23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Mkuu TAG apiga marufuku siasa makanisani

*Atangaza kuchukua hatua kwa wachungaji watakaokiuka 

*Askofu Kanisa Katoliki aonya uzazi kwa vijana

Safina Sarwatt -K’njaro CLARA MATIMO -MWANZA

KANISA la Tanzania Assemblies of God (TAG), limepiga marufuku siasa katika makanisa yake nchini na kwamba madhabahu hayo yatumike kuhubiri injili na kuliombea taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Askofu Mkuu wa TAG Tanzania, Dk. Barnabas Mtokambali, wakati wa uzinduzi wa Kanisa la TAG Kilimanjaro Temple Revival mjini Moshi jana.

Askofu Dk. Mtokambali alisema kamwe makanisa ya TAG nchini kote, hayataruhusu madhabahu yake kutumika kufanya siasa aina yoyote na kwamba atakayehusisha kanisa hilo kwa jambo lolote la kisiasa atachukuliwa hatua.

Alisema kusudi la kuanzishwa kanisa hilo ni kulihubiria taifa kukemea maovu.

“Ni marufuku kutumia madhabahu ya kanisa kufanya jambo lolote la kisiasa, mimi kama mkuu wa kanisa, sitalifumbia macho wala sitaruhusu,” alisema.

Alisema nyumba ya bwana ni mahali patakatifu, hivyo ni vema kanisa likahubiri kweli na haki.

“Ukweli na haki inatuweka huru taifa, wachungaji wenzangu tendeni haki, hubirini amani, simameni katika haki, tukifanya hivyo na kufuata miiko yetu, tutajenga taifa bora,” alisema.

Alisema kanisa likisimamia kweli na kuacha kujiingiza katika mambo yanayohusiana na siasa, watakuza  uchumi na elimu ya taifa.

“Kweli huleta amani na upendo na kuondoa chuki baina ya watu na watu, pamoja na viongozi mbalimbali,” alisema Askofu Dk. Mtokambali.

Alisema yapo mambo mengi ambayo taifa linapitia na kanisa likisimama katika nafasi yake ya kuliombea, litasimama imara.

Naye Meya wa Manispaa ya Moshi, Ryamod Mboya, alisema kanisa lina nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi, ndiyo maana siku zote Serikali inashirikiana nalo kuleta maendeleo kwa wananchi.

Alisema kanisa likisimama kuhubiri haki na amani, taifa litapiga hatua kubwa kimaendeleo.

Akisoma risala, Albert Mruma alisema ujenzi wa kanisa hilo umegharimu zaidi ya Sh bilioni 2.5 fedha ambazo ni michango ya waumini na wadau mbalimbali.

ASKOFU NKWANDE

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus  Nkwande, amesema ubinafsi ulioingia ulimwenguni na kuwakumba binadamu, umewafanya wamsaliti Mungu na kuacha kushiriki uumbaji kwa kuzaa idadi ndogo ya watoto.

Askofu Nkwande alisema hayo jijini Mwanza jana, akihubiri wakati wa misa takatifu ya Jumapili kabla kutoa sakramenti ya kipaimara iliyofanyika Kanisa la Mtakatifu Monika, Parokia ya Buhongwa.

Alisema wanadamu wengi katika karne hii wakiwamo wafanyabiashara, hawazai  watoto zaidi ya watatu kwa kisingizio cha maisha magumu, wakati  kitendo hicho ni kukataa kumtolea Mungu matoleo.

“Ubinafsi uliopitiliza umewafanya binadamu wamesahau kumtolea Mungu matoleo ya watoto, vijana wa leo wanazaa wakiwa na miaka 30 na kuendelea, ukiwauliza kwanini umekawia kuzaa, jibu wanalotoa ni maisha magumu.

“Mama yangu alinizaa akiwa na umri wa miaka 17, alikuwa akija kunisalimia shuleni wanafunzi wenzangu wanadhani ni dada yangu.

“Karne hii, vijana wengi wamejiingiza katika matumizi ya dawa za kuzuia uzazi, hii ni dhambi kwa sababu ni kikwazo cha matoleo ya Mungu, acheni kutumia hizo dawa, hata hao waliozileta saizi wanajuta, maana kwenye nchi zao hawana watoto, wanapokuja huku kwetu msidhani wanakuja kutalii kwa kuangalia wanyama, wanakuja kuona watoto tulionao ili kufurahisha mioyo yao kwa kuwa kwao hawapo.

“Ndugu zangu, tumwombe mwenyezi Mungu atujalie tuweze kubadilika, dhambi imezidi ulimwenguni, leo hii nchi za wenzetu, kuna ndoa za jinsia moja na hapa kwetu baadhi  ya watoto wetu wanashiriki mapenzi ya jinsia moja, wengine kinyume cha maumbile.

“Nasema haya mbele yenu watoto ambao leo mtapata sakramenti ya Kipaimara ili mjihadhari, ogopeni kutenda dhambi, tambueni mshahara wa dhambi ni mauti.

“Wazazi tujiulize tumekosea wapi, naamini baadhi ya wazazi na walezi hatutimizi wajibu wetu wa malezi kwa watoto.

“Niliwahi kuwauliza watoto wa kiume wanaojihusisha na ushoga, wengi wao waliniambia walianza vitendo hivyo wakiwa darasa la tatu, inaumiza. Naamini wazazi wao wangekuwa karibu nao yawezekana wangebaini mapema na wangewasaidia kubadilika,” alisema.

Aliwataka wazazi wa kiroho na mwili wa watoto ambao walipata sakramenti ya kipaimara kuwalinda na kuwalea vizuri ili nao wawaokoe wengine kwa kuwafundisha matendo mazuri.

Kwa mujibu wa Katekista Devota Gaspary, watoto  262 walipata sakramenti hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles