27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Adha ya corona

Waandishi Wetu

HATUA ya askari kukamata daladala zilizosimamisha abiria Dar es Salaam kudhibiti kuenea virusi vya corona ambavyo vimeshasababisha kifo cha mtu mmoja nchini, imeleta kizaazaa huku baadhi wakikaidi na kupanda zilizojaa na kuketi eneo la katikati kusiko na viti.

Hali hiyo ilishuhudiwa jana maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambapo kwa daladala zilizoamua kutotii sheria bila shuruti, abiria waliokuwa wamesimama walishushwa.

MTANZANIA lilitembelea vituo vya mabasi vya Mbezi Louis, Gongo la Mboto, Buza, Boma na Mwembeyanga na kushuhudia daladala zikipakia abiria kulingana na idadi ya siti.

Katika baadhi ya maeneo abiria waliokuwa wamesimama walishushwa huku daladala zikitakiwa kulipa faini kabla ya kuendelea na safari.

“Aingie mmoja tu jamani leo ni mwendo wa ‘level seat’,” alisikika kondakta wa daladala linalofanya safari zake Buza – Makumbusho.

Kondakta huyo, Nassor Jumanne alisema madereva wengi walikuwa hawana taarifa kuhusu kuanza kwa utaratibu huo na umewagharimu kwa kutakiwa kulipa faini. 

“Bora hata wangekuwa wanakamata na kukuandikia ‘notification’ wanakuacha unaendelea na safari, lakini unakamatwa, abiria wanashushwa, unapigwa na faini.

“Sisi wengine tulikuwa hatujui utaratibu huu, tumeshangaa tunafika Abiola (katikati ya Yombo na Buza) tunasimamishwa na kuandikiwa faini,” alisema Jumanne.

Dereva wa daladala linalofanya safari Machinga Complex – Mwenge, Shukuru Hassan, alisema utaratibu huo utaathiri biashara yao na kuomba viwango vya nauli viongezwe.

“Dada yangu (mwandishi) hali ya biashara ni mbaya, anayepeleka hesabu ya Sh 100,000 usishangae akapeleka Sh 40,000. Mfano unapakia abiria wote wanashuka Makumbusho, hakuna anayeshukia njiani, inakuwaje?

“Ukipakia ‘level seat’ unapata Sh 8,000 kwa sababu unachukua abiria 20 tu, siti zilizong’olewa hapo katikati ni tano wakati ukisimamisha abiria, hapo katikati wanasimama watu 10 hadi 20,” alisema Hassan.

Hata hivyo, kondakta wa daladala linalofanya safari Gongo la Mboto – Mbezi, Samuel Joseph, aliunga mkono utaratibu huo ili kuzuia kuenea virusi vya corona.

“Mimi siwezi kulaumu, roho yangu nyeupe kabisa, kwa sababu ugonjwa unazidi kusambaa. Lakini hesabu inabidi ishuke iwe Sh 40,000,” alisema Joseph.

Katika baadhi ya maeneo ya vituo, pia kulikuwa na ndoo za maji na sabuni kuwezesha watu kunawa mikono kabla ya kuingia kwenye magari.

Dereva Martin Kambi anayeendesha gari linalofanya safari zake kati ya Kigogo Sokoni na Makumbusho, alisema hali ya usafiri ni mbaya na kama itakuwa hivyo kwa siku tatu watapaki magari yao.

“Tutagombana bure na matajiri kwakuwa wao bado hawajashusha hesabu, unafanya kazi kutwa nzima unaishia kupata hela ya tajiri, bora nikabidhi gari nikalime mboga mboga,” alisema Kambi.

Akizungumza na MTANZANIA, dereva John Mathayo anayefanya safari kati ya Mbezi na Temeke, alisema suala la ‘level seat’ limewaathiri kiuchumi kwa sababu mzunguko mmoja wanatumia mafuta ya Sh 30,000 na mmiliki anahitaji hesabu ya Sh 100,000 kwa siku.

Dereva Ramadhan Nyanya ambaye anafanya safari zake Segerea-Mbezi, alisema hesabu kwa siku Sh 80,000 na mafuta wanatumia gharama ya Sh 80,000.

MTANZANIA ilitembelea maeneo mbalimbali na kujionea askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakiwa wanafuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo.

Pia ilishuhudia baadhi ya abiria waliozidi katika daladala wakishushwa kisha kuruhusu gari liendelee na safari.

ABIRIA

Katika maeneo mengi abiria waliozungumza na MTANZANIA walilalamikia uchache wa daladala na kusababisha msongamano vituoni kutokana na watu kusubiri usafiri muda mrefu.

“Mimi nimefika hapa (Buza Kanisani) saa 12:30 asubuhi na hadi saa hizi (saa 1:53 asubuhi) sijapata usafiri. Magari yanapita tayari yakiwa ‘level seat’, watu wanaanza kupanda kwa Lulenge (eneo jirani na Buza Kanisani) wanageuka nayo,” alisema Salma Sudi.

Mkazi wa Chanika Zingiziwa, Salama Idrisa alisema kuwa aliamka alfajiri kwa lengo la kuwahi kwenye shughuli zake za kuuza duka Kariakoo, lakini cha ajabu hadi saa tatu alishindwa kupata usafiri.

“Tunaomba Serikali itusaidie kupanga utaratibu ambao utaturahisishia usafiri kwakuwa leo (jana) tumepata shida ya usafiri, magari mengi yamesitisha safari huku mengine yakikatisha ruti,” alisema Salama.

KAMANDA TRAFIKI

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim, alisema kwa kawaida gari za mjini zinaruhusiwa kusimamisha abiria, lakini utaratibu wa kupakia kulingana na idadi ya siti ni wa dharura ili kukabili ugonjwa wa corona.

“Hii ni dharura, hizi gari za mjini zinaruhusiwa kusimamisha, lakini kwa sababu ni ‘emergency’ (dharura), kama Jeshi la Polisi na kwa kuzingatia sheria tunakwenda nasi kwenye utaratibu huo.

“Mimi mwenyewe nimepita huko, kwa kweli uitikiaji ni ‘positive’, watu wameitikia, kwa wananchi hakuna shida kabisa,” alisema Kamanda Muslim.

LATRA

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Barabara wa Mamlaka ya Usimamizi Usafiri wa Nchi Kavu (Latra), Jahansen Kaharatano, alisema kuhusu tishio la mgomo wa daladala kuhusiana na ‘level Seat ‘ ni Jeshi la Polisi ambao ndio wasimamizi wa agizo hilo lililotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Naomba muwasiliane na polisi ambao ndio wameagizwa kusimamia agizo hilo, kwa sababu hata ofisi yangu hakuna ambaye anafuatilia masuala hayo,” alisema Kahatano.

LATRA CCC

Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi Watumiaji Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu (Latra CCC), Dk. Oscar Kikoyo, amewataka abiria kuchukua tahadhari kwa kupunguza safari zisizo na lazima kwao.

Alisema kila abiria atambue kwamba kujichanganya na abiria wengine pasipo sababu za msingi kunaleta mikusanyiko yenye athari za kiafya, hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa corona.

Aliwataka wamiliki wa daladala kuangalia faida zaidi ya hatua hiyo katika kipindi hiki badala ya hasara.

“Nawashauri wamiliki wa daladala kwenye matatizo wasiangalie faida ila kikubwa waangalie jinsi ya kutatua tatizo,” alisema Kikoyo.

MWANZA       

Mkoani Mwanza pia wameanza kutekeleza agizo la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, kuhusu daladala kutosimamisha abiria.

Kamanda Muliro aliwasisitiza madereva na makondakta kuzingatia maelekezo hayo ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya covid-19 ambavyo vimesababisha janga la dunia la ugonjwa wa corona.

Hata hivyo baada ya utekelezaji kuanza juzi chini ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na watumishi wa LATRA, baadhi ya daladala zilikamatwa zikiwa zimesimamisha abiria na kujikuta zikitozwa faini Sh 250,000 hadi 300,000.

MTANZANIA ilishuhudia ukaguzi uliokuwa ukifanywa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani ndani ya daladala na abiria waliokuwa wamesimama walishushwa  huku madereva wakiandikiwa faini kulingana na makosa yao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda Muliro alisema lengo la kuweka amri hiyo na faini kubwa ni  sehemu ya mikakati ya kujiepusha kuambukizana virusi vya Covid-19 vinavyosababisha ugonjwa wa corona.

“Lengo siyo faini kubwa, bali kusudi letu ni kutaka madereva waache kabisa kusimamisha abiria ili kuepusha kuambukiza ugonjwa wa corona.

“Nirudie kusema ugonjwa huu ni hatari kwa kila mtu na unaua, sasa inashangaza kuona malalamiko wakati tunachokifanya ni kwa faida ya wote.

“Tulianza kushirikishana na kuelimishana vizuri ingawa wengine walitishia kugoma wakidai kwamba watapata hasara na kushindwa kujiendesha kwa faida, lakini tulikumbushana sheria na utaratibu wa vyombo vya usafiri sambamba na vibali walivyopewa.

“Wote tulifikia mwafaka mzuri kwamba hata nauli iliyokuwa imepangwa ilizingatia kila abiria akae kwenye kiti chake, kitendo cha abiria kusimama ni kinyume na sheria zetu, lakini hapa nchini tumezoea kwa sababu ya uhaba wa vyombo vya usafiri, hivyo kutokana na ugonjwa huu tumerudi kusimamia sheria.

“Pesa tunayotoza sisi polisi ya Sh 30,000 kwa kila kosa na ile ya Latra ya Sh 250,000 ni ndogo sana kulingana na uzito wa ugonjwa huu.

“Tunawaomba madereva na wamiliki wa vyombo hivyo wazingatie amri hizo, najua wengine wanalalamikia ubovu wa barabara wakitaka nauli ipandishwe, binafsi nasema pesa hizo wanazotozwa zitarudi baadaye  kuboresha miundombinu hiyo baada ya kuingia katika mfumo rasmi wa mapato na kurejeshwa,” alisema Kamanda Muliro.

HABARI hii imeandaliwa na CHRISTINA GAULUHANGA, SABINA WANDIBA, AVELINE KITOMARY, NORA DAMIANI (DAR) na BENJAMIN MASESE (MWANZA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles