25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

ARGENTINA HATARINI KUKOSA KOMBE LA DUNIA

BUENOS AIRES, ARGENTINA

TIMU ya Taifa ya Argentina, ipo hatarini kukosa kushiriki michuano ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi baada ya mchezo wao wa juzi wa kuwania kufuzu kutoka suluhu dhidi ya wapinzani wao Peru.

Kwa hatua waliyofikia, Argentina wanahitaji kushinda mchezo mmoja uliobaki ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki, lakini wakishindwa kufanya hivyo basi wataingia kwenye historia mpya kwa mara ya kwanza kutoshiriki michuano hiyo tangu mwaka 1970.

Bara la Amerika ya Kusini timu tano zinatakiwa kufuzu Kombe la Dunia, tayari kuna baadhi ya timu ambazo zimeanza kuonesha dalili ya kufuzu ikiwa ni pamoja na Brazil ambao wanaongoza wakiwa na pointi 38, wakifuatiwa na Uruguay wenye pointi 28, Chile pointi 26, Colombia pointi 26 na Peru wakiwa na pointi 25.

Hata hivyo, Argentina wana pointi 25, jambo ambalo linawapa wakati mgumu wa kufuzu kwa kuwa wanalingana pointi na wapinzani wao Peru, lakini wapinzani mwingine ambao wanakutana na Argentina ni Paraguay wenye pointi 24, hivyo kama watashinda mchezo unaofuata na Argentina wakapoteza pamoja na Peru, basi Paraguay watakuwa wanafuzu huku wapinzani hao wakibaki.

Argentina wanaweza kuishangaza dunia endapo watashindwa kufuzu Kombe la Dunia, ikiwa miaka mitatu iliyopita katika fainali zilizofanyika nchini Brazil walifanikiwa kufika fainali dhidi ya Ujerumani.

Katika mchezo huo wa juzi, mshambuliaji wa timu hiyo, Lionel Messi, alijaribu kupambana kuhakikisha wanapata ushindi, lakini mambo yalikuwa magumu japokuwa shuti lake lilikwenda kugonga mwamba na kutoka nje.

Baada ya mchezo huo kumalizika, wachezaji wa Argentina walionekana kukata tamaa wakitoka nje na vichwa wameinamisha chini, lakini bado mashabiki wao walionekana kuwa na imani na mchezo wa mwisho wiki ijayo dhidi ya Ecuador, mchezo huo Argentina watalazimika washinde ili kujihakikishia kufuzu.

Timu nyingine ambazo zimejihakikishia kufuzu ni pamoja na mabingwa watetezi Ujerumani baada ya kuwachapa wapinzani wao, Ireland Kaskazini mabao 3-1 mjini Belfast. Timu nyingine ni England baada ya kuichapa Slovenia bao 1-0, lililowekwa wavuni na nahodha ambaye ni mshambuliaji wao, Harry Kane, katika dakika ya 90.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles