25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Abednego Mafuluka: Ni miujiza kupata mapacha wanne

PICHA*Aomba msaada aweze kuwahudumia

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

KWA kawaida watu wawili (mke na mume) wanapoamua kuanza maisha ya ndoa tarajio lao kubwa katika siku za usoni huwa ni kupata watoto.

Mtoto huwa ni kiunganishi muhimu ambacho huongeza furaha na amani katika ndoa nyingi na ndio maana watu huangaika huku na huko pindi wanapokaa kwa muda mrefu bila ya kupata mtoto.

Naweza kusema kwamba furaha ya wanadamu wengi waliokamilika na kuingia kwenye maisha ya ndoa hukamilishwa na kuzaliwa kwa watoto ingawa huwa ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu kwa mja wake.

Familia ya Abednego Mafuluka na Sara Dimosa imejawa na furaha tele baada ya Mwenyezi Mungu kuwajalia kupata watoto pacha wanne April 4, mwaka huu ambapo watatu kati yao ni wa kike na mmoja wa kiume.

Akizungumza na MTANZANIA Mafuluka anasema mkewe Sara alijifungua watoto wake hao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa njia ya upasuaji.

“Kwa kweli nashangaa maajabu ya Mungu, namshukuru kwa kumwezesha mke wangu kujifungua salama. Siku moja alienda kliniki na aliporudi aliniambia kuwa amejulishwa kwamba ana mapacha.

“Wakati ule waliwaona wapo watatu nilijisikia furaha kubwa lakini kumbe walikuwa wanne na amejifungua salama hakika hii ni neema ya ajabu,” anasema Mafuluka.

Huku tukielekea katika wodi namba 10 iliyoko kwenye jengo la wazazi ambako Sara amelazwa kwa mapumziko, Mafuluka anasema ana imani amepata mapacha hao kwa kurithi kutoka kwenye familia yake na ya mkewe.

“Mama yangu mzazi alizaliwa pacha na mwenzake na mke wangu huko kwao kuna dada na shangazi zake ambao walizaliwa pacha,” anasema.

Akiwa amejaa furaha na tabasamu kubwa usoni, Mafuluka anasema jambo analomshukuru Mungu ni kwamba hadi sasa mke wake pamoja na mapacha wake afya zao zinaendelea vizuri.

“Tuna watoto wengine wawili Irene (9) ambaye yupo darasa la kwanza na Precious (5) ambaye ameanza elimu ya awali mwaka huu. Kwa maana hiyo tuna watoto sita,” anasema.
Ashindwa kuwapa majina

Mafuluka anasema familia yake na ya mkewe ilipopata taarifa ya kuzaliwa kwa mapacha hao waliwapongeza huku kila mmoja akitamani kumpatia jina walau mtoto mmoja kati ya hao wanne.

“Kwa kweli wametuletea furaha kwenye familia yetu, kila mmoja anatamani angalau apate nafasi ya kumpatia mtoto hata mmoja jina hadi daktari aliyemuhudumia mke wangu anajisikia fahari kwamba amefanikisha upasuaji huo kwa salama, jambo hili linanipa changamoto bado tunatafakari majina ya kuwaita,” anasema.

Waitwa baba na mama wanne

Tukiwa katika wodi hiyo, kila mmoja anaonekana kuwapongeza wazazi hao huku wakiwatania kwa kuwaita baba na mama wanne jambo ambalo linazidi kuwafurahisha wawili hao.

“Hata mkiwapa majina lakini hili la baba na mama wanne litaendelea kila siku mna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuwasaidia na kuwapa watoto hao,” anasema mmoja wa wauguzi aliyekuwamo ndani ya wodi hiyo.
Mke anena

Akionekana mwenye afya njema mama wa mapacha hao, Sara anasema anajisikia fahari kuwa mama wa watoto hao wanne.
“Nilipokea vyema taarifa ya kujifungua watoto hawa tena wakiwa salama, sikuamini nilibaki namshukuru Mungu kwa kunisaidia maana awali kulikuwa na changamoto nyingi. Ilikuwa safari ndefu ilifika mahali nikawa naumwa nikapewa mapumziko kazini na nikawekwa ‘bed rest’ ,” anasema Sara.

Anasema ingawa alikuwa wakati mwingine akiruhusiwa kwenda nyumbani kwake kupumzika ilimlazimu kuwasiliana na daktari wake pale anapokuwa akijisikia kuumwa.

“Nina matarajio makubwa kwa wanangu naomba Mungu anisaidie wasiugue na hatutarajii kuongeza wengine, nimeshauriana na mume wangu kwamba hawa tulionao kwa sasa wanatutosha, tujitahidi kuwalea vizuri,” anasema.
Waomba msaada

Hata hivyo, wawili hao pamoja na furaha waliyonayo kwa kupata mapacha hao, wanasema changamoto kubwa inayowakabili ni namna watakavyoweza kuwalea na kufanikiwa kuwakuza.

“Mimi ni fundi umeme ambaye nimejiajiri mwenyewe na kama nilivyokueleza dada yangu kwamba nina watoto wengine wawili hivyo wamefikia sita, inanifanya nitafakari jinsi gani nitaweza kuwalea watoto wangu vile inavyostahili ili wakue.

“Kwa hali ya maisha ya sasa ambapo nimepanga na naona naweza kufika mahali nikakwama kuwapatia mahitaji yao mbalimbali.

“Wanahitaji maziwa ya ziada na hili ndilo linalonifanya niwaze zaidi kwa kuwa maziwa ya mama yao hayatoki kwa kiasi ambacho kitawatosheleza wote wanne,” anasema.

Mafuluka anaiomba serikali na wasamaria wema kujitokeza na kumsaidia ili aweze kupata angalau maziwa ya kuwapatia watoto wake ili aweze kutafuta chakula kwa ajili ya familia yake na kutafuta kodi ya pango.

“Nashukuru Mungu pia familia zetu zimepokea kwa furaha juu ya watoto wetu na wamekuwa wakitusaidia lakini hatuwezi kuwategemea kila siku kwa kila kitu. Tunahitaji kuwa na wasichana zaidi ya mmoja wa kutusaidia ambao tutatakiwa kuwalipa mshahara ndio maana tunaomba jamii nayo itusaidie,” anasema.
Enessy Mwambene ni mmoja wa wauguzi walimuhudumia Sara anasema wanajisikia fahari kufanikisha kuzaliwa kwa watoto hao.

Kwa mujibu wa muuguzi huyo, mtoto wa kwanza wa kiume alizaliwa na kilo 2.2, wa pili kilo 1.9 wakati watatu alizaliwa na kilo 1.5 na wanne kilo 1.45.

“Kwa muda mrefu hatujazalisha mama mapacha wanne, wengi wanakuja hapa wanaishia wawili au watatu, hii imekuwa neema kwetu katika mwaka huu na tunashukuru kwamba wamezaliwa salama kwa sababu mara nyingi wengi huzaliwa wakiwa wameungana sehemu mbalimbali za miili yao.

“Lakini kulea watoto wanne si jambo dogo kweli anahitaji msaada, mimi nilijifungua pacha wawili nilipata changamoto je itakuwaje kwa huyu mwenye wanne. Hivyo nawashauri watu wajitokeze ili waweze kumsaidia watoto hawa wakue vyema,” anasema Enessy.

Kwa yeyote atakayekuwa tayari kuisaidia familia hii awasiliane na Abednego Mafuluka kwa namba 0713 816685, 0755 317880.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles