24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

AMWOMBA RAIS MAGUFULI AMSADIE FIDIA YA KIFO CHA MKE WAKE

Na Aziza Masoud – Dar es Salaam

MKAZI wa Mbezi Dar es Salaam, Prosper Mkumbi, amemwomba Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati kwa kulitaka Shirika la Elimu Kibaha kumlipa fidia ya Sh milioni 200 kwa amri ya mahakama baada ya Hospitali ya Tumbi kufanya uzembe na kusababisha kifo cha mke wake, Martina Mkumbi mwaka 1998.

Malipo ya fidia hiyo yametokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Juni 2014 baada ya mlalamikaji kupeleka malalamiko dhidi ya shirika hilo na kuomba fidia ya usumbufu baada ya mke wake kufariki Novemba 24, 1998 mara tu baada ya  kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Tumbi ambako alikwenda kujifungua.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Mkumbi alisema mke wake alifikishwa hospitalini hapo Novemba 23 na hospitali hiyo ilishauri afanyiwe upasuaji ili aweze kujifungua hatua ambayo ilisababisha umauti wake.

Mkumbi ambaye ni mfanyabiashara, alisema baada ya kifo hicho, alisafirisha mwili wa mke wake kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kwa kufanya shughuli za mazishi Novemba 26.

“Baada ya kuzika nilirudi mjini na kuendelea na biashara zangu, lakini baada ya mwaka mmoja nikasikia kwenye redio Wizara ya Afya ikatangaza kumtia hatiani daktari mmoja baada ya kusababisha kifo cha mjamzito kwa uzembe na lilitajwa jina la mke wangu,” alisema Mkumbi.

Alisema baada ya kusikia habari hizo katika vyombo vya habari, alilazimika kwenda Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii kwa wakati huo kutafuta nakala ya hukumu iliyomtia hatiani daktari huyo na baadae mwaka 2002 alifungua kesi.

 “Baada ya miaka miwili nilipata nakala ya hukumu kutoka Wizara ya Afya na kuamua kufungua kesi ya madai ya kuhitaji Sh milioni 200 kwa ajili ya fidia, mahakama ilitoa hukumu kwa kulitaka Shirika la Elimu Kibaha linilipe fedha hizo, lakini wananizungusha malipo yangu, naomba Rais Magufuli anisaidie nipate fedha zangu,” alisema Mkumbi.

Akizungumzia madai hayo, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Cyprian Mpemba, alisema malalamiko ya mtu huyo ni ya kweli isipokuwa taratibu za malipo zitafanywa na Hazina.

“Hiyo ni kesi ya miaka 15 nyuma, hata mimi sikuwepo hapa, lakini nilipitia hukumu ile pamoja na kikoa cha Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika ambacho kiliamuru barua ya maombi ya fedha yapelekwe Hazina ambao wanapaswa kufanya utaratibu wa kumlipa mlalamikaji,” alisema Mpemba.

Alisema tangu iandikwe barua hiyo ya maombi kwenda Hazina ni takribani wiki mbili, hivyo lazima zifuatwe taratibu za Serikali.

Alimtaka muhusika kuwa na subira kwakuwa suala hilo linashughulikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles