29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Ahueni ya corona, wagonjwa 4,000 wapona

Wuhan, CHINA

TUME ya Afya ya China, imesema maambukizi mapya ya virusi vya corona yamepungua kwa siku saba mfululizo, na kwamba wagonjwa wengi zaidi wamepona.

Kwa mujibu wa gazeti la China Daily, Jumatatu maambukizi mapya 381 yalithibitishwa ikilinganishwa na maambukizi mapya 444 ya Jumapili, na 890 ya Februari 3.

Hadi Jumatatu usiku watu waliokuwa wamethibitika kuwa na virusi hivyo walikuwa 37,626 huku vifo vikiwa 1,016 na wengine 4,000 wameshatibiwa na kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Taarifa iliyotolewa na Mshauri Mkuu wa Masuala ya Afya wa China, Zhong Nanshan, ilisema ripoti zinaonyesha kupungua kwa maambukizi mapya ya corona katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo, na dalili zinaashiria baada ya mwezi huu kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo itapungua.

Masoko ya fedha na mitaji duniani yamepokea vyema taarifa hiyo, licha ya tahadhari kutoka kwa wataalamu wa kimataifa waliotishwa na namna homa hiyo ilivyoenea kwa kasi na kuua watu zaidi ya 1,000.

Nanshan ambaye utabiri wake wa siku zilizopita haukuwa sahihi, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa anaamini ifikapo Aprili, mlipuko wa homa hii hatari utakuwa umemalizika, ingawa kuanza tena kwa shughuli za usafiri kunawapa wasiwasi baadhi ya watu.

”Kwa wakati huu, watu wengi wanaanza safari kurejea sehemu zao za kazi na hili linasababisha wasiwasi juu ya uwezekano wa kuzidisha tishio la maambukizi mapya. Lakini kwa kuzingatia hali ya sasa, siamini kwamba hofu yao ina msingi,” alisema Nanshan.

Tangazo hilo la matumaini la viongozi halijazuia shaka miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini China kuhusu uaminifu wa takwimu zinazotolewa, baada ya hatua ya Serikali kubadili maelekezo katika mfumo wa kukusanya data za maambukizi ya homa ya virusi vya corona.

Wakati huo huo, idadi ya wasafiri walioambukizwa virusi vya corona katika meli ya Diamond Princess imepanda na kufika 175, kufuatia kugunduliwa kwa visa vipya 39.

Meli hiyo iliwekwa chini ya karantini nje ya bandari ya Yokohama, Japan Februari 3.

Ofisa mmoja wa kufuatilia karantini hiyo ni miongoni mwa wagonjwa wapya.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, jana akiwa Geneva alisema virusi hivyo vimepewa jina la Covid-19, na kwamba ni muhimu kuepuka unyanyapaa.

“Chanjo ya kwanza kwa ajili ya virusi hivi inaweza kupatikana baada ya miezi 18, kwa hiyo kwa sasa lazima tutumie kila silaha iliyopo,” alisema Ghebreyesus.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles