24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Assah Mwambene ang’olewa Maelezo

assahNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel, amemteua Zamaradi Kawawa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo).

Taarifa iliyotolewa  kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema hatua hiyo imetokana na aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, kuhamishiwa Wizara ya Mambo Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,  atakakopangiwa majukumu mengine.

Zamaradi alikuwa Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya uratibu wa mawasiliano serikalini wa wizara hiyo.

Assah Mwambene aliteuliwa Agosti, 2012 kuwa mkurugenzi wa idara hiyo na alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Clement Mshana ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Tanzania(TBC).

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Ashukuru

Akizungumzia  mabadiliko hayo, Mwambene alisema  alipata fursa ambayo wengine hawakuipata kwa   miaka minne.

“Namshukuru Mungu kwa nafasi hiyo na ninamshukuru Mheshimiwa Rais aliyeona kwamba naweza kumsaidia katika eneo hilo na kwa sasa niko tayari tena kwa furaha kutimiza wajibu wangu kwa   nafasi nyingine.

“Nawashukuru nyote kwa ushirikiano mlionipatia nikiwa katika nafasi ya ukurugenzi. Nitaendelea kuwa mtumishi wa umma mwaminifu katika nafasi nitakayopewa kufanya.

“Mwisho nimepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wakurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) akiwemo  Raphael Hokororo, Jamal Zuberi, Vicent Tiganya na Zamaradi Kawawa.

“Nimejifunza mengi kwao pamoja na uongozi wa wizara. Nilianza kuonja utendaji kazi uliotukuka wa Mhe Nape Nnauye na Katibu Mkuu, Profesa Elisante ole Gabriel,” alisema Mwambene.

Yakukumbukwa kwa Assah

Septemba 27,  2013, Serikali kupitia Msajili wa Magazeti wa wakati huo, Assah Mwambene, ilitoa tangazo la kufungiwa kwa magazeti la ya MTANZANIA na Mwananchi.

Magazeti hayo yalifungiwa  kwa kile kilichodaiwa ni mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha amani na mshikamano  nchini.
Gazeti la MWANANCHI lilifungiwa kutochapishwa kwa  siku 14 kuanzia 27 Septemba 2013.

Kwa upande wa gazeti la MTANZANIA, Mwambene  alilifungia  kutochapishwa kwa siku  90 kuanzia Septemba 27, 2013 kwa madai ya kuchapisha habari zenye uchochezi.
Julai 30,2012, Serikali ilitangaza kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la kila wiki la Mwanahalisi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuandika habari na makala za uchochezi.

Mbali na hilo pia alisimamia kufungiwa kwa gazeti  jingine la kila wiki la Mawio kwa kile kilichodaiwa kuandika habari za uchochezi kuhusu uchaguzi wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles