27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sheikh Farid azua tafrani mahakamani

Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed
Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43), jana amezua tafrani mahakamani baada ya kuhoji kwanini anashitakiwa Tanzania Bara kwa ugaidi wakati Zanzibar ni nchi ambayo ina Mahakama Kuu.

Sheikh Farid alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa baada ya kuunganishwa na watuhumiwa wengine 19 wa ugaidi na kufanya idadi yao kufikia 20.

“Mheshimiwa hakimu, sisi wote hapa tunatoka Zanzibar, hatuna ndugu hapa, gerezani wanazuia watu wasije kutuona.

“Tumetolewa Zanzibar tumekuja kushitakiwa huku Tanganyika,  kwani Zanzibar hakuna Mahakama Kuu? kwanini tusishitakiwe kwenye nchi yetu?

“Zanzibar ina kila kitu, yupo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nchi yetu inafanywa kama si nchi, tunashangaa kushitakiwa hapa, tumeletwa kuonewa tu, sisi watuhumiwa tu, tumeshaonewa sana, hasa mimi nimechoka kuonewa,” alisema Sheikh Faridi.

Alisema kama hakimu atataka kujua kila mshitakiwa ana jambo gani, wataeleza kwani kila mmoja ana jambo lake la kulalamikia.

Hata hivyo, Jamhuri ikiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benard Kongola, ilidai hakuna maelekezo yoyote ya kuwakataza ndugu wa washitakiwa kufika gerezani kuwaona.

Hakimu Riwa, alisema ataangalia sheria inasemaje, na kwamba alikuwa anahisi labda wanafanya hivyo kutokana na uzito wa mashitaka yanayowakabili, na upelelezi haujakamilika.

“Mashitaka ya ugaidi hapa nchini ni mapya, nitaenda kusoma zaidi kuangalia inakuwaje,” alisema Hakimu Riwa.

Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kongola, Sheikh Faridi na wenzake, inadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014 katika  maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama ya kutenda kosa la kuingiza watu nchini kufanya ugaidi.

Katika shitaka la pili, wanadaiwa katika kipindi hicho walikubaliana kumuingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.

Kongola alisema Shitaka la tatu, linamkabili Sheikh Faridi peke yake, ambaye anadaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014 maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akijua ni kosa, alimuingiza nchini Sadick na Farah kufanya ugaidi.

“Sheikh Faridi pia anadaiwa kuwahifadhi Sadick na Farah huku akijua watu hao walitenda vitendo vya kigaidi,” alisema Kongola.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote, kwa kuwa upelelezi haujakamilika na mahakama iliahirisha kesi hadi Agosti 21, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo, ni Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally na Juma Juma.

Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro na Said Sharifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles