30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ALLY HAPI: TUSHIRIKIANE KUKUZA UTALII WA NDANI

NA SIDI MGUMIA, IRINGA

UTALII una manufaa makubwa kwa uchumi wa Tanzania na ungeweza kuleta manufaa makubwa zaidi katika siku zijazo iwapo utasimamiwa ipasavyo.

Sekta hii imepanuka kwa haraka katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa na idadi inayoongezeka ya wageni kila mwaka.

Licha ya faida ambazo tayari zinatokana na sekta hii, Watanzania walio wengi bado hawajafaidika kadri iwezekanavyo.

Hatahivyo watalii wengi ni watu wa mataifa ya nje lakini pia shughuli zote za kitalii zimejikita katika maeneo machache ambayo inaelezea kwa nini sehemu nyingine za nchi hazijaunganishwa.

Pia, hata katika maeneo ambayo yanatembelewa sana, umasikini bado ni changamoto, hususani vijiji vilivyo karibu na Hifadhi za Taifa, ikiashiria kwamba bado miundombinu mibovu iliyopo haisaidii kuleta maendeleo endelevu.

Pamoja na kuwapo kwa jitihada mbalimbali za kukuza utalii nchini, bado baadhi ya watanzania wana dhana kuwa wageni kutoka nje ya nchi, ndio wanaopaswa kutembelea hifadhi za wanyama na kuangalia kumbukumbu mbalimbali.

Katika mahojiano na gazeti la Mtanzania, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, anaeleza kwamba Watanzania bado wanahitaji kueleimishwa juu ya umuhimu wakufanya utalii na faida inayopatikana endapo watatembelea hifadhi za taifa.

“Bado tuna kazi kubwa ya kuendelea kutoa elimu juu ya maswala ya utalii kwasababu kuna hali ya kutokuwa na msukumo na mwamko mkubwa wa utalii wa ndani na swala la utalii wa ndani linatakiwa kujengwa kuanzia kwenye shule zetu, lazima watoto wetu tuwajengee utamaduni wa kutembelea hifadhi zetu na hii ndio itawafanya waweze kuhamisha utamaduni huo kwa vizazi vyao vingine”, alisema Hapi

Aliongeza kuwa, “Uelewa upo watu wanajua kuna Makumbusho ya Mkwawa, Boma, Kalenga na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na historia nyingine nyingi lakini watanzania bado hatujawa na utamaduni wakufanya utalii katika vivutio vyetu vya ndani.”

Katika kuhakikisha utalii Iringa unaleta tija, Hapi anasisitiza kuwa wao kama mkoa zipo shughuli nyingine wanazozifanya moja ni kuutangaza mkoa.

“Nafikiri kwamba bado nina kazi ya kufanya ya kuvitangaza vivutio vya Iringa na kutangaza watu waijue Iringa ni nini lakini kubadilisha mitazamo ya watu pia ya watendaji wa Serikali ndani ya Iringa, watoa huduma sekta za hoteli, sekta za biashara ili hawa wote watengeneze mfungamano baina ya Serikali, sekta binafsi, Mkoa na wananchi kutengeneza na kuuza utalii,” alisema Hapi

Pia amesema wameanza juhudi za kufanya ukarabati wa uwanja wao wa ndege wa Iringa, ambo wanaamini kabisa utakapoanza kupata safari za ndege kutoka katika Shirika la ndege la Tanzania itatusaidia kuwaongezea wageni wengi, wawekezaji wengi zaidi wanaokuja kuwekeza katika sekta za hoteli lakini pia watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Tumeamua kutumia nguvu zetu sisi kama mkoa pamoja na wadau wa ndani ya mkoa kuboresha jengo la kupokelea wageni, hatukutaka kusubiri bajeti ya Serikali, tuliamua kufanya kwa nguvu zetu wenyewe na sasa tumeshaezeka, na tunashukuru tulifanya mazungumzo na wenzetu wa viwanja vya ndege, Mamlaka ya anga wametuletea mashine mpya kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo ya abiria, ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria wengi zaidi na tunatarajia kuanzia mwezi wa tatu kupokea safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania,” alisisitiza Hapi

Aliongeza kuwa, kama mkoa hawajakaa, wanafanya juhudi zao kwanza, mikakati yao ni kuhakikisha ya kwamba wanaendelea kuutangaza mkoa wao kuwavutia watalii zaidi waende kutembelea maeneo ya utalii ili kuhakisha wanatengeneza pato la mkoa wao lakini pia pato la taifa.

“Kama nchi kwa muda mrefu sana imekuwa haitoi kipaumbele kwa kutangaza fursa za utalii hasa utalii wa kusini. Hivyo mi nitoe tu rai kwa Wizara, Mamlaka zinazosimamia utalii na kwamba sasa ni wakati wa kutangaza vivutio vilivyopo nyanda za juu Kusini ili watalii wetu nao wajue kuwa wana ‘options’ lakini pia kwa kuenda kutembelea mahali pamoja tu wageni watachoka hivyo kuwatangazia vivutio vingine kusini vitatufanya tupate watalii wengi kwani watalii watajua kuwa bado kuna maeneo mengine ya utalii wanahitaji kuyatembelea.”

Mbali na hilo, Hapi alisisitiza kuwa, “Tunataka kuifanya Iringa ifanane na Arusha, Zanzibar na mikoa mingine yenye vivutio vya kitalii lakini huwezi kufanya hivyo kama unategemea mgeni atoke Arusha mpaka hapa kwa basi haiwezekani ndio maana nikasema tunataka tuanzishe safari za ndege na tumefanikiwa kwasababu mashirika na taasisi zote zinazohusika na safari za ndege wamekuja kufanya ukaguzi wameridhika kwamba mwezi wa tatu tutanza kupata ndege aina ya Bombardier na kwamba gharama haitakuwa dola 800 tena, itakuwa laki mbili au tatu hivyo utapunguza gharama, utarahisisha usafiri kwahivyo hii ni mikakati inayoenda kuifanya Iringa ifanane kabisa na mikoa mingine kwa maana ya utalii, kwa kupokea idadi kubwa ya watalii na tunaimani kabisa kwamba hiyo ndiyo dhamira yetu na tuna uwezo wa kuifikia ndani ya kipindi kifupi kinachokuja.”

Kwahivyo ni jambo la kitaifa na jambo ambalo linatakiwa lifanyiwe kampeni na kila mmoja kuhamasisha kufanya utalii wa ndani kabla hatujaenda kutafuta watalii wa nje.

Yusuf Mwinde (42), ambaye ni mmiliki wa mashine ya kusaga unga katika kijiji cha Mapogolo anadai kuwa tabia ya watanzania kutotembelea hifadhi za wanyama ulijijenga tangu awali, Serikali ilipotenga maeneo maalumu ya hifadhi kwani haikuwashirikisha wananchi.

Lakini Mwinde anasema kuwa pamoja na hilo ni wakati sasa wa wananchi kubadilika na wawe na nia ya kutembelea hifadhi mbalimbali za wanyamapori, kwani licha ya kufurahia na kupata mafunzo mbugani, utalii ni chanzo cha mapato katika kuongeza uchumi wa nchi.

Wasichojua wengi ni kuwa utalii wa mbuga nchini ulianzia Mikoa ya kusini mwaka 1947 na haswa mkoa wa Iringa ambao ulikuwa na wazungu wengi na mwingiliano na nchi za Malawi, Zambia na  Zimbabwe wakati huo zikiwa ni makoloni ya Mwingereza.
Naye Hidaya Lucas (33), mkulima katika kijiji cha Makifu kilichopo karibu na Hifadhi ya Ruaha amekiri kuwa wanajua kuna suala la kutembelea hifadhi lakini akidai kuwa gharama zake ni kubwa na kwamba ni mambo ya wageni na sio wazawa kwa maana ya kutokuwa na faida ya moja kwa moja kwao.

Shaban Mulusamba (52) mkazi wa kijiji cha Ipogolo ameshauri kuwa Serikali lazima ifikirie njia bora zaidi ya kuvutia uwekezaji binafsi na kuchukua hatua za kutengeneza mazingira yanayofaa zaidi ya kufanya biashara ya utalii kama vile barabara.

“Kwasasa kidogo watu tumeanza kuelewa maswala ya utalii yanavyokwenda kwakuwa maafisa utalii wa Hifadhi ya Ruaha wanajitahidi kutuelimisha lakini bado tunashauri elimu iendelee kutolewa kwa wazawa na ndio iwe rahisi kwetu kushiriki kikamili kwenye maswala mazima ya uhifadhi wanyamapori,” alisema Mpili Maluo (45)

Kwa upande wake Afisa Utalii na Masoko wa Hifadhi ya Ruaha, Antipas Mgungusi, anasema changamoto, ni kutokuwa na uelewa wa hifadhi za Taifa na taratibu zake, kwahiyo wapo ambao wakisikia tu utalii wanadhani ni kwa ajili ya wageni kutoka nje kwahiyo sisi kama Hifadhi tunaendelea kuwafikia na kuwapa elimu zaidi pia tuna kampeni ya kuwatembelea watu nyumba hadi nyumba, shuleni na kwingineko.

“Lakini pia kama hifadhi na idara ya utalii, tumeona tuweke utaratibu wa usafiri wa pamoja ambao utawawezesha wananchi kufika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwa mfano kila Jumamosi, Ijumaa au Jumapili ya mwisho wa mwezi ziwe ni siku ambazo  mtu anatakiwa tu kuwa makini na ratiba zetu ambapo tutakuwa na tangazo na tutatangaza kiwango ambacho kitatolewa kwa ajili ya kutembelea mbuga kwa gharama nafuu. Utaratibu huu utaanza mara moja utakapomalizika matayarisho yake,” alisema Mgungusi

Wakiwa kama wadau wa Uhifadhi wa wanyamapori na utalii na mazingira  kwa ujumla, Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani kupita mradi wake wa Protect (USAID Protect) nao pia wamejikita katka kutoa elimu kukuza uelewa haswa kwa wandishi wa habari lengo likiwa ni kuhakikisha wanaandika habari za uhifadhi kwa wingi na ufasaha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles