25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

AJIRA SAWA ILA JIONGEZE KIDOGO – 2

Na ATHUMANI MOHAMED

KARIBUNI tena kwenye safu yetu nzuri mpendwa msomaji wangu. Leo nahitimisha mada hii iliyoanza wiki iliyopita, ambapo tunaangalia kwa undani kuhusu namna ambavyo mtu anaweza kuishi bila kutegemea mshahara kwa asilimia mia moja. Sasa tumalizie mada yetu katika vipengele vilivyosalia hapa chini;

MSHAHARA HUWA HAUTOSHI

Huu ndiyo ukweli ndugu yangu. Hata kama unalalamika labda mshahara wako ni mdogo, ukweli ni kwamba ukiongezwa asimilia 50 ya unacholipwa leo, bado utaendelea kulalamika kuwa mshahara hautoshi. Ilivyo ni kwamba, watu wengi hubadilisha staili zao za maisha baada ya vipato vyao kupanda, jambo ambalo halitakiwi kabisa kwa mtu ambaye ana malengo makubwa kwenye maisha yake. Katika kufanikiwa, hata kama ukiongezwa mshahara wako, ishi kama vile hakuna kilichoongezeka. Endelea na staili yako ileile ya awali, utaona mafanikio katika maisha yako.

MATUMIZI YAKO YAKOJE?

Lakini pia ni vizuri sana kuangalia namna unavyotumia fedha zako. Acha kufanya matumizi ya rafu kama vile wewe ndiye unayetengeneza fedha. Itakuwa jambo la hekima ikiwa utakuwa unayafahamu matumizi yako vizuri ya siku, wiki, mwezi na kadhalika. Mfano, ukiwa unatoka asubuhi nyumbani kwenda kazini, uwe na fedha inayotosha kwa mahitaji yako na akiba kidogo. Utumie kwa namna ulivyopanga. Hiyo itakusaidia usione makali ya tatizo la mshahara pindi utakapochelewa au kama unahisi labda unacholipwa hakitoshi.

WEKA AKIBA

Jitahidi kuwa na akiba binafsi inayotokana na mshahara wako. Kwa mfano, kama mshahara wako ni laki tatu, jitahidi angalau uhifadhi hata laki moja kila mwezi, ambazo utakuwa umeziweka kama akiba yako ikitokea dharura yoyote. Wengi hawana utamaduni wa kuweka akiba na kubaki wakitegemea tarehe fulani lazima watapata fedha. Rejea vipengele vilivyopita; Usitegemee fedha ambayo haijafika mikononi mwako.

NUNUA VYAKULA 

Dawa nyingine ya kupunguza matatizo ya kuishiwa fedha mapema wakati wa kusubiri mshahara ni kununua vyakula. Jenga mazoea ya kununua vyakula vya mwezi mzima (vile visivyoharibika). Hiyo itakusaidia sana wakati ukiwa kwenye hali ngumu kabisa, unaweza kupika familia ikala wakati ukitafakari cha kufanya au ukisubiri mshahara wako. Makali ya mshahara huja wakati una uhitaji mkubwa tegemeo hata la siku moja tu linaweza kukuathiri ukiwa huna kitu kabisa.

FUNGUA MIRADI

Hili nilishasema huko nyuma. Miradi ni jambo zuri, siyo lazima ufungue biashara ya mtaji mkubwa sana. Tafuta chochote ambacho kinaweza kujiendesha ambacho kitakuwa mkombozi wako wakati ukiwa na uhitaji. Narudia tena, mshahara haujawahi kutosha ndugu yangu. Mwingine anaweza kusema: Biashara sawa, nitafunguaje bila mtaji? Acha kuwaza kuhusu mtaji kwanza, tengeneza wazo. Uwe na kitu cha kufanya kisha fedha itakuja baadaye. Ajira yako inaweza kukusaidia kupata mkopo, lakini ni vyema uchukue mdogo kwanza na ufungue mradi ambao unaweza kuusimamia bila kuathiri ajira yako. Muhimu kufanya utafiti wa biashara husika kabla hujafungua. Mikopo ni mkombozi wa wafanyakazi. Wengi wamejikuta wakifanya mambo mazuri baada ya kutumia mikopo yao vizuri.  Jiulize, wewe umefanyia nini mkopo wako? Kumbuka kuingiza mkopo kwenye sehemu ambayo haizalishi, maana yake ni kwamba unakuwa kwenye msongo wa mawazo mara mbili.

Katika mada zinazofuata nitafafanua vizuri kuhusu suala la mikopo kama mada inayojitegemea. Muhimu kwako kufahamu, kama mfanyakazi, mkopo ni mkombozi kwako na unaweza kukutoa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kimafanikio.

KUHUSU AJIRA

Wengine wanaweza kuwaza kwamba bora sasa waache kazi watafute biashara kwa sababu mshahara hautoshi, siyo sawa. Ajira ni muhimu. Biashara ni fani za watu. Kama wewe ni mfanyakazi, ajira inaweza kuwa mstari mzuri kwako kukupeleka kwenye mafanikio. Kama unatamani biashara au unaamini biashara inaweza kukutoa kimaisha, unaweza kufanya majaribio ukiwa ndani ya ajira yako kabla ya kufanya uamuzi baada ya kuona unaweza kusimama  mwenyewe.

Penda kazi yako, jitume, fanya kwa bidii, Mungu atakupa sawa na jasho lako. Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles