23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Al-Shabaab wafanya mauaji ya kutisha Kenya

Kundi la Al-shabaab
Kundi la Al-shabaab

MANDELA, Kenya

MAUAJI ya kutisha yameendelea kutikisa nchini Kenya baada ya jana asubuhi kundi la wanamgambo la Al-Shabaab kuua watu 36 katika machimbo ya mawe huko Koromey, Kaunti ya Mandera.

Watu waliouawa wote hawakuwa Waislamu na wengi wao wanatoka eneo la Chaka, Kiganjo katika Kaunti ya Nyeri.

Shambulio hilo baya lililotokea karibu na mpaka wa Somalia limekuja ikiwa ni wiki moja tu baada ya kundi hilo kuua watu wengine 28 kwenye kaunti hiyo.

Watu hao waliuawa baada ya kushushwa kutoka kwenye basi walilokuwa wakisafiria na kutenganishwa na Waislamu kabla ya kuwapiga risasi.

Kabla ya kuuawa walilazwa katika mstari na wengi wao walipigwa risasi kichwani, huku wengine wakichinjwa.

Shambulio hilo lilisababisha mashirika ya kijamii kuandaa maandamano kushinikiza Mkuu wa Polisi, David Kimaiyo na Waziri wa Usalama, Joseph ole Lenku kujiuzulu.

Juzi chama kikuu cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) kilitangaza kuandaa maandamano ya kushinikiza Rais Uhuru Kenyatta na Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Julius Karangi kujiuzulu kwa kushindwa kulinda Wakenya dhidi ya mashambulizi ya watu kutoka nje ya nchi.

Baadhi ya walionusurika katika shambulio la jana waliiambia polisi kuwa Waislamu waliokuwa eneo hilo hawakuguswa.

Al-Shabaab imekiri kuhusika na shambulio hilo.

Tukio hilo limekuja wakati Serikali ya Rais Kenyatta ikizidi kuandamwa kwa kushindwa kulinda maisha ya raia.

Miongoni mwa makosa ya dhahiri ni kupuuza taarifa za kiintelijensia, hasa katika maeneo ya mpaka na Somalia, ambako kuna askari wachache na udhaifu mkubwa wa usalama.

Polisi wanasema waathirika walishambuliwa wakati wakiwa wamelala kwenye mahema yao machimboni saa 7 usiku.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kimaiyo, alisema wanamgambo hao walishambulia machimbo hayo yaliyopo kilomita 10 kutoka mjini Mandera na baadaye kuvuka mpaka kurudi Somalia.

Shambulio hilo lilitokea saa 4 tu baada ya watu waliokuwa na bunduki aina ya AK-47 kuishambulia klabu moja huko Wajir ambako walimuua kwa risasi mtu mmoja na kujeruhi wengine 13.

Watu hao walioficha nyuso zao, walishambulia klabu ya Ngamia, iliyopo karibu mita 800 kutoka kituo cha Polisi cha Wajir.

Baada ya kuishambulia klabu hiyo, walienda kushambulia kituo kidogo cha umeme, lakini walizidiwa nguvu na walinzi waliokuwa wakilinda.

Ikulu imetoa taarifa kuhusu mashambulizi ya Mandera na Wajir jana na ilisema uchunguzi wa matukio hayo mawili umeanza

“Serikali inatuma pole kwa familia za waliopoteza wapendwa wao na iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu,” sehemu ya taarifa hiyo ilisema.

Baadaye Rais Kenyatta alitoa hotuba kwa taifa, akisema Kenya haitachoka katika vita vyake dhidi ya ugaidi.

Aidha Kenyatta amelaani wanamgambo hao kwa kutaka kuigawanya Kenya katika misingi ya kidini.

Hata hivyo, wapinzani wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, sasa wanamtaka Kenyatta mwenyewe ajiuzulu.

Mbali ya kushindwa kulinda raia, upinzani unasema nusu ya nchi kwa sasa inadhibitiwa na wanamgambo na magaidi.

“Wakenya wanauawa kama kuku na hata maofisa wa usalama pia. Kuanzia Westgate na Eastleigh mjini Nairobi hadi Mpeketoni na Lamu hadi Kapedo na Mombasa. Simulizi ni ile ile katika Mto Tana, Garissa, Isiolo, Baringo, Bungoma, Samburu, Turkana na Mandera,” ilisema taarifa ya ODM na Seneta wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles