27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Alazwa wodini miaka miwili, kufanyiwa upasuaji mara nane

 

Ebon stephen akimuonyesha mshono mwandishi wa makala haya.
Ebon stephen akimuonyesha mshono mwandishi wa makala haya.

Na Clara Matimo, Mwanza

EBON Stephen (46), mkazi wa Nyakato National jijini Mwanza, alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando tangu Feburuari 27 mwaka 2009 na kuruhusiwa kurejea nyumbani kwake Feburuari 30 mwaka 2011.

“Nilikuwa na maumivu makali ya tumbo ambayo yalinianza Feburuari 25 mwaka 2009, nilikuwa nikiishiwa nguvu, nikapewa dawa ya kutuliza maumivu lakini sikupata nafuu.

“Ilipofika Feburuari 27 mwaka 2009 nilihisi maumivu makali  kupindukia ndipo nilipopelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando nikaanza maisha ya siku zaidi ya 730 hospitalini hapo,” anasema Ebon.

Katika mahojiano na MTANZANIA  anasema, wakati anafikishwa Bugando Feburuari 27 mwaka 2009, tayari tumbo lake lilikuwa limevimba upande wa kushoto.

Alichukuliwa sampuli za vipimo vikapelekwa maabara hata hivyo, kabla ya majibu kutolewa alipelekwa chumba cha upasuaji wa dharura ili kuokoa maisha yake  yaliyokuwa mahututi.

“Nilifanyiwa upasuaji, baada ya siku saba madaktari walikuja kukagua kidonda wakakuta hakijakauka. Nilimuuliza Daktari kilichokuwa kikinisibu akasema walikuta utumbo wangu ukiwa umetoboka, aliniambia walitoa lita mbili na nusu za usaha,” anasema.

Anasema madaktari walikata utumbo uliokuwa na matundu yenye usaha uliokuwa umesambaa hadi nje ya utumbo na kuweka plastiki ili ziwe badala ya utumbo ulioondolewa.

“Madaktari wa Bugando walichukua usaha ule ili kwenda kuuotesha (kitaalamu wanaita Culture) kwa lengo la kutafuta chimbuko la maambukizi. Baada ya kufanya uchunguzi waliniambia hawakuona ugonjwa,” anafafanua.

Baada ya hatua hiyo, Ebon anasema aliandikiwa kipimo cha ‘Ultra Sound’  ambacho baadaye kilionesha alikuwa na jipu kwenye mizizi ya ini.

“Hiyo ilikuwa Machi 25 mwaka 2009 nilipofanyiwa upasuaji kwa mara ya pili hospitalini hapo, madaktari wakasema walikuta utumbo wangu ukiwa umejikunja, wakaukata na kuuondoa wakati lile jipu waliondoa usaha,” Ebon anaendelea kusimulia.

Ebon anasema madaktari wa hospitali hiyo walimwambia utumbo ulijikunja kwa sababu ya kukosa chakula muda mrefu kwa kuwa tangu alipoanza kuugua hakuweza kula chakula.

“Sampuli zilipopelekwa maabara mara nyingine, niliambiwa sikuwa na ugonjwa, wakanipiga ‘X-Ray’ ya kifua na mgongo, walinipiga ‘Ultra Sound’ ya tumbo, halafu wakanipima Virusi vya Ukimwi (HIV) na kusema sikuwa na maambukizi yoyote.

“Tumbo langu liliendelea kunisumbua, wakati katika kidonda cha upasuaji wa pili usaha uliendelea kuvuja kama ilivyokuwa mwanzo. Madaktari wakaniambia labda utumbo ulikuwa umetoboka tena  yawezekana nilipokuwa nikila chakula kilikuwa kikipitiliza hadi kwenye kidonda ndiyo maana  usaha ulikuwa ukiendelea kuvuja,” Ebon anafafanua masahibu ya maisha yaliyomkuta.

Alipelekwa chumba cha upasuaji mara ya tatu Juni 4, mwaka 2009, ambapo madaktari walipofanya upasuaji walikuta jipu juu ya bandama.

Anasema pia kwa kuwa alikuwa mara nyingi akilalia upande wa kushoto, mbavu za kushoto zilipata shimo kutokana na nyama kulika na kusalia mifupa tu.

“Walinisafisha kwa dawa kisha waliniwekea dawa za kuotesha nyama ubavuni. Nilikaa  majuma mawili pasipokuona usaha, kisha ukarejea kwa namna ya kunikatisha tamaa.

“Baada ya mjadala mkali wa madaktari nilishauriwa kula chakula  kingi kwa awamu tofauti, nilikula chakula kama nilivyoshauriwa, nikapata nguvu kidogo mwilini lakini usaha uliendelea kuvuja kama ilivyokuwa awali.

“Wakati huo sikumjua Mungu mpaka Juni 30 mwaka 2009 alipokuja Mhubiri wa madhehebu ya dini akaniuliza kama nilitaka kuombewa. Nilikubali nikafanyiwa sala ya toba pale kitandani kwa kuwa sikuweza kusimama wala kukaa.

“Niliaambiwa nisome biblia, nikawa nasoma Zaburi 51:1-9, Zaburi 23:1-6 na Zaburi 117:16-18 nikarejewa na matumaini kwamba siku moja Mungu angeniponya na maradhi haya ya kutatanisha,” anasema.

Anasema alishangaa kuona ndugu, jamaa na rafiki zake waliokuwa wamemnyanyapaa wakianza kuja hospitalini hapo kumtazama na kumpa msaada.

Anasema kuna wachungaji waliofunga kwa ajili yake wakimwombea apone.

“Nilishangaa watu wengi wakiwamo wauguzi na matabibu waliokuwa wakininyanyapaa kutokana na kutokwa usaha kwa muda mrefu wakianza kunisogelea na kunipa msaada niliohitaji.

“Agosti 18 mwaka 2009, madaktari  walipopita wodini walikuta usaha ukizidi kuvuja huku ukiwa na rangi tofauti, wakawaambia wauguzi kuniandaa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kwa mara ya nne siku iliyofuata yaani Agosti 19. Kwa hiyo nikafanyiwa tena upasuaji wa tumbo kwa mara ya nne,” anasema Ebon.

Anafananisha usaha uliokuwa ukitoka tumboni mwake na mboga za majani zilizopondwa-pondwa kwa kuwa ulikuwa mweusi wenye harufu mbaya.

“Agosti 20 mwaka 2009 madaktari walipokuja wodini waliniambia walikuta pafu la upande wa kushoto likiwa na jipu na wakafafanua kwamba usaha huo mweusi ulikuwa ukitokea kwenye pafu hilo,” Ebon anafafanua, huku akisema daktari alimwambia alidhani hiyo ingekuwa operesheni ya mwisho kwa kuwa walikuwa wamesafisha tumbo lake lote lililokuwa na usaha.

Anasema madaktari wa Bugando walimtoboa wakaweka mpira wa kutoa usaha nje usije ukavujia tumboni na kuleta madhara makubwa.

“Hata hivyo katika hali ya kushangaza sana siku moja ilikuwa saa sita mchana siku chache baada ya operesheni ya nne, madaktari walipofika wodini walinikuta nikiwa navuja usaha mwingi kuliko ilivyokuwa mwanzo. Walikuta mpira walioniwekea umejaa na mwingine mwingi ukiwa unamwagika  sakafuni.

“Dk. Emmanuel akawaambia wenzake waniwahishe chumba cha upasuaji kwa dharura kwa mara ya tano na kwamba yeye angekuja baada ya muda,” anasema Ebon huku akitaja Oktoba 28 mwaka 2009 kwamba ni siku alipofanyiwa upasuaji mkubwa wa tumbo.

 

Anasema siku iliyofuata madaktari walimwambia kwamba walikuta usaha mwingi  na shimo kubwa kwenye ukuta wa tumbo.

 

Anasema usaha uliendelea kuvuja na ilipofika Januari 15 mwaka 2010 alifanyiwa upasuaji mara ya sita.

 

Madaktari walimwambia baada ya upasuaji wa sita kwamba walikuta wadudu waliokuwa pafu la kushoto wakiwa wamehamia la kulia huku wakikuta jipu katika pafu hilo la kulia lililosababisha usaha kujaa tumboni.

 

“Miezi minne baada ya operesheni ya sita, usaha ulianza kuvuja kwa wingi hali iliyofanya madaktari kunirejesha chumba cha upasuaji kwa mara ya saba…ilikuwa Juni 9, mwaka 2010.

 

“Nakumbuka siku hiyo nilitolewa wodini saa mbili asubuhi nikapelekwa chumba cha upasuaji. Saa 10 Alasiri ndipo waliponifanyia operesheni kwa kuwa walikuwa na kazi kubwa siku nzima kuhudumia akina mama wenye fistula.”

 

Anasema baada ya operesheni hiyo ya saba aliambiwa kuwa kuta zote za tumbo lake zilikuwa zimeoza.

Itaendelea wiki ijayo…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles