30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

AISHITAKI NOKIA KISA SIMU IMEMSABABISHIA UVIMBE KWENYE UBONGO

Na HASSAN DAUDI NA MITANDAO



KAMPUNI ya Simu za Nokia huenda ikajikuta ikilazimika kutoa kitita cha Pauni milioni 1 (zaidi ya Sh bil tatu za Tanzania) kutokana na ugonjwa wa uvimbe katika ubongo alionao mteja wake wa miaka mingi, Neil Whitfield (60).

Ripoti ya madaktari imeonesha kuwa Whitfield, raia wa Uingereza ana uvimbe wenye ukubwa wa mpira wa gofu katika eneo la makutano ya ubongo na sikio na tayari tatizo hilo limempotezea uwezo wa wake wa kusikia.
Mzee huyo mkazi wa mjini Wigan, anakuwa Muingereza wa kwanza kuipeleka mahakamani kampuni ya simu kutokana na madhara ya kiafya.

Whitfield, baba wa watoto sita, alianza kupotezea uwezo wa kusikia baada ya kufanyiwa upasuaji mwaka 2001.
Akisimulia ilivyokuwa katika mahojiano yake na gazeti la Mirror, anasema tatizo hilo la uvimbe limetokana na kutumia simu aina ya Nokia kwa muda mrefu.

“Sina shaka kabisa kuwa tatizo langu lilitokana na simu ya mkononi.
“Nilitumia miaka mitano hivi nikiwa ‘busy’ kwa muda mrefu na simu yangu. Kuna kipindi niliweza hata kuhisi kuna joto kali linatoka katika simu,” anasema.

Wakati huo huo, anakiri kuwa anajua wazi haitakuwa rahisi kwake kupata haki kwa kuwa anashindana na kampuni kubwa, akiifananisha vita hiyo na ile ya Daud na Goliath iliyosimuliwa katika vitabu vya dini za Kiislam na Kikiristo.
“Huenda ikachukua muda mrefu kumalizika lakini sitakata tamaa. Hii ni kwa ajili ya hatima ya watoto wangu na wengine,” anaongeza.

Madai ya mzee huyo yanakuja huku tayari kukiwa na tetesi nyingi juu ya madhara yanayotokana na matumizi ya simu za mkononi, japo mara nyingi zimekuwa zikionekana kuwa ni porojo.

Anaendelea kusimulia kuwa kutokana na uvimbe wake, alilazimika kuacha kazi yake ya mauzo na kwenda kuwa mwalimu wa chuo, jambo ambalo lilisababisha mshahara wake upungue kwa Pauni 20,000.
Nokia ilikuwa miongoni mwa kampuni kubwa za mawasiliano nchini Uingereza katika miaka ya 1990 na iliweza kuuza mamilioni ya simu.

Hata hivyo, kati ya mwaka 1995 hadi 2015, tafiti juu ya bidhaa hizo ulionesha kuwa watumiaji wake 2,531 walikuwa wanakabiliwa na gharama za upasuaji wa uvimbe katika ubongo.
Aidha, akilizungumzia hilo, huyu ni mtaalamu wa teknolojia, Colin Purnell, ambaye naye licha ya kuwa mtumiaji wa simu za mkononi, pia anaguswa na tatizo hilo.
“Watumiaji wa zamani wako hatarini zaidi kwa kuwa hakukuwa na wingi wa vifaa vya kuzuia mionzi,” anasema Purnell.

Katika taarifa yao, ambayo hata hivyo wataalamu wa afya wanaiona kama utetezi, Nokia wanadai kuwa kwa miaka mingi kipaumbele chao kimekuwa usalama wa watumiaji wa bidhaa zao.

“Bidhaa zote zinafuata matakwa ya kimataifa na kila kinachoendana na matakwa ya mamlaka za afya. Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) linasema ‘tafiti nyingi zimekuwa zikifanywa kwa miaka 20 iliyopita kuangazia madhara ya simu za mkononi kiafya.

“Hadi leo hii, hakuna iliyojibu moja kwa moja athari mbaya za matumizi ya simu za mkononi,” inasomeka taarifa hiyo ya Nokia, kampuni ambayo ilianzishwa mwaka 1865.

Lakini sasa, utetezi wao huo unapingana na kile kinachoaminiwa na taasisi ya Utafiti wa Saratani nchini Uingereza, ambayo inasema matumuzi ya simu za mkononi yamekuwa na uhusiano wa moja kwa moja na ugonjwa huo.
Tafiti za taasisi hiyo zimebaini kuwa watumaji wa simu wamekuwa hatarini kupata uvimbe wa ubongo au aina mbalimbali za kansa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles