24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

AJALI KWA WAANDISHI NI MIPANGO YA MUNGU AU ….

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA



Septemba 3 na 9, mwaka huu ni siku ambayo waandishi wa Mkoa wa  Mwanza na Simiyu hawawezi kuisahau hasa wale waliokuwa katika msafara wa Rais Dk. John Magufuli  kutokana na kupata misukosuko iliyokuwa na taswira ya kupoteza uhai wao.

Waandishi wa Mwanza walipata ajali Septemba 3, mwaka huu katika eneo la Suguti Wilaya ya Bunda mkoani Mara, wakati msafara wa Rais Magufuli ukielekea Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo na kuwahutubia wananchi wa wilaya hiyo.

Tunashukuru Mungu hakuna  vifo vilivyotokea isipokuwa majereha  ambayo kwa jitihada za wataalamu wa sekta ya afya, waliweza kutoa huduma nzuri na tayari wanataaluma hao wamerejea katika majukumu yao.

Wakati tunaendelea kutoa pole kwa wenzetu hao, Septemba 9, mwaka huu zinapatikana taarifa tena ya msafara huo kupata misukosuko mkoani Simiyu, ambapo kwa mara nyingine  tena ni waandishi ambao mkono wa sheteni uliendelea kuwatafuta lakini Mungu akaingilia kati na kuzuia kile kilichokuwa  kimepangwa.

Katika ajali hiyo, baadhi ya waandishi wa vyombo mbalimbali walipata majereha na hadi ninapoandika makala haya, wapo waliotibiwa na kuruhusiwa na wachache wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Kanda ya Bugando iliyopo jijini  Mwanza.

Ajali hizo mbili zikitanguliwa na  ile ya  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala ya Agosti 4, mwaka huu ambapo ilisababisha  kifo cha Ofisa Habari wake, Hamza Temba  na ile ya Naibu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Viwanda,  Ludovick Nduhiye ambayo nayo ilisababisha Ofisa Habari Mwandamizi, Shadrack Sagati kupoteza maisha, kumekuwapo na hisia na mitazamo kadhaa katika tasnia ya habari.

Hivi sasa mazungumzo ya  wanataaluma  na hata kwenye mitandao ya kijamii,  wameonekana kuwa na shaka juu ya usalama wao katika safari zao na viongozi wa Serikali, ambapo wengine wakionekana kutokuwa na utayari kusafiri na wenye mamlaka makubwa.

Unaweza kujiuliza kwanini magari ya waandishi ndiyo yanayopata ajali, majibu yanaweza kutofautiana lakini mwisho wa siku utaelezwa kuwa ni mipango ya Mungu ama  ni majaribu ya shetani. Binafsi na kwa uzoefu wangu, naweza kusema kwamba inapotokea uwepo wa ziara yoyote ile, utashuhudia suala la gari za waandishi kutafutwa mwishoni kabisa na kuonekana si muhimu sana.

Pili, kwa namna waandishi wanavyokaa kwenye gari  moja, utadhani ni viazi vya Mbeya  kutokana na idadi kubwa inayozidi uwezo wa  viti vilivyomo ndani ya gari na  huwezi kufunga mkanda.

Tatu, inawezekana kabisa  pengine  madereva wanaoendesha waandishi unakuta hawajazoea misafara yenye mwendo wa kasi, pia mara nyingi hupewa gari ambazo si zao wanazoziendesha kila siku. Nne tumekuwa tukishuhudia   baadhi ya ziara gari kukodishwa na kuwabeba waandishi ama watumishi wengine, sasa dereva wa mitaani anapoingia kwenye misafara ya namna hiyo lazima kutakuwapo na changamoto.

Tano, wamiliki wa vyombo vya habari nao wanachangia waandishi wao kupata misukosuko hiyo kwa kutowawezesha ili kujitegemea katika kutimiza majukumu yao, kitendo ambacho kinafanya wanataaluma hao kusubiri  hisani ya wadau na Serikali  kuwapa vyombo vya usafiri ambavyo kwa namna moja au nyingine havijafanyiwa ukaguzi ipasavyo.

Tunashukuru wapo viongozi wa Mkoa wa Simiyu walionekana hadharani wakiwajulia waandishi wa habari wakati wanatibiwa na kutoa mkono wa pole, ambapo hata wagonjwa walifarijika sana, hii inadhihirisha wazi Rais Magufuli hakukosea kuwasifu kwa namna wanavyofanya kazi katika mkoa huo na kuuletea maendeleo.

Kwa upande wa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza, licha ya kupata ajali nje ya mkoa wao na kutibiwa huko ambapo Septemba 7, mwaka huu Mkuu wa Mkoa huo aliwaita waandishi  waliokuwa katika ziara  ofisini kwake na kuwapa maneno ya faraja kwa ujumla wao.

Kwa wale waliopata misukosuko na kupata majereha kadhaa, inadaiwa nao walipewa  bahasha ambayo inaelezwa ilikuwa na mkono wa pole, lakini haijulikani na kiasi gani kwani wale wa Simiyu pesa ilitolewa hadharani na ikajulikana. Kilichofanywa Simiyu huwa tunakishuhudia kwa Rais Magufuli ambaye huwa anatoa fedha hadharani  na utawala wake ni wa wazi na ukweli, lakini wengine hawajatambua hilo na kufanya siri.

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles