24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Ally Hapi: Tushirikiane kukuza utalii wa ndani

SIDI MGUMIA, IRINGA

UTALII una manufaa makubwa kwa uchumi wa Tanzania na ungeweza kuleta manufaa makubwa zaidi katika siku zijazo iwapo utasimamiwa ipasavyo.

Sekta hii imepanuka kwa haraka katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa na idadi inayoongezeka ya wageni kila mwaka.

Licha ya faida ambazo tayari zinatokana na sekta hii, Watanzania walio wengi bado hawajafaidika kadiri iwezekanavyo kwa kukosa maarifa ya kushiriki kikamilifu na kubakia kuwa watazamaji.

Hata hivyo, watalii wengi ni watu wa mataifa ya nje, lakini pia shughuli zote za kitalii zimejikita katika maeneo machache ambayo inaelezea kwanini sehemu nyingine za nchi hazijaunganishwa. Hali hiyo imesababisha kuwa makini katika kuuendeleza utalii maeneo yote ya nchi kwani utalii una sura nyingi na sekta mbalimbali kila moja kwa hitaji na ridhaa ya mhusika. Matangazo rasmi yanahitajika.

Pia, hata katika maeneo ambayo yanatembelewa sana, umasikini bado ni changamoto, hususan vijiji vilivyo karibu na Hifadhi za Taifa, ikiashiria kwamba bado miundombinu mibovu iliyopo haisaidii kuleta maendeleo endelevu. Wakati mwingine umasikini huo umegeuzwa kuwa ndio utalii wenyewe kwa wale ambao umasikini uusoma vitabuni na si kukutana nao ana kwa ana. Uzuri wake kila mtu anaufahamu  umasikini ingawa hawaishi hivyo.

Wakati sekta ya utalii ikipanuka kwa kasi, bado baadhi ya Watanzania wana dhana kuwa wageni kutoka nje ya nchi, ndio wanaopaswa kutembelea hifadhi za wanyama na kuangalia kumbukumbu mbalimbali ambazo zimekuwa tunu ya nchi hii adhimu.

Katika mahojiano na gazeti la MTANZANIA, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, anaeleza kwamba Watanzania bado wanahitaji kuelimishwa juu ya umuhimu wakufanya utalii na faida inayopatikana endapo watatembelea hifadhi za taifa.

“Bado tuna kazi kubwa ya kuendelea kutoa elimu juu ya masuala ya utalii kwa sababu kuna hali ya kutokuwa na msukumo na mwamko mkubwa wa utalii wa ndani na suala la utalii wa ndani linatakiwa kujengwa kuanzia kwenye shule zetu, lazima watoto wetu tuwajengee utamaduni wa kutembelea hifadhi zetu na hii ndiyo itawafanya waweze kuhamisha utamaduni huo kwa vizazi vyao vingine,” alisema Hapi na kuongeza:

 “Uelewa upo watu wanajua kuna Makumbusho ya Mkwawa, Boma, Kalenga na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na historia nyingine nyingi lakini Watanzania bado hatujawa na utamaduni wakufanya utalii katika vivutio vyetu vya ndani.”

Katika kuhakikisha utalii Iringa unaleta tija, Hapi anasisitiza kuwa wao kama mkoa zipo shughuli nyingine wanazozifanya moja ni kuutangaza mkoa.

“Nafikiri kwamba bado nina kazi ya kufanya ya kuvitangaza vivutio vya Iringa na kutangaza watu waijue Iringa ni nini lakini kubadilisha mitazamo ya watu pia ya watendaji wa Serikali ndani ya Iringa, watoa huduma sekta za hoteli, sekta za biashara ili hawa wote watengeneze mfungamano baina ya Serikali, sekta binafsi, mkoa na wananchi kutengeneza na kuuza utalii,” alisema Hapi.

Pia amesema wameanza juhudi za kufanya ukarabati wa uwanja wao wa ndege wa Iringa, ambao wanaamini kabisa utakapoanza kupata safari za ndege kutoka katika Shirika la ndege la Tanzania, itatusaidia kuwaongezea wageni wengi, wawekezaji wengi zaidi wanaokuja kuwekeza katika sekta za hoteli lakini pia watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Tumeamua kutumia nguvu zetu sisi kama mkoa pamoja na wadau wa ndani ya mkoa kuboresha jengo la kupokelea wageni, hatukutaka kusubiri bajeti ya Serikali, tuliamua kufanya kwa nguvu zetu wenyewe na sasa tumeshaezeka na tunashukuru tulifanya mazungumzo na wenzetu wa viwanja vya ndege, Mamlaka ya anga wametuletea mashine mpya kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo ya abiria, ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria wengi zaidi na tunatarajia kuanzia mwezi wa tatu kupokea safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania,” alisisitiza Hapi.

Aliongeza kuwa kama mkoa hawajakaa, wanafanya juhudi zao kwanza, mikakati yao ni kuhakikisha ya kwamba wanaendelea kuutangaza mkoa wao kuwavutia watalii zaidi waende kutembelea maeneo ya utalii ili kuhakikisha wanatengeneza pato la mkoa wao lakini pia pato la taifa.

“Kama nchi kwa muda mrefu sana imekuwa haitoi kipaumbele kwa kutangaza fursa za utalii hasa utalii wa Kusini. Hivyo nitoe tu rai kwa Wizara, Mamlaka zinazosimamia utalii na kwamba sasa ni wakati wa kutangaza vivutio vilivyopo Nyanda za Juu Kusini ili watalii wetu nao wajue kuwa wana ‘options’ lakini pia kwa kwenda kutembelea mahali pamoja tu wageni watachoka hivyo kuwatangazia vivutio vingine Kusini vitatufanya tupate watalii wengi kwani watalii watajua kuwa bado kuna maeneo mengine ya utalii wanahitaji kuyatembelea.”

Mbali na hilo, Hapi alisisitiza kuwa “Tunataka kuifanya Iringa ifanane na Arusha, Zanzibar na mikoa mingine yenye vivutio vya kitalii lakini huwezi kufanya hivyo kama unategemea mgeni atoke Arusha mpaka hapa kwa basi, haiwezekani ndio maana nikasema tunataka tuanzishe safari za ndege na tumefanikiwa kwa sababu mashirika na taasisi zote zinazohusika na safari za ndege wamekuja kufanya ukaguzi wameridhika kwamba mwezi wa tatu tutaanza kupata ndege aina ya Bombardier na kwamba gharama haitakuwa dola 800 tena, itakuwa laki mbili au tatu hivyo utapunguza gharama, utarahisisha usafiri kwa hivyo hii ni mikakati inayoenda kuifanya Iringa ifanane kabisa na mikoa mingine kwa maana ya utalii, kwa kupokea idadi kubwa ya watalii na tuna imani kabisa kwamba hiyo ndiyo dhamira yetu na tuna uwezo wa kuifikia ndani ya kipindi kifupi kinachokuja.”

Kwa hivyo ni jambo la kitaifa na jambo ambalo linatakiwa lifanyiwe kampeni na kila mmoja kuhamasisha kufanya utalii wa ndani kabla hatujaenda kutafuta watalii wa nje.

Yusuf Mwinde (42), ambaye ni mmiliki wa mashine ya kusaga unga katika Kijiji cha Mapogolo, anadai kuwa tabia ya Watanzania kutotembelea hifadhi za wanyama ulijijenga tangu awali, Serikali ilipotenga maeneo maalumu ya hifadhi kwani haikuwashirikisha wananchi.

Lakini Mwinde anasema k pamoja na hilo ni wakati sasa wa wananchi kubadilika na wawe na nia ya kutembelea hifadhi mbalimbali za wanyamapori, kwani licha ya kufurahia na kupata mafunzo mbugani, utalii ni chanzo cha mapato katika kuongeza uchumi wa nchi.

Wasichojua wengi ni kuwa utalii wa mbuga nchini ulianzia mikoa ya Kusini mwaka 1947 na hasa Mkoa wa Iringa ambao ulikuwa na wazungu wengi na mwingiliano na nchi za Malawi, Zambia na  Zimbabwe wakati huo zikiwa ni makoloni ya Mwingereza.
Naye Hidaya Lucas (33), mkulima katika Kijiji cha Makifu kilichopo karibu na Hifadhi ya Ruaha amekiri kuwa wanajua kuna suala la kutembelea hifadhi lakini akidai kuwa gharama zake ni kubwa na kwamba ni mambo ya wageni na si wazawa kwa maana ya kutokuwa na faida ya moja kwa moja kwao.

Shaban Mulusamba (52), mkazi wa Kijiji cha Ipogolo, ameshauri kuwa Serikali lazima ifikirie njia bora zaidi ya kuvutia uwekezaji binafsi na kuchukua hatua za kutengeneza mazingira yanayofaa zaidi ya kufanya biashara ya utalii kama vile barabara.

“Kwa sasa kidogo watu tumeanza kuelewa masuala ya utalii yanavyokwenda kwa kuwa maofisa utalii wa Hifadhi ya Ruaha wanajitahidi kutuelimisha lakini bado tunashauri elimu iendelee kutolewa kwa wazawa na ndio iwe rahisi kwetu kushiriki kikamilifu kwenye masuala mazima ya uhifadhi wanyamapori,” alisema Mpili Maluo (45).

Kwa upande wake Ofisa Utalii na Masoko wa Hifadhi ya Ruaha, Antipas Mgungusi, anasema changamoto ni kutokuwa na uelewa wa hifadhi za Taifa na taratibu zake, kwa hiyo wapo ambao wakisikia tu utalii wanadhani ni kwa ajili ya wageni kutoka nje na sisi kama hifadhi tunaendelea kuwafikia na kuwapa elimu zaidi pia tuna kampeni ya kuwatembelea watu nyumba hadi nyumba, shuleni na kwingineko.

“Lakini pia kama hifadhi na idara ya utalii, tumeona tuweke utaratibu wa usafiri wa pamoja ambao utawawezesha wananchi kufika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwa mfano kila Jumamosi, Ijumaa au Jumapili ya mwisho wa mwezi ziwe ni siku ambazo  mtu anatakiwa tu kuwa makini na ratiba zetu ambapo tutakuwa na tangazo na tutatangaza kiwango ambacho kitatolewa kwa ajili ya kutembelea mbuga kwa gharama nafuu. Utaratibu huu utaanza mara moja utakapomalizika matayarisho yake,” alisema Mgungusi.

Wakiwa kama wadau wa uhifadhi wa wanyamapori na utalii na mazingira kwa ujumla, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani kupita mradi wake wa Protect (USAID Protect), nao pia wamejikita katika kutoa elimu kukuza uelewa hasa kwa waandishi wa habari lengo likiwa ni kuhakikisha wanaandika habari za uhifadhi kwa wingi na ufasaha.

Kwa kuwatuliza wananchi wa Iringa na wa maeneo ya Kusini mwa nchi Serikali na Tanapa wameamua kwa dhati kulifanyia kazi suala hilo na limepata mkopo mkubwa wa kuboresha kila kitu kwenye mbuga na kuamua kuwa makao makuu ya utalii kwa Kusini yatakuwa Iringa kama ilivyokuwa mwaka 1947.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles