24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli apeleka jina la Waziri Mkuu bungeni

SAM_2397NA MWANDISHI WETU, DODOMA

RAIS Dk. John Magufuli amewasili mjini Dodoma jana, huku akiwa na siri nzito ya jina la Waziri Mkuu ambalo anatarajia kuliwasilisha bungeni kesho.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge iliyotolewa wiki iliyopita, jina la Waziri Mkuu litawasilishwa kesho na Rais Magufuli kwa Spika Job Ndugai.

Baada ya kuwasilisha jina hilo, litasomwa mbele ya wabunge wote na kuthibitishwa, kisha watapiga kura ya kumchagua.

Baada ya kuthibitishwa kwa Waziri Mkuu, siku hiyo hiyo Naibu Spika atachaguliwa na kula kiapo cha uaminifu, na baada ya hapo wabunge watajiweka tayari kwa hotuba ya kwanza ya Rais Magufuli, itakayotolewa keshokutwa saa kumi jioni.

Baada ya Rais Magufuli kumaliza kuhutubia Bunge, litaahirishwa na Waziri Mkuu hadi tarehe itakayotajwa.

Dk. Magufuli aliwasili mkoani Dodoma akitumia usafiri wa njia ya barabara kitendo ambacho ni nadra kufanywa na viongozi wakubwa wa taifa hili.

Itakumbukwa hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, Dk. Magufuli alitumia usafiri wa barabara kupiga kampeni nchi nzima karibu miezi miwili.

Hali hiyo, ni tofauti na watangulizi wake, ambao kwa nyakati tofauti za kampeni mwaka 2005 na 2010 walitumia usafiri wa helikopta (Chopa) kuzunguka nchi nzima.

Watanzania wengi wanaamini Waziri Mkuu ajaye atatoa picha kamili ya mwelekeo wa Rais Magufuli katika suala zima la utendaji kazi wa kila siku wa Serikali yake yenye kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi tu’.

Viongozi waliowahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere (1961-1962), Rashid Kawawa (1962 na 1972-1977) na Edward Sokoine (1977-1980, 1983-1984) ambao wote ni marehemu.

Wengine ni Cleopa Msuya (1980-1983, 1994-1995), Dk. Salim Ahmed Salim (1984-1985), Joseph Sinde Warioba (1985-1990), John Malecela (1990-1994), Frederick Sumaye (1995-2005), Edward Lowassa (2005-2008) na Mizengo Pinda (2008-2015).

 

NAIBU SPIKA

Katika hatua nyingine, wingu zito limetanda katika mchuano wa kumpata Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hali hiyo imekuja, baada ya Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama ambaye awali alitajwa kuchukua fomu ya unaibu spika na hivyo kutarajiwa kutoa upinzani mkali dhidi ya Dk. Tulia Akson kutofanya hivyo.

Habari zilizopatikana mjiniDodoma jana zilidai Mhagama aliamua kutogombea nafasi hiyo ili kumpa nafasi Dk. Tulia kushinda nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chanzo cha habari kutoka mjini humo kililiambia MTANZANIA kuwa, Mhagama alikuwa amejiandaa kugombea
nafasi hiyo baada ya kuombwa na wabunge wengi wa CCM na yeye kukubali, lakini alibadili uamuzi wake baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni ‘kutishwa’ na wakubwa asigombee.

“Wabunge wengi wa CCM walimtaka Mhagama agombee nafasi hiyo kwa sababu anao uzoefu wa miaka mingi, akiwa
Mwenyekiti wa Bunge la 10 akisaidiana na Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu pamoja na Mbunge wa Viti Maalum,
Lediana Mng’ong’o,” kilisema chanzo hicho.

Pia zipo taarifa zinazoeleza kuwa baadhi ya wabunge wa CCM wameapa kutomuunga mkono mgombea aliyeletwa
na ‘wakubwa’ huku wakitishia kuwa kama ni suala la kuangalia jinsia basi wako tayari kumpigia mgombea wa Ukawa ambaye ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF).

Mhagama ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa CCM alipotakiwa kuzungumzia taarifa kwamba nia yake ya
kuwania nafasi hiyo imesitishwa na baadhi ya vigogo wa Serikali wanaotaka Dk. Tulia achukue nafasi hiyo, alisema
hakugombea nafasi hiyo ili kuwaachia nafasi wengine wawe viongozi.

“Katika chama chetu kila mwanachama ana fursa na haki ya kugombea nafasi anayoona anaiweza.

“Sijapata maagizo ya kuondoa jina langu, wala sijachukua fomu, kwa hiyo, hizo taarifa hazina ukweli wowote.
“Pamoja na kwamba sigombei, bado naamini waliogombea ni viongozi wazuri na naamini tutampata naibu spika mzuri kupitia hao waliogombea,” alisema Mhagama.

Katika mkutano huo, Mhagama aliwataja wabunge wa chama hicho waliochukua fomu za kugombea unaibu Spika wa Bunge kuwa ni watano.

“Hadi sasa kuna wabunge watano wa CCM wamechukua fomu kuwania nafasi ya Naibu Spika wa Bunge na tayari
wameshazirudisha.

Wabunge hao ni Dk. Tulia Akson, Sadifa Juma Hamis, Mussa Zungu, Mariam Kisangi na Bahati Ally
Abeid.
“Kwa hiyo, leo usiku (jana), vitafanyika vikao viwili kujadili na kuchuja majina haya ambapo kikao cha kwanza kitakuwa ni cha kamati ya uongozi ya wabunge wa CCM ambacho kitachuja wagombea hao na kubakisha majina matatu.

“Majina hayo matatu, yatawasilishwa katika kikao cha wabunge wote wa CCM ambao jukumu lao litakuwa ni kupitisha jina moja litakalopelekwa Ofisi ya Katibu wa Bunge kwa ajili ya kushindanishwa na wagombea
wengine bungeni,” alisema Mhagama.

Wakati CCM wakijadili majina hayo matano, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameshapitisha jina la Magedelena Sakaya (CUF) kuwania nafasi hiyo kwa niaba ya vyama vinne vinavyounda umoja huo.

Naibu Spika wa Bunge anatarajia kuchaguliwa leo baada ya Spika wa Bunge kupatikana jana.

NDUGAI USPIKA

Katika hatua nyingine, aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la 10 na Mbunge wa Kongwa (CCM), Job Ndugai, amechaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 11.

Ndugai alichaguliwa kushika wadhifa huo jana, baada ya kuwashinda wapinzani wake saba aliokuwa akigombea nao
katika nafasi hiyo.

Kwa ushindi huo, Ndugai anakuwa Spika wa saba wa Bunge hilo akitanguliwa na Spika wa kwanza, Karimjee,
Adam Mkwawa, Ernest Mang’enya, Pius Msekwa, Samuel Sitta na Anne Makinda.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa kumpata Spika wa Bunge jana, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alisema Ndugai alishinda kwa asilimia 70, baada ya kupata kura 254 kati ya kura 365 zilizopigwa.

Wakati Ndugai akipata ushindi huo, aliyefuata alikuwa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa
zamani, Gudluck ole Medeye aliyekuwa akigombea kupiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyepata kura 109.

“Hadi sasa wabunge waliosajiliwa ni 368 na kura zilizopigwa wakati wa kumchagua Spika ni 365, lakini kura mbili ziliharibika.

“Mgombea Dk. Godfrey Malisa wa Chama cha CCK, amepata kura sifuri, Gudluck ole Medeye wa Chadema amepata kura 109, Hashimu Rungwe wa Chauma amepata kura sifuri, Hassan Almas wa NRA amepata
kura sifuri, Job Ndugai wa CCM amepata kura 254, Peter Sarungi wa AFP amepata kura sifuri, Richard Lyimo wa TLP amepata kura sifuri na Alexander Kasinini wa DP amepata kura sifuri.

“Kwa matokeo hayo, mshindi  wa kiti cha uspika ni Job Ndugai wa CCM aliyepata kura 254 ambazo ni sawa na asilimia 70,” alisema Dk. Kashilillah.
Hata hivyo, Rungwe wa
Chauma ambaye alikuwa ni mgombea urais wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu, hakuwapo bungeni wakati wa
kujieleza, ingawa Dk. Kashilillah alisema alikuwa amethibitisha kuwapo bungeni kwa ajili ya kuomba kura.

ATOA AHADI

Akizungumza baada ya kula kiapo cha utii, Ndugai aliahidi kuongoza Bunge hilo bila ubaguzi, huku akiahidi
kuwatendea haki wabunge wote.
“Ushindi huu kwangu ni historia ambayo sitaisahau kwa sababu nilipokuwa mdogo, kuna swali nilikuwa namuuliza sana mama yangu mzazi.
“Mimi ni mtoto pekee kwa mama yangu, nilipokuwa mdogo nilikuwa namuuliza mama kwa nini niko peke yangu, wakati kwa majirani zetu kuna watoto wengi.
“Nilikuwa namwambia mama aende zahanati akachukue mtoto kwa sababu nilikuwa nikijua watoto wanapatikana zahanati.

Kwa bahati mbaya, sikumbuki mama yangu alikuwa akinijibu nini.
“Pamoja na kuzaliwa peke yangu, hivi sasa nina ndugu wengi, nina marafiki wengi na sasa wamenichagua kuwa Spika.

“Kwa hiyo, nawaahidi kufanya kazi bila upendeleo wowote, nitafanya kazi kwa kufuata kanuni, nitatenda haki
kwa kila mbunge na kwa kila chama kwa sababu nafahamu matarajio ya Watanzania kupitia Bunge hili.

“Namuahidi pia rais wetu, John Magufuli, kwamba tutampa ushirikiano kilawakati,” alisema Spika Ndugai
Pamoja na hayo, aliwashukuru maspika waliomtangulia kwa kile alichosema kuwa wamemlea na kumsaidia kwa nyakati tofauti kuwa na uelewa mpana wa masuala ya uongozi wa Bunge.

Aliwataja maspika hao kuwa ni Pius Msekwa, Samuel Sitta na Anne Makinda akisema kuwa alijifunza mambo mengi kwake tangu alipokuwa naibu spika wake katika Bunge la 10.

Awali wagombea wa nafasi hiyo walipokuwa wakiomba kura kwa nyakati tofauti, walisema wana uwezo wa kuongoza Bunge kwa sabab wanajua majukumu ya spika na wajibu wake kwa wabunge.

NAPE

Katika hatua nyingine, mgombea ole Medeye alisema amemsamehe Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM)
baada ya kumuuliza swali alilosema ni la kuudhi.

“Kuna mbunge hapa aliniuliza swali ambalo katika lugha za kibunge tunaliita ni swali la kuudhi. “Mbunge huyo namsamehe, sina chuki naye kwa sababu najua kinachomsumbua ni utoto tu, akikua ataacha,” alisema Ole
Medeye.

Ingawa hakumtaja moja kwa moja, kauli hiyo ya ole Medeye ilionekana kumlenga Nape kwa kuwa kati ya wabunge watatu waliomuuliiza maswali wakati akiomba kura, Nape ndiye aliyeuliza swali la uchokozi ambalo Mwenyekiti wa Muda wa Bunge, Andrew Chenge, alimzuia ole Medeye asilijibu kwa kuwa halikuwa swali.

Katika swali lake, Nape alimtaka mgombea huyo aeleze kama ameacha tabia yake ya ubaguzi kwa kuwa aliyekuwa
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) aliwahi kumtuhumu bungeni, kwamba ni mbaguzi.

Wakati huo huo, wabunge jana walianza kuapa ambapo wabunge saba waliapa kabla Bunge halijaahirishwa saa saba
mchana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles