Imechapishwa: Fri, Aug 11th, 2017

AKUTWA AMEFARIKI KWA KUJINYONGA NA MKANDA

Na BEATRICE MOSSES-MANYARA

MTU mmoja amekutwa akiwa amefariki baada ya kujinyonga maeneo ya Negamsii, Kata ya Bagara, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 8, mwaka huu, saa moja asubuhi.

Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, marehemu alifahamika kwa jina la Ramadhani Amani (32), mkazi wa Kwa Mrombo, mkoani Arusha na kwamba alijinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali yake.

“Mtu huyu alikutwa akiwa amejinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali yake huku mwili wake ukiwa kwenye mti ambao alining’iniza mkanda huo.

“Mwili wa marehemu ulipochunguzwa, haukukutwa na jeraha lolote na inasemekana marehemu enzi za uhai wake alikuwa akifanya kazi ya kupaka rangi mjini Babati na hakuwa mkazi wa mjini hapa.

“Lakini taarifa zaidi zinasema kwamba, Agosti 5 mwaka huu, alimuaga fundi mwenzake aitwae Richard Kilasi (23) na kumwambia anarudi nyumbani kwao Arusha kwa kuwa kazi aliyokuwa anaifanya ya kupaka rangi ilikuwa imemalizika.

“Lakini tangu siku hiyo aliyomuaga mwenzake, hakuonekana hadi alipokutwa akiwa amefariki dunia,” alieleza Kamanda Massawe huku akisema chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana ingawa polisi wanaendelea na uchunguzi.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

AKUTWA AMEFARIKI KWA KUJINYONGA NA MKANDA