30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Aweso: waliokula fedha za mradi wa maji ukarawa watazitapika

Na Elizabeth Kilindi, Njombe

Naibu Waziri wa maji na umwagiliaji nchini Jumaa Aweso, ametangaza kiama kwa watakaobainika kula fedha za mradi wa maji wa kijiji cha Ukarawa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe akisema watazitapika.

Aweso alitoa kauli hiyo jana katika ziara yake Mkoani Njombe ambapo akiwa halmashauri ya wilaya ya Njombe alisomewa taarifa na mhandisi wa maji, Rajabu Yahaya na kushindwa kumueleza kilichosababisha mradi wa Ukarawa kutotoa maji tangu ukamilike.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ukarawa baada ya kukagua mradi huo ambao umekamilika lakini hautoi maji na zaidi serikali ikiwa imekwishamlipa mkandarasi milioni 532, Aweso alisema lazima ifike hatua watu waogope fedha za miradi ya maji.

Mradi huo wenye thamani ya  milioni 562, ulilenga kutatua adha ya maji kwa wakazi wa vijiji vya Ukarawa na Kitole .

‘’Mradi huu ni wa miaka mingi wakati mwingine mnasababisha mama zetu wanashindwa kupaka mafuta wala poda kutokana na kukosekana kwa maji.

‘’Wakati mwingine mambo hayawezi kwenda sawa,lazima ifike hatua tusioneane haya..haiwezekani miaka yote maji hakuna na fedha tayari zimeshalipwa’’alisema

Aweso pia aligundua matumizi mabaya ya fedha za kuendeshea mradi na ameagiza aliyekuwa mhandisi na mkandarasi wa mradi huo aitwe kutolea maelezo ya fedha ambazo hazijulikani zilipo.

“Jambo la msingi tunapotoa milioni 562 tulitegemea wananchi hawa wapate maji..tuna vituo zaidi ya 13 napata taarifa Kitole hakuna hata kituo kimoja kinachotoa maji sasa mimi ninachokuomba mhandisi wa maji wewe huwezi kuachiwa mradi lazima umeachiwa na fedha…na nikuagize mhandisi ambaye alikuwa anasimamia mradi huu Johakim Sanga mpigie simu aje asubuhi kwa Mkuu wa Mkoa na lazima nichukue hatua”alisema Aweso.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Lupembe,  Joram Hongoli alisema mradi huo umechukua muda mrefu bila mafanikio.

‘’Mbaya zaidi katika kijiji cha Kitole hadi hatua hii hakuna hata tone moja la maji lililotoka’’alisema Hongoli.

Katika ziara hiyo Aweso amekagua mradi  maji wa Ihang’ana ambao nao hakuridhishwa na ujenzi wa tanki lake.

Katika kijiji cha Kidegembye, Aweso alieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi inayoendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles