23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu asimulia mgawo wa Escrow

Nzigilwa-bishopNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

HATIMAYE Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, amevunja ukimya na kusimulia namna alivyopokea Sh milioni 40.4 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engireering & Marketing Ltd, James Rugemalila.
Fedha hizo, ni sehemu ya kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Askofu Nzigilwa ni mmoja wa watu waliotajwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), mwaka jana kuwa alipokea kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake iliyopo Benki ya Mkombozi jijini Dar es Salaam.
Alisema fedha hizo ziliwekwa na James Rugemalila, kwa ajili ya matoleo na shughuli za kikanisa.
Taarifa iliyotolewa na Askofu Nzigilwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema siku zote amekuwa akishirikiana na Rugemalila katika masuala mbalimbali yakiwamo ya kifamilia, kikanisa na kijamii tangu alipokuwa katika Parokia ya Makongo Juu.
“Katika moja ya mawasiliano yetu mwanzoni mwa Februari, mwaka jana, Rugemalila aliniomba nimpatie namba yangu ya akaunti Benki ya Mkombozi ili aweke matoleo yake.
“Kiasi alichodhamiria kutoa nilikuwa sikifahamu hadi pale nilipokwenda kuona taarifa zangu za fedha na kuona VIP imeniingizia Sh milioni 40.4 katika akaunti yangu,” alisema.
Askofu huyo alisema baada ya kuingiziwa fedha hizo aliwasiliana na Rugemalila kwa mshangao kuhusu kiasi hicho kikubwa cha fedha.
“Aliniambia kwamba amekitoa kwa ajili ya matoleo yake ambayo yangesaidia shughuli za kitume na kichungaji.
“Kwa kweli nilimshukuru kwa ukarimu wake mkubwa, kutokana na matoleo hayo kutolewa na mtu anayefahamika kwa ukaribu wake katika kusaidia kanisa na watumishi wake,” alisema.
Alisema hakuwa na shaka ya kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalila kutokana na ambavyo anafahamu uwezo wake wa kiuchumi.
“Ni desturi ya kawaida waumini kutoa michango na matoleo mbalimbali kwa kila mmoja kwa uwezo na ukarimu wa moyo wake… matoleo ya waumini huhusika katika shughuli za uinjilishaji, parokia na taasisi zake, ikiwamo kutumika katika miradi maalumu iliyokusudiwa na matoleo hayo na pia hutumika kwa matakwa na malengo ya mtoaji,” alisema.
Askofu Nzigilwa alisema alipokea matoleo hayo kwa roho safi na moyo mweupe kama ambavyo siku wamekuwa wakifanya pindi wanapokea zawadi.
“Tangu matoleo hayo yalipopokewa Februari 2014, hakuna mamlaka yoyote iliyowahi kuniuliza kuhusu jambo hili,” alisema.
Tamko la Askofu Nzigilwa, limekuja wiki mbili baada ya Rais Jakaya Kikwete kuhutubia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Desemba 22, mwaka jana, ambapo alitangaza kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Profesa Tibaijuka alifutwa kazi baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka maadili ya uongozi baada ya kuingiziwa katika akaunti yake binafsi Sh bilioni 1.6, zikiwa ni sehemu ya fedha zilizochotwa katika akaunti hiyo.
Siku moja baada ya mkutano huo ofisi ya Rais Ikulu, ilitangaza kumsimamisha kazi Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ili kupisha uchunguzi dhidi yake kuhusu sakata hilo.
Hata hivyo, katika mkutano huo, Rais Kikwete alimweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa maelezo kwamba uchunguzi dhidi yake haujakamilika na kuahidi kumchukulia hatua baada ya kujiridhisha na tuhuma zake.
Rais Kikwete katika kutimiza maazimio manane ya Bunge, alisema atashughulika na viongozi wa Serikali kwa kuwa wanawajibika katika suala la maadili huku kwa upande wa viongozi wa dini, alisema hana mamlaka nao.
Askofu mwingine anayetuhumiwa kupokea fedha za Escrow ni Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini ambaye anadaiwa kupokea Sh milioni 80.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles