ACACIA yaeleza ongezeko uzalishaji wa dhahabu

0
616

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya ACACIA imesema imepata mafanikio katika uzalishaji wa dhahabu kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa ACACIA, Peter Geleta,  ilisema imekuwa imara na kufikia uzalishaji wa dhahabu wakia 391,000.

“Tuna furaha kubwa kutoa taarifa juu ya utendaji kazi wetu imara kwa kipindi cha tangu mwanzo wa mwaka mpaka sasa tukiwa tumezalisha wakia 391,000 za dhahabu hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 2018.

“Kutokana na hili, tunategemea kuvuka lengo letu la uzalishaji kwa mwaka mzima kutoka wakia 435,000 hadi kufikia 475,000 na sasa tumelenga uzalishaji kupitiliza mpaka kufikia wakia 500,000 kwa mwaka mzima,” alisema Geleta.

Alisema kampuni hiyo  imezalisha wakia 136,640 ndani ya robo hii ya tatu ikiwa ni pungufu ya asilimia 29 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2017 (191,203).

“Hii inatokana na kupungua uzalishaji katika Mgodi wa Bulyanhulu na uchakataji wa mashapo katika mgodi wa Buzwagi. Hata hivyo, pengo hili lilizibwa na uzalishaji wa juu katika mgodi wa North Mara.

“Uzalishaji katika robo hii ulivuka matarajio ya kampuni kutokana na uzalishaji wa hali ya juu katika migodi yote mitatu.

“Wakia 135,875 za dhahabu ziliuzwa katika kipindi hiki   sambamba na kiwango kilichozalishwa,” alisema

Alisema mgodi wa North Mara umezalisha wakia 89,287 za dhahabu katika   robo ya tatu mwaka huu  ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na kiwango kilichozalishwa kipindi kama hicho mwaka jana.

“Mgodi wa Buzwagi umezalisha wakia 36,460 katika robo ya tatu ya mwaka 2018 ambayo ni pungufu ya asilimia 47 ikilinganishwa na robo ya tatu 2017 (69,097).

“Hii ilitokana na kuhamia kwenye uchakataji wa mashapo ya daraja la chini   kwenda sambamba na mpango wa uhai wa mgodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here