrufani kashindwa kuishawishi mahakama kuona kwamba ilikosea kufikia maamuzi hayo, hakuna namna nyingine zaidi ya kutupilia mbali maombi ya mrufani,” alimaliza kusoma Naibu Msajili.

Mrufani aliyewakilishwa na wakili wake Gaudioz Ishengoma, aliwasilisha maombi ya marejeo dhidi ya  hukumu iliyotolewa Septemba 13 na kusomwa Septemba 16 mwaka 2016 na aliyekuwa Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza.

Mleta maombi alitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo na jopo la majaji watatu, Jaji Benard Luanda, Sauda Mjasiri na Senistocles Kaijage.

Akiwasilisha sababu mbili za kuomba marejeo, Ishengoma alidai mteja alinyimwa haki ya kusikilizwa wakati wa kutathmini ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa kuegemea tu kwenye ushahidi wa upande wa mashtaka.

Alidai katika kuchanganua ushahidi ambao uamuzi wa mahakama uliegemea, mahakama ilishughulika na ushahidi wa msingi (Exam in Chief) wa upande wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu ushahidi wa utetezi, hususan wa Bageni au haikuutazama kabisa.

Ishengoma alidai mahakama ilimtia hatiani mrufani kwa hoja ambazo hazikujadiliwa wakati wa usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na Jamhuri, wakipinga Mahakama Kuu kuwaachia huru washtakiwa.

 “Mahakama Kuu ilisema kwamba washtakiwa wote walikuwepo msituni, lakini mahakama haiwezi kumtia hatiani mtu aliyesaidia mauaji na kumwacha aliyeua, hivyo inawaachia huru,” alidai.

Alidai Mahakama Kuu ilisema kosa la kuua na kosa la kusaidia kuua ni makosa mawili tofauti, si sahihi kwa mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji kutiwa hatiani kwa kosa jingine ambalo tangu mwanzo mshtakiwa alitakiwa kulijua ili aweze kujitetea.

Ilisema makosa hayo si makosa yanayofanana, hivyo mahakama hiyo ilitofautiana na hoja za upande wa Jamhuri kwamba washtakiwa watiwe hatiani kwa kosa la kusaidia kuua baada ya kushindwa kutiwa hatiani kwa mauaji.

 “Jamhuri katika sababu za kukata rufaa walitaka washtakiwa wote watiwe hatiani kwa sababu walionekana wote walikuwepo msituni Pande.

“Mahakama badala ya kujikita katika eneo hilo, yenyewe ilijiuliza maswali kwamba walienda Pande kufanya nini, walipelekwa na nani, hoja ambazo hazikuwepo katika sehemu ya mabishano, mrufani alijikita kujibu sababu za rufaa na si maswali yaliyoibuliwa na mahakama,” alidai.

Alidai katika utetezi wake, Bageni alisema hakwenda msituni, lakini mahakama ilipochambua ushahidi iliangalia ushahidi wa upande wa Jamhuri na kuacha utetezi wa mshtakiwa na haikusema chochote kuhusu utetezi huo.

Akizungumzia sababu ya pili ya kuomba marejeo, alisema kulikuwa na dosari ya wazi katika kumbukumbu za mahakama.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya, akijibu hoja za mleta maombi, alidai anapinga maombi yaliyowasilishwa na kwamba mleta maombi alisikilizwa sana.

Bageni alikuwa mshtakiwa wa pili na katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati mwaka 2009 wote waliachiwa huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo, hivyo alikata rufaa dhidi yao katika rufaa namba 358 ya mwaka 2013.

Kabla ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP aliwaondolea rufaa wajibu rufaa watano na kubaki wajibu rufani wanne ambao waliachiwa huru pia Septemba 16 mwaka huu.

Walioachiwa huru ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle na Rajabu Bakari baada ya mahakama kuona hakuna ushahidi wa wazi ama mazingira kuwatia hatiani.

Katika kesi ya msingi, Bageni alidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese , Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande Mbezi Luis akahukumiwa kunyongwa hadi kufa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles