23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Basi la Takbir laua watu 12

PgNA SEIF TAKAZA,  IRAMBA

WATU 12  wamefariki dunia papo hapo na wengine 19 kujeruhiwa, baada ya basi la Kampuni ya Takbir kugongana na lori la mafuta katika Kijiji cha Kizonzo, Shelui Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Ajali hiyo ilitokea katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Mwanza.

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, aliwaambia waandishi wa habari jana  kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 1.30 usiku  wakati basi hilo lilipokuwa  likitoka Dar es Salaam kwenda Geita.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori,   Charles Kayene ambaye baada ya ajali hiyo  alitoroka na anatafutwa na polisi.

“Dereva huyo alikuwa akiendesha lori ya Scania   namba   T 230 BRJ.

“Kabla ya ajali dereva huyo alikuwa akitaka kuyapita magari mengine  lakini kwa bahati mbaya alipoteza mwelekeo na kusababisha ajali hiyo.

“Lori hilo lilikuwa na tela   namba   T 314 CTS lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam,” alisema Kamanda Sedoyeka.

Alisema hadi sasa waliofariki dunia   hawajatambuliwa na wala haijulikani mahali walikokua wakienda, ingawa basi hilo husafiri kati ya Dar es Salaam na Geita.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dk. Timoth Sumbe, alisema walipokea maiti 12 na majeruhi 19.

Alisema kwa kuwa hospitali hiyo haina chumba kikubwa cha kuhifadhi maiti,  baadhi ya maiti ilisafirishwa kwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Singida.

Alisema majeruhi watano wako katika hali mbaya na   wanatarajia kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Bugando  mkoani Mwanza  kwa   matibabu zaidi.

Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo,   Oscar Uzengi, aliiambia MTANZANIA kuwa mwendo wa basi lao ulibadilika na kuwa wa kasi baada ya dereva wa pili wa basi hilo kuliendesha walipofika Singida.

Alisema  walianza safari  Dar es Salaam katika hali ya kawaida ingawa walikamatwa na polisi wa usalama barabarani baada ya kufika Singida.

“Mimi nilikuwa nimekaa viti vya mbele nilikuwa nikiona mwendo wa gari ukiwa wa kawaida ingawa tulipofika Singida  tulikamatwa na trafiki.

“Baadaye aliingia dereva mwingine na hapo ndipo mwendo ulianza kuwa wa kasi na kuwafanya baadhi ya abiria wakawa wanalalamika kwa sauti za chini chini.

“Kwa bahati mbaya  haukupita muda mrefu  ndipo ajali ikatokea na kusababisha madhara haya,” alisema abiria huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles