27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi mwingine adaiwa kuua kwa fimbo

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

ASKARI  wa Jeshi la Polisi mkoani  Mwanza,  PC Joel Francis (41)  mwenye namba F.4965 anadaiwa kumpiga Donald Magalata (30)  kwa fimbo na kumsababishia kifo.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni wiki moja  imepita,baada ya askari   mwingine mkoani hapa Dau Elisha  mwenye namba H 852 PC  wa  kituo cha Nyamagana  kumuua askari mwenzake    PC Petro   Matiko wenye namba  H 5950 kwa risasi na baadaye kujipiga  risasi  kichwani na kufariki dunia papo hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema  tukio hilo lilitokea Januari mosi, mwaka huu saa moja asubuhi katika kambi ya Polisi  Mabatini.

Alisema  siku hiyo,  PC Francis alikwenda  nyumbani kwake na kumkuta marehemu ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu  akiwa amelala.

Alisema baada ya askari huyo  kuingia ndani kwake, aligundua pochi yake ya kutunzia fedha, kadi mbili za benki na kitambulisho cha kazi  vyote vilikuwa havionekani ndipo alipoanza kuhoji.

“Marehemu alikuwa rafiki yake PC Francis, alikuwa  akimsaidia kazi mbalimbali za nyumbani, ingawa marehemu  alikuwa akifanya kazi ya ulinzi hotel ya Mwanza   iliyopo katikati ya jiji.

“Sasa mzozo huo, ulisababisha PC Francis kumfunga  pingu  miguuni marehemu na kuanza kumpiga ovyo sehemu mbalimbali za mwili  kwa kutumia fimbo kitendo kilichosababisha kupiga kelele kuomba msaada.

“Kelele za kuomba msaada ziliwafanya majirani zake pale kambini wafike na kumkuta akiwa na hali mbaya na kumchukua hadi Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili matibabu,”alisema.

Alisema  kutokana na kipigo alichopata, marehemu  alifariki Januari 2, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu.

Alisema tayari jeshi hilo, linamshikilia Pc Francis kwa mahojiano juu ya tukio hilo na atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa taratibu wa kijeshi.

Kamanda Kamugisha, alisema anashangazwa na tukio hilo kufanywa na askari ambaye anapaswa kusimamia sheria na haki za binadamu, huku akisisitiza kitendo hicho kisichukuliwa kama maadili na maagizo ya jeshi la polisi, bali ni tabia ya mtu mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles