24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali ilivyoandoa uhai wafanyakazi Azam

*JPM, TEF wawalilia, majeruhi wahamishiwa Muhimbili

WAANDISHI WETU-DAR/IRAMBA

RAIS Dk. John Magufuli, amemtumia salamu za pole Mwenyekiti wa Kampuni za Said, Salim Bakhresa kutokana na vifo vya wafanyakazi watano wa vyombo vya habari vya Azam Media Limited waliofariki dunia kwa  ajali ya gari.

Ajali hiyo, ilitokea jana eneo la Shelui mkoani Singida na kusababisha vifo vya wafanyakazi watano wa Azam Media.

Wafanyakazi hao, ni kati ya watu saba waliofariki dunia katika ajali hiyo, baada ya basi aina ya Toyota Coaster, walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori, lililokua likielekea Dar es Salaam, wakati wakielekea wilayani Chato mkoani Geita katika uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Chato-Burigi.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, ilisema Rais Dk. Magufuli alisema ameshtushwa na ajali hiyo, huku akiwaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi.

“Nimeshtushwa na vifo hivi, nampa pole Mwenyekiti  Said Salim Bakhresa na ndugu wa marehemu wote, Mtendaji Mkuu, Tido Mhando na wafanyakazi wote wa Azam na wanahabari wote,”alisema Rais Magufuli katika taarifa hiyo.

Pia aliwaombea majeruhi watatu wa ajali hiyo kupona haraka ili kuendelea na majukumu yao ya kila siku, huku akitoa wito kwa watumiaji wa barabara hasa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

TIDO ATOA NENO

Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV, Tido Mhando alisema ajali hiyo ni pigo kwa wafanyakazi wa Azam Media.

“Kutokana na vifo vya wenzetu hivyo kutatokea mabadiliko makubwa katika matangazo yetu, hivi sasa tunaandaa mipango ya mazishi na tutakuwa tunakatisha mara kwa mara matangazo yetu,”alisema Tido.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Igunga, wawili hali zao si nzuri,lakini mmoja afadhali hali yake ni nzuri.

“Mpaka sasa tumepata msaada mkubwa kutoka kwa wenzetu wa Tanapa ambao wametuma helikopta kwa ajili ya kubeba maiti kutoka Iramba na mipango ya haraka imefanyika kwa ajili ya kuwachukua majeruhi walioko kule Igunga ili waletwe Hospitali ya Taifa Muhimbili,”alisema.

MAJINA YA MAREHEMU

Mkurugenzi wa Uzalishaji Vipindi wa kampuni hiyo,Azam, Yahya Mohamed aliwataja waliofariki dunia, kuwa ni Salim Mhando, Florence Ndibalema, Said Haji, Sylvanus Kasongo na Charles Wandwi.

DAKTARI

Akizungumza na MTANZANIA muda mfupi baada ya ajali hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dk. Hussein Sepoko alisema baada ya kupata taarifa hiyo ya ajali kutoka jeshi la polisi wilayani Iramba, ndipo yeye timu yake wakaelekea katika eneo hilo.

“Baada ya kupata taarifa kutoka Jeshi la Polisi niliondoka mimi na baadhi ya madaktari na wauguzi tukaenda eneo la ajali hiyo, ambayo ilitokea eneo la Kizonzo Tarafa ya Shelui Wilaya ya Iramba.

“Tukakuta miili ya watu saba waliofariki na wengine ni majeruhi watatu walipelekwa Igunga mkoani Tabora kwa matibabu zaidi kwa kuwa eneo lililotokea ajali Hospitali ya Igunga ni karibu kuliko Hospitali ya Kiomboi,”alisema.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kiomboi, Dk. Abel Mafuru aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi muda huo amepata majina manne tu waliofariki.

Aliwataja kuwa, ni Juma Hatibu ambaye alikuwa dereva wa Costa iliyokuwa imewachukua wafanyakazi wa Azam, Salimu Juma Mhando, Saidi Haji Hassan na Hussein Habibu Kiguto wote ni wakazi wa Dar es Salam na watatu hawajajulikana kwa kuwa hawakuwa na vitambulisho .

Hata hivyo, uongozi wa Hospitali ya Wilaya na jeshi la polisi, wamesafirisha miili ya marehemu hao katika Hospitali ya Rufaa mjini Singida kwa kuwa chumba cha maiti cha hospitali hiyo hakina uwezo wa kuhifadhi miili zaidi ya moja.

Katika majeruhi watatu waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, ni mmoja tu halijulikana kwa jina la Mohammed Mwinyishee, wawili hawajajulikana majina yao na jitihada za waandishi wa habari kumtafuta Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, hazikufanikiwa kupata majina mengine ya majeruhi.

UMMY MWALIMU

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliandika katika ukurasa wake Twitter: “Ohh poleni  @azamtvtz kwa msiba huu mkubwa, natoa pole kwa familia za marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, Mwenyezi Mungu awape subra katika kipindi hiki kigumu.

“Wapumzike kwa Amani, Inna lillah waina ilayhi rajjiun, Bwana ametwaa Bwana ametoa,”aliandika Ummy Mwalimu.

JUKWA A LA WAHARIRI

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),  nalo lilieleza kupokea kwa mshtuko taarifa hiyo ajali iliyosababisha vifo vya wafanyakazi hao wa Azam Media.

Taarifa iliyotolewa kwa vyomvo vya habari na TEF na kusainiwa na Katibu wa jukwaa hilo, Nevile Meena, ilisema TEF inaungana na wanataaluma wote wa tasnia ya habari nchini kuupa pole uongozi na menejimenti na wafanyakazi wa Azam Media.

“TEF tumehuzunishwa, kusikitishwa na kuumizwa na msiba huu kwani tasnia imewapoteza wafanyakazi wanataaluma mahiri ambao walikuwa wakielekea Chato mkoani Geita, kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma wa kuwafahamisha Watanzania na dunia kwa ujumla tukio la uzinduzi wa Hifadhi ya Taifaya Burigi-Chato.

“Tunatoa pole kwa viongozi wa Azam na tunaungana nao pamoja na familia za wafiwa katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo,”ilisema taarifa hiyo.

IGP SIRRO NA UCHUNGUZI

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro ameagiza kufanyika uchunguzi kubaini chanzo cha ajali ya magari mawili iliyotekea eneo la Shelui mkoani Singida na kusababisha vifo vya watu saba wakiwemo wafanyakazi watano wa kampuni ya Azam Media.

Akizungumza jijini Mwanza jana katika ziara yake ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za polisi eneo la Myamhongolo, IGP Sirro ameuagiza uongozi wa jeshi hilo mkoani Singida kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyojeruhi wafanyakazi wengine wa kampuni hiyo.

CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), pia kimetoa salamu za rambirambi na pole kwa vyombo vya habari vya kampuni hiyo ya Azam.

“Chadema inatoa pole kwa tasnia ya habari nchini, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote waliguswa na vifo hivyo. Wakati tunawaombea marehemu wapate pumziko la Amani, tunawaombea pia majeruhi uponyaji wa haraka warejee katika siha njema,”alisema msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles