25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Shoo: Msijipatie fedha kwa njia ya aibu

Upendo Mosha -Siha

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amewaonya wachungaji, watumishi na waumini wa kanisa hilo wasijifanye mabwana, na wasitake kujipatia fedha kwa njia za aibu.

Aliyasema hayo juzi, wakati wa ibada maalumu ya kumstaafisha mchungaji wa kanisa hilo na kuwaingiza kazini baadhi ya wachungaji katika Usharika wa Oshara, Jimbo la Siha, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.

Alisema kujipatia fedha kwa njia za aibu ni jambo ambalo halipendezi na ni chukizo mbele za Mungu.

NENO LA SHUKRANI

Akitoa neno la shukrani baada ya kuchaguliwa kuliongoza tena kanisa hilo, Dk. Shoo alisema; “imempendeza Mungu kuliongoza kanisa hilo kwa kipindi kingine cha miaka minne, na kwamba uchaguzi ulifanikiwa kutokana na maombi na si kwa nguvu zake mwenyewe.

“Nimshukuru mwenyezi Mungu kwakuwa yeye ametutendea mambo makuu sana… Mungu kwetu ni kimbilio la nguvu, tena msaada utakaoonekana wakati wa mateso, hakika tumeona mkono wake Mungu na uweza wake.

“Mungu alisema hata kama maadui wakijiinua namna gani yeye aliahidi atatuokoa… napenda kuwashukuru wana KKKT wote kwa maombi yenu na ushirikiano wenu na mshikamano wenu, maana hata katika hili tulilolisikia mkutano mkuu, mlinionyesha mshikamano… Mungu awabariki.”

Dk. Shoo aliwataka viongozi wa dini na Wakristo nchini kusimama pamoja na kuzingatia wito wa Mungu ili kuendelea kuwa kielelezo duniani.

“Tuelewe wito huu kwa unyenyekevu, kila mmoja ameitwa kwa nafasi yake… kipekee sisi ambao tumepewa dhamana ya kulichunga kundi la Bwana, tunapaswa kulichunga kwa uaminifu wote kwa bidii na kwa moyo wa upendo na unyenyekevu,” alisema.

WAKATI MWAFAKA

Mchungaji mstaafu wa kanisa hilo, Jeremiah Kileo, alisema ni wakati mwafaka wa waumini kusimama imara na kuliombea kanisa hatua ambayo itasaidia kuepusha changamoto mbalimbali zinazohusu shetani.

“Kwa umoja wetu tunapaswa kuliombea kanisa ili tusiyumbishwe na yule adui muovu shetani. Pia tusimamie imani zetu bila kuyumbishwa,” alisema.

Dk. Shoo alitangazwa mshindi usiku wa kuamkia juzi dhidi ya wagombea wengine katika uchaguzi huo na ataliongoza kanisa kwa kipindi cha miaka minne.

Alipata kura 144, huku mshindani wake wa karibu, Dk. Abednego Keshomshahara akipata kura 74 kati ya 218 zilizopigwa mzunguko wa mwisho baada ya kubaki wao wawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles