27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

AJALI ZAUA 9, ZAJERUHI 67 MORO

Na Ramadhan Libenanga – Morogoro

WATU tisa wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti ya ajali yaliyotokea mkoani Morogoro jana.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei, alisema ajali ya kwanza ilihusisha basi la Kampuni ya Mfundo Trans linalofanya safari zake kati ya Ulanga, Ilonga na Morogoro.

Alisema ajali hiyo, iliyotokea maeneo ya mlima Ndororo wilayani Ulanga, ilisababisha vifo vya watu saba na majeruhi 38.

Alisema kati ya majeruhi hao, wanaume ni 17 na wanawake 21 ambao wote wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Ulanga kwa matibabu.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, Dk. Rajab Risasi, alisema amepokea miili ya watu saba waliofariki dunia katika ajali hiyo.

Alisema majeruhi wanne wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya St Francia Ifakara kwa matibabu zaidi.

Imedaiwa chanzo cha ajali hiyo ni gari kufeli breki na kutumbukia kwenye korongo katika mlima huo.

 

AJALI YA TRENI

Katika tukio la pili, Kamanda Matei alisema wanafunzi wawili wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa, baada ya basi aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T 438 ABR walilokuwa wakitumia kugonga treni.

Alisema basi hilo, lililokuwa limebeba wanafunzi wa shule mbili za sekondari – Tushikamane na Mjimpya za Manispaa ya Morogoro, liligonga treni jana saa moja asubuhi, eneo la Tanesco ambako kuna makutano ya reli na barabara.

Chanzo cha ajali hiyo kimetajwa kuwa ni uzembe wa dereva basi hilo ambaye alilazimisha kupita wakati  treni  ya abiria ikiwa karibu, licha ya kusimamishwa kwa kuonyeshwa kitambaa chekundu.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jacob, alikiri kupokea majeruhi wa ajali hiyo.

Alisema katika majeruhi waliopokewa, wawili walifariki dunia hospitali  hapo, wakati wakitibiwa.

“Wanafunzi wawili wamefariki dunia, majeruhi 29  wamelazwa wakiendelea kupatiwa matibabu, kuna mtoto mmoja yupo chumba cha wagonjwa mahututi,” alisema Dk. Jacob.

Alisema madaktari wanaendelea kukusanya orodha ya  majeruhi na itakapokamilika watatoa taarifa.

Alimshukuru Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz  Abood kwa kujitolea msaada wa dawa kwa majeruhi.

“Tunamshukuru mbunge kwa kusaidia upungufu wa dawa kwa ajili ya majeruhi, wengine wenye nia ya kusaidia waje watusaidie kuongeza dawa,” alisema Dk. Jacob.

Mmoja wa mashuhuda, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Tushikamane, Stella Michael, alisema walimpigia kelele dereva kuhusu ujio wa treni, lakini aliwajibu wasimfundishe kazi.

“Tulimpigia kelele sana dereva kuhusu kitambaa  chekundu chenye kumzuia, lakini aliyapita magari mengine na kuvuka reli na kusababisha kugongwa na treni,” alisema Stella.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles