31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ashambuliwa na simba kwa mama lishe

NA HADIJA OMARY

LINDI

MKAZI wa Kata ya Rutamba wilayani Lindi, Kizito Mgogo (59), amelazwa Hospitali ya Sokoine mkoani hapa baada ya kushambuliwa na simba usiku.

Akizungumza na MTANZANIA hospitalini hapo, mdogo wa majeruh huyo, Michael Mathei, alisema kaka yake huyo ambaye ni mgonjwa wa akili, alipatwa na mkasa huo Aprili 26, mwaka huu kati ya saa 5 na 6 usiku akiwa amejilaza katika kibanda cha mama lishe.

Alisema Mgogo akiwa anarejea nyumbani kwake, alipofika katika eneo la Namatili, alikuta kibanda hicho kilichokuwa kimezungushiwa fito na kukandikwa kwa udongo upande mmoja na akaamua kuingia na kulala.

Mathei alisema kaka yake akiwa kwenye usingizi, simba wawili waliokuwa kwenye mawindo yao wakikimbiza mbwa bila mafanikio, walipofika katika kibanda cha mama lishe walisimama na kisha kuangalia kilichopo ndani.

Alisema simba hao baada ya kubaini kuwa ndani ya kibanda kuna kitu, mmoja wao alipitisha mkono kupitia matundu ya fito na kucha zake zilifika kati ya tumbo na kifua cha ndugu yake ndipo aliposhtuka na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada.

“Kutokana na kelelealizokuwa akipiga kaka, simba waliamua kuondoka, huku wakimaacha akiendelea kuvuja damu zilizotokana na kubanwa na kucha za simba.

“Walifika wasamaria wema na kumkuta akiwa ana majeraha ndipo walimchukua hadi Kituo cha Polisi Rutamba ambako alipewa fomu namba tatu (PF3) na kumkimbiza Kituo cha Afya cha Rondo, lakini kutokana na majeraha yake mganga wa kituo hicho aliandika rufaa na kuhamishiwa Hospitali ya Sokoine,” alisema.

Mmoja wa madaktari wanaompatia matibabu mgonjwa huyo, Dk. Ernest Muhando, alisema walimpokea akiwa na majeraha kifuani na tumboni kutokana na kujeruhiwa na simba.

Naye Ofisa Maliasili Wilaya ya Lindi, Victor Shau, aliiambia MTANZANIA kuwa tayari wameshawasiliana na uongozi wa kijiji pamoja na kuwaomba wananchi wanaoishi maeneo yanayokaribiana na Msitu wa Rondo, kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wa maisha yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles