24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waliomvamia Jaji Mgeta waenda jela miaka 30

Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewahukumu watuhumiwa wanne kwenda jela miaka 30 kwa makosa matano, likiwamo la kuvunja na kunyang’anya kwa kutumia silaha nyumbani kwa Jaji John Mgeta.

Mtuhumiwa mmoja katika kesi hiyo aliachiwa huru.

Watuhumiwa wanadaiwa kufanya tukio hilo maeneo ya Tegeta Ununio jijini Dar es Salaam.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Warioba, Abdulkarim Mohamed, Seif Said na Lusekelo Godfrey ambao kwa pamoja walitenda kosa hilo Januari 18, mwaka 2012 saa tisa usiku baada ya kuvamia nyumba hiyo na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 15.5.

Alisema mahakama hiyo ilisikiliza mashahidi 12 kutoka upande wa Jamhuri na kubaini kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa yanayowakabili na walikula njama sababu ilionyesha walikuwa wanawasiliana.

Hata hivyo, upande wa mashtaka uliunga mkono ushahidi wao kwa kufikisha vielelezo ambavyo vilipokewa.

Kutokana na mahakama kujiridhisha bila kuacha shaka, imewaona washtakiwa wana hatia, hivyo imewatia hatiani kwa makosa matano.

Kabla ya kutoa adhabu, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Edson Mwavanda, aliiomba mahakama hiyo kuwapa adhabu kali watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Kwa upande wa washtakiwa hao, kwa pamoja waliomba mahakama hiyo kuwaachia huru kwa madai kuwa walishakaa jela zaidi ya miaka minne.

“Ninaiomba mahakama yako kutuachia huru kwa sababu hatujatenda kosa hilo, halafu tumeshatumikia jela zaidi ya miaka minne,” alisema Warioba ambaye ni mshtakiwa wa kwanza kwenye kesi hiyo.

Akitoa adhabu, Hakimu Kisoka alisema kutokana na hali hiyo, mahakama imewahukumu kwenda jela miaka 37, ambapo miaka 7 kwa kosa la kula njama na miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha, huku adhabu hizo zikienda pamoja.

“Mahakama imemuachia huru mtuhumiwa namba tano kwenye kesi hii, Benjamini Macklin baada ya kubaini hana hatia yoyote,” alisema Hakimu Kisoka.

Jaji Mgeta ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alivamiwa nyumbani kwake Januari 18, 2012 ambapo kabla ya kufanya tukio hilo, washtakiwa hao walimfunga kamba za miguu na mikono jaji huyo na familia yake na kuwatishia kwa mapanga, visu na nondo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles