24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu Mpya ni Majaliwa Kassim

 

kassimNA MAREGESI PAUL, DODOMA

WAZIRI Mkuu mteule, Kassim Majaliwa, amesema hakutegemea kupata nafasi hiyo baada ya Bunge kumpitisha kwa kura nyingi jana.

Majaliwa alitoa kauli hiyo bungeni alipokuwa akiwashukuru wabunge dakika chache baada ya Bunge kumthibitisha kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano kwa kupata kura 258 kati ya 351 zilizopigwa.

“Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuongoza wote kuwa hapa leo, na nawashukuru wabunge wote kwa kupitisha jina langu.

“Namshukuru pia mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuniteua kuwa Waziri Mkuu wa nchi yetu.

“Nawashukuru sana waheshimiwa wabunge kwa kupitisha jina langu kwa kura nyingi, nawashukuru sana kwa sababu sikutegemea kabisa jambo hili kwani ni jambo kubwa, lakini nimelipokea vizuri.

“Mheshimiwa Spika, wakati unaendesha mchakato huu, mimi nilikuwa nikikuangalia kupitia televisheni, nikawa naona unavyofungua jina kwenye bahasha tatu.

“Kwahiyo, napenda kuwahakikishia kwamba, nitawapa ushirikiano wa hali ya juu waheshimiwa wabunge wote bila kujali tofauti za vyama vyenu.

“Tutafanya kazi pamoja kufuatilia shughuli za maendeleo, na nitasikiliza kila ushauri mtakaonipa kwa sababu najua wote mna kiu ya maendeleo.

“Kwa leo (jana), sikuwa na maandalizi yoyote ya kuzungumza na hata kwenye karatasi hii sijaandika kitu, lakini itoshe tu kuwahakikishia, kwamba nitashirikiana na nyinyi na nitatembelea maeneo yenu kuona changamoto mlizonazo na kuona maendeleo mliyofikia,” alisema Majaliwa.

 

WABUNGE WAZUNGUMZA

Baada ya uteuzi huo, baadhi ya wabunge walipewa fursa ya kuchangia ambapo walisifia uteuzi huo wa Rais Magufuli na kusema kwa nyakati tofauti, kwamba Majaliwa ni mchapakazi na mwadilifu anayejali masilahi ya taifa.

Aliyekuwa wa kwanza kuchangia ni Mbunge wa Isimani, William Lukuvi (CCM), aliyesema uteuzi wa Majaliwa umekuja wakati mwafaka kwa kuwa ana uwezo wa kushika nafasi hiyo.

“Huu ni uteuzi makini na ni uteuzi sahihi kwa sababu namfahamu Majaliwa, nimewahi kufanya naye kazi, najua ni mwadilifu, ni msikivu na ni mfuatiliaji,” alisema Lukuvi.

Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM), pamoja na kuunga mkono uteuzi huo, alisema Majaliwa ni kati ya viongozi wachapakazi watakaomsaidia Rais Magufuli katika utendaji kazi wake.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamis Kigwangala (CCM), alimmwagia sifa Majaliwa na kusema ni msikivu, mnyenyekevu na ana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo.

Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM), alisema baada ya Watanzania kumpata rais ambaye ni tingatinga, Tanzania imempata Waziri Mkuu makini ambaye ni mara chache watu wa aina hiyo kuzaliwa duniani.

Naye Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), alisema alimfahamu Majaliwa tangu mwaka 2006 wakati alipokuwa Mkuu wa Wilaya moja nchini.

Kwa mujibu wa Chenge, alipofuatilia utendaji kazi wa Waziri Mkuu huyo mteule, aligundua kuwa ni kati ya Watanzania wenye uwezo mkubwa wa kuiongoza nchi.

 

WABUNGE WA UPINZANI

Wakati wabunge wa CCM wakimsifia Majaliwa, baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani, walionyesha kutoridhishwa na uteuzi huo kwa kuwa Majaliwa si aina ya Waziri Mkuu anayetakiwa na Watanzania.

Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alisema Majaliwa hana kasi, na kwamba hatamsaidia Rais Magufuli katika utatuzi wa kero za Watanzania.

“Hana jipya, hana uwezo wa kuwa waziri mkuu bali kilichofanyika ni rais kuteua mtu mwenye uwezo wa chini yake,” alisema Silinde.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema Majaliwa hana makundi, ni msikivu na ni mwadilifu, lakini hana uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoikabili Serikali.

Kutokana na hali hiyo, alisema hatarajii jambo jipya kutoka serikalini kwa kuwa watendaji wa aina ya Majaliwa, hawatakiwi katika kipindi hiki ambacho taifa limejaa matatizo.

 

MCHAKATO ULIVYOKUWA

Mchakato wa Bunge kumthibitisha Majaliwa kuwa Waziri Mkuu, ulianza jana saa tatu asubuhi baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusoma dua ya kuliombea Bunge.

Baada ya dua hiyo, Spika Ndugai aliwatangazia wabunge, kwamba kazi iliyokuwa mbele yao kwa wakati huo ni kuthibitisha jina hilo litakalowasilishwa kwake na Rais Magufuli.

Uwasilishwaji wa jina hilo ulichelewa, na hivyo wabunge kulazimika kusubiri hadi saa 3:45, bahasha yenye jina la waziri mkuu mteule ilipowasilishwa kwa Spika na mlinzi binafsi wa rais akiongozwa na askari wawili wa Bunge.

Bahasha hiyo iliyokuwa na bahasha nyingine ndogo mbili ilipokabidhiwa kwa Spika, alimuita Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah ili washirikiane kuifungua kwa kuwa ilikuwa imefungwa na gundi maalumu.

Saa 3:38, ufunguzi huo ulikamilika ambapo Spika Ndugai alisoma jina la waziri mkuu mteule huku akisema karatasi yenye jina hilo ilikuwa imeandikwa kwa mkono na Rais Magufuli.

Baada ya hatua hiyo, wabunge walipiga kura za kukubali uteuzi huo na matokeo hayo yalisomwa na Dk. Kashilillah baada ya kura kuhesabiwa.

“Kazi ya kuhesabu kura imekamilika na kwa mujibu wa Katiba, wabunge wanaotakiwa kikatiba ni 394. Lakini hadi sasa wabunge waliosajiliwa ni 369 na akidi inayotakiwa ni wabunge 184.

“Wakati kura zinapigwa, wabunge waliokuwa ukumbini ni 351, kura zilizopigwa ni 351, kura zilizoharibika ni mbili na kura halali ni 349.

“Kura za hapana ni 91 ambazo ni sawa na asilimia 25.9, kura zilizoharibika ni mbili ambazo ni sawa na asilimia 0.06 na kura za ndiyo ni 258 ambazo ni sawa na asilimia 73.5,” alisema Dk. Kashilillah.

Baada ya matokeo hayo, Spika Ndugai alimtangaza Majaliwa kuwa ndiye Waziri Mkuu mteule atakayeapishwa leo katika Ikulu ndogo ya Chamwino mjini Dodoma.

Hatua hiyo ilipokamilika, wabunge walipumzika kwa dakika 45 na waliporudi bungeni saa 4:45, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisoma wasifu wa Majaliwa na kutoa hoja ya wabunge kuidhinisha uteuzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles