30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘Sekta ya Elimu taabani’

12NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

UBORA wa elimu katika Serikali ya Awamu ya Nne umetajwa kushuka kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu kutokana na kukosekana kwa falsafa ya kuendeleza elimu licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa Uzinduzi wa Ripoti ya Elimu ya Miaka 10 ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage, alisema katika kipindi cha uongozi wa Kikwete kumekuwa na fursa za elimu kwa watoto wengi nchini lakini ubora wa elimu hiyo umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka.

Kalage alisema endapo falsafa ya kuendeleza elimu nchini haitajengwa, vyuo vya elimu ya juu nchini vipo hatarini kufungwa kutokana na kukosekana wanafunzi wenye sifa.

“Katika kipindi cha uongozi wa Kikwete kumekuwa na upanuzi wa vyumba vya madarasa, idadi ya walimu, udahili pamoja na kuimarika idadi ya jinsia ya wanaojiunga na kuhitimu elimu mbalimbali, lakini ubora wa elimu umekuwa ukizidi kudorora kutokana na wanafunzi wengi kukosa sifa.

“Kwani shule za msingi katika kipindi hicho zimeongezeka kutoka 14,257 kwa mwaka 2005 hadi kufikia 16,538 mwaka 2015 aliomaliza muda wake na wanafunzi wakiongezeka kutoka 7,541, 208 hadi kufikia 8,202, 892, shule za sekondari 1, 745 mwaka 2005 hadi kufikia 4,753 mwaka 2015 huku idadi ya wanafunzi wa sekondari ikiongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi kufikia 1,804, 056 mwaka 2015,” alisema Kalaghe.

Kuhusu vyuo vya ufundi, alisema viliongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi kufikia 744 mwaka 2015 huku wanafunzi wakiongezeka katika vyuo hivyo kutoka 40,059 hadi kufikia 145,511 mwaka 2015.

Pia alisema kuwa katika kipindi hicho hicho bajeti ya elimu ilikuwa kubwa zaidi kuliko sekta nyingine yoyote na iliongezeka kutoka Sh bilioni 669.5 mwaka 2005/2006 hadi Sh trilioni 3.4 mwaka wa fedha wa 2014/2015 na ongezeko hilo liliwezesha asilimia 98 ya watoto wanaostahili kupata elimu kuandikishwa na udahili kwa shule za msingi kuongezeka kwa asilimia 26.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye pia ni mtafiti wa ripoti hiyo, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kutokana na kukosekana kwa falsafa ya elimu mambo mengi ya kielimu yameshindwa kuendelezwa.

Alisema inasikitisha kuona shule nyingi nchini zikiwemo zenye historia ya kipekee kama Tambaza, Bwiru, Pugu, Tabora na nyingine zikiwa zimechoka kutokana na miundombinu yake kuchakaa.

“Hadi sasa ukiangalia shule za sekondari za Serikali zinazosimama ni asilimia chache tu jambo ambalo ni aibu,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema Kikwete alifanikiwa katika utawala wake kukomesha udini na aliondoa ubaguzi kwa shule za kidini kuchagua aina ya wanafunzi kulingana na dini.

“Kwa asilimia 26, Kikwete alipanua elimu lakini pia Rais mstaafu Benjamini Mkapa naye alifanya kazi kubwa katika suala la elimu na ndiyo maana falsafa yake inaendelezwa hadi leo,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema mashirika mbalimbali yamefanya utafiti na kubaini watoto wengi hawajui kusoma wala kuandika na wengi wao hawafahamu Kiingereza.

Mkumbo alisema mbali ya kuwekeza katika elimu lakini ubora haupo na fedha nyingi zimetumika katika makongamano na posho.

Alisema ni vyema Serikali ya sasa ikajitahidi kuwekeza katika elimu ili kuondoa changamoto iliyopo sasa.

Pia alisema kwa sasa kuna vyuo kama UDSM na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) havina wanafunzi katika baadhi ya kozi kutokana na kukosekana wanafunzi wenye sifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles