30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU MALASUSA ASIPOANGUKA, ATAANGUSHWA


Na EVANS MAGEGE       |   

ASKOFU Dk. Alex Malasusa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, amewakasirisha wakubwa wenzake, wamemnunia na sasa wameamua kumtenga.

Ndani ya maisha ya kutengwa na wakubwa nayaona mapito ya Askofu Malasusa kwenye njia nyembamba, ngumu na yenye majaribu ya hali ya juu.

Nayaona mapito yake kwa sasa yapo chini ya amri ya kutumikia miezi mitatu ya kuhakikisha anamaliza safari yake ya kujitafakari kuhusu sababu zilizowalazimu wakubwa wenzake ndani ya kanisa hilo wakasirike na kumnunia kwa kiwango hicho.

Wamemwamuru kupita njia nyembamba, yenye ukimya mwingi ili apate wasaa mzuri wa kujitafakari juu ya kile kilichomponza hadi awachukize wenzake.

Michomeko ya fikra zangu inatanabaisha kwamba hao wakubwa wenzake, namaanisha Baraza la Maaskofu wa KKKT, ambalo limeketi hivi karibuni na kuchukuwa uamuzi wa kumtenga.

Mtego mkubwa kuliko yote uliopo ndani ya njia hiyo nyembamba waliyomwamuru kupita ni matope ya utelezi wa udongo wa mfinyazi ambayo hata kama atamudu kupita bila kuteleza, matope yatamrukia na bila shaka yatachafua kanzu yake ya utume aliyotunukiwa kuwa mlishi wa kondoo wa Bwana.

Kanzu ambayo huvaliwa na wachache kati ya wengi walioteuliwa na Bwana, yenye mvuto wa aina yake kwa nakshi nzuri za maua ya rangi mbalimbali yakiwamo yale ya mng’ao wa dhahabu.

Washadadia ubazazi nao hawakosi la kunong’ona. Kwa nyakati tofauti tangu uamuzi wa wakubwa uchukuliwe dhidi ya Askofu Malasusa, wamenidokeza kwamba, utelezi uliowekwa kwenye mapito yake safari hii ni wa hali ya juu ukilinganisha na changamoto mbalimbali alizowahi kukumbana nazo na kuzishinda kwa nyakati tofauti huko nyuma.

Kuna ubazazi mwingine unadai kwamba, kabla ya wakubwa hao kumchukulia hatua ya kumtenga, Askofu Malasusa aliwaomba radhi lakini kwa kumtambua kuwa yeye ni jemedari wa vita, hawakumkubalia moja kwa moja badala yake wakamwambia akae kando kwa miezi mitatu ili apate muda wa kujitafakari kisha aombe radhi waumini wake.

Kwa uchokonozi wa mambo ushauri huo unaonekana ulikuwa ni mchomeko wa nguvu wa kuhakikisha askofu huyo hapenyezi ushawishi wa kupangua ile hoja inayotafsirika kuwa ni ya ‘usaliti’ wa maazimio ya wakubwa wenzake akiwamo yeye mwenyewe.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Askofu Malasusa amepangua mishale mingi ndani ya mapito yake huko nyuma. Kumbukumbu zinaonyesha alipata kuchafuka kwa matope kiasi cha kutotamanika lakini alituliza nafsi akaoga, akang’aa na akaendelea na safari ya ulishi wa kondoo wa Bwana kama kawaida.

Pamoja na mikwamo na tuhuma dhidi yake, hata hivyo alifanikiwa kuibuka mshindi kati yao kwa kuchaguliwa kuwa mkuu wa nafasi ya juu kabisa ya kanisa hilo nchini.

Kwa historia hiyo, mtazamo wangu unanielekeza kuwa wakubwa wenzake safari hii wameamua kumwamuru atumie njia ambayo hajawahi kuipita yenye tope zito, vikwazo, vitisho na majaribu mengi kwa lengo la kuhakikisha anateleza na kuanguka, kama hataanguka, ataangushwa hata kama hataanguka, kanzu yake ya thamani itachafuka kwa sababu ya mpepesuko wa kukanyaga tope jingi lililotuama kwenye mapito yake.

Naona wakubwa wenzake wameamua kumtwika zigo la majaribu mengi katika safari yake ya miezi mitatu ya kujitafakari.

Na wamefanya hivyo kwa makusudi tu ili kuivuruga saikolojia yake ishindwe kutambua matumizi ya ‘bawabu na bawaba’ katika utumishi wa kanisa hilo.

Ninachokiona katika hoja hiyo ni kwamba, sababu ya wakubwa kufanya hivyo ni kuchokoza sauti za watu walio nje ya mfumo wa kanisa wamtetee ili ipatikane sababu ulinganisho wa tuhuma zilizojaa mawazoni mwa watu hususani waumini wa kanisa hilo kuwa Askofu Malasusa hakuwa mwenzao kwa dhati katika ulishi wake kwa wanakondoo.

Hapa namaanisha kuwa ipo dhana fikirishi inayodai aidha ni busara au urafiki alionao na watu wengi umekuwa na ushirika mkubwa na mwenendo wa washirika wa siasa jambo ambalo sidhani ni baya, lakini baadhi ya wanakondoo wanadai kuwa linapausha sura pana ya kanisa machoni mwa watu.

Ukiangalia kwa kina sababu za kutengwa kwake ni hoja ya kuzuia waraka wa Pasaka usisomwe katika dayosisi yake.

Nakumbuka waraka huo uliibua mjadala mkubwa kutokana na muktadha wa maudhui yake kuonekana kuishambulia Serikali iliyopo madarakani.

Baada ya uamuzi wa wakubwa wenzake, kwa sasa Askofu Malasusa anaonekana kama kavishwa kengele ya ‘usaliti’ dhidi ya azimio la wakubwa wenzake kila kona sakata lake limekuwa gumzo.

Wapo wanaodai, uamuzi wa wakubwa wenzake kumtenga ni sawa na kuitenga Dayosisi yote ya Mashariki na Pwani.

Kutokana na mitazamo hiyo, swali la kujiuliza je, washarika wa dayosisi anayoiongoza watamuunga mkono katika kipindi hiki cha kutengwa mpaka hapo muda wa miezi mitatu utakapotimia?

Je, wapo tayari kumsamehe kwa tuhuma alizotuhumiwa kama ikitokea akawaomba radhi?

Hakuna ubishi kuwa kutengwa kwa askofu huyo ni sawa na kutengwa kwa dayosisi nzima, je, watakuwa tayari kuishi maisha ya kutengwa?

Mwisho Askofu Malasusa anaushawishi wa kiwango gani cha kuweza kujisafisha dhidi ya tuhuma nzito alizopewa na wakubwa wenzake? Wakati tukiyatafakari hayo macho na masikio yameelekezwa kwa washarika wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, kwa maana nyingine wao ndio wameshika mpini.

Kwa maoni 0718-814925

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles