24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Aston Villa wavunja benki kwa Samatta

LONDON, ENGLAND

MSHAMBULIAJI wa klabu ya KRC Genk na timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta, yupo katika hatua za mwisho kumalizana na klabu ya Aston Villa kwa uhamisho wa kitita cha Euro milioni 10, zaidi ya bilioni 25 za Kitanzania.

Samatta mwenye umri wa miaka 27, anatakiwa kusajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya kuziba nafasi ya mshambuliaji Wesley Moraes ambaye amepata majeruhi ya goti.

Majeruhi ya Moraes yatamfanya kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, hivyo Aston Villa wamefikia makubaliano na Samatta kwa ajili ya kumsajili.

Kwa sasa klabu hiyo ipo nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Ligi nchini England, sehemu ya kushuka daraja, hivyo wanaamini wakiinasa saini ya mshambuliaji mwenye uwezo atawasaidia kubakia kwenye ligi.

Jana asubuhi mchezaji huyo aliungana na wachezaji wenzake wa KRC Genk, lakini mchana aliondoka na inadaiwa kwenda kumalizana na klabu hiyo ya Aston Villa.

Dili hilo likikamilika itakuwa Samatta ametimiza ndoto zake za kucheza soka la kulipwa katika Ligi Kuu nchini England na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi hiyo.

Samatta amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Genk tangu ajiunge mwaka 2016 ikiwa pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini Ubelgiji msimu uliopita.

Amecheza jumla ya michezo 191 kwa kipindi cha misimu minne amefunga jumla ya mabao 76 na kupiga pasi 20 za mwisho

Msimu huu bado amekuwa kinara wa kupachika mabao kwenye klabu yake akiwa amefunga jumla ya mabao saba.

Moja ya sababu ambayo inawafanya Aston Villa waweke ofa yao ni kitendo cha mchezaji huyo kuonesha kiwango kizuri msimu huu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akipachika bao kwenye mchezo dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool huku Genk ikipoteza kwa mabao 2-1 hatua ya makundi.

Japokuwa Samatta atafanikiwa dili hilo, lakini anaweza kukutana na kikwazo cha kibari cha kufanyia kazi kutokana na jinsi Tanzania ilipo kwenye viwango vya FIFA. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 134.

Urahisi unaweza kuwepo kutokana na mchezaji huyo kumaliza kinara wa mabao msimu uliopita kwenye Ligi Kuu nchini Ubelgiji pamoja na kutwaa tuzo ya mchezaji bora mwenye asili ya Afrika anayecheza soka la kulipwa Ubelgiji (Soulier d’Ebene).

Majira ya joto msimu uliopita Samatta alikuwa anawindwa na klabu mbalimbali ikiwa pamoja na West Ham, Newcastle, Lyon na zingine nyingi, lakini hakuwa tayari kuondoka kwa kuwa lengo lake kubwa lilikuwa kucheza Ligi ya Mabingwa, baada ya kutimiza ndoto hizo ameona huu ndio muda wake sahihi wa kuondoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles