23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Sifadhili ACT-Tanzania

Edward Lowassa
Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema hatua ya kuhusishwa kwake na Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) ni upuuzi na mwendelezo wa mikakati ya kumchafua.

Kauli ya Lowassa imekuja siku moja baada ya kuhusishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), kwamba kwa pamoja wamekuwa wakipanga mikakati ya siri ya kuhujumu chama hicho.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam kutoka katika ofisi ya Lowassa ilisema habari zilizoandikwa na moja ya magazeti ya kila siku (si MTANZANIA) hazina kweli na zina lengo la kumchafua na kumgonganisha.

“Habari hizi ni uzushi na ni mwendelezo wa mikakati ya kumchafua na kumgonganisha na wanasiasa wenzake wa kada na maeneo mbalimbali.

“Lowassa kama walivyo wabunge wengine wa CCM, amekuwa na uhusiano na wabunge wenzake bila kujali tofauti ya vyama vyao. Ni kiongozi makini ambaye hawezi kupoteza muda wake kujiingiza katika masuala yasiyo na tija kwa nchi, wananchi na ustawi wa demokrasia makini na endelevu nchini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alisema anatumia muda wake kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM jimboni kwake, Monduli.

“Mimi na chama chetu tuna jukumu kubwa la kutekeleza ilani yetu, kuwaletea maendeleo wananchi ili wazidi kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika chaguzi zijazo,” ilisema taarifa hiyo.

Lowassa alisema anathamini mchango wa vyama vyote vya siasa nchini pamoja na Chadema katika kujenga demokrasia yenye tija kwa Taifa.

Jana moja ya magazeti ya kila siku (si MTANZANIA) lilidai kugundua kuwa Lowassa ndiye mfadhili mkuu na mpanga mkakati mkuu wa kundi linalomfuata Zitto ambalo limeanzisha chama ACT-Tanzania.

Linadai kwa wiki kadhaa za hivi karibuni makundi ya wanachama, washauri na wapanga mikakati wa Lowassa na Zitto wamekuwa wakikutana katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam na kupeana mbinu, lengo kuu likiwa ni jinsi ya kukimega CHADEMA vipande vipande ili kidhoofike kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ilielezwa kazi kubwa anayoona mbele yake ni kuanza mapema kusambaratisha CHADEMA ili kupunguza upinzani wakati wa kampeni utakapofika.

Zitto amekuwa akitajwa kuwa ndiye mwasisi mwenza wa ACT na amekuwa na uhusiano wa “kikazi” na Lowassa, hata kabla hajaingia kwenye matatizo ya wazi na chama chake, ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilimvua nyadhifa zote za uteuzi kutokana na tuhuma mbalimbali.

Hata hivyo, inadaiwa Zitto anatarajiwa kujiunga rasmi na ACT mwanzoni mwa Septemba, mwaka huu na timu ya Lowassa imedhamiria kumfadhili ili kujenga taswira ya mpasuko ndani ya CHADEMA.

Mbali ya hilo, madai mengine yalidaiwa kuwa moja ya ajenda ni kufadhili na kupandikiza watu ndani ya mfumo wa CHADEMA ambacho kinaendelea na uchaguzi wa ndani, ili wapate nafasi za uongozi, wazitumie kupata taarifa na mipango ya chama na baadaye wajivue nafasi hizo na kukimbilia ACT ili kuleta msisimko wa kitaifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles