33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waislamu watakiwa kulinda amani

Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal

MANENO SELANYIKA NA ASIFIWE GEORGE

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amewataka Waislamu kote nchini kuhakikisha wanadumisha amani na umoja.

Mbali na kutoa wito huo, Dk. Bilal alilaani mauaji yaliyotokea nchini Palestina na kuwataka viongozi wote duniani kukaa na kujadili namna ya kurejesha amani hiyo.

Kauli hiyo aliitoa jana kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa Shaaban Simba, katika ibada maalumu ya Sikukuu ya Idd El Fitri, iliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.

Alisema kutokana na mauaji yanayoendelea Palestina, ni wajibu wa kila kiongozi kukemea vitendo hivyo ili kila mtu aweze kuishi kwa amani.

“Ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kulitokea vitendo vingi vya mauaji na umwagaji damu nchini Palestina, lakini cha kushangaza hakuna kiongozi yeyote au taasisi za kutetea haki za binadamu waliojitokeza kuongelea masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Ni wajibu wa kila Mwislamu pamoja na taasisi mbalimbali za kidini kushirikiana na viongozi  kuhakikisha kwamba wanadumisha amani na umoja wetu.

“Yale yote mema tuliyoyafanya katika mfungo wa mwezi mtukufu tunatakiwa kuyaendeleza kwa kutoa zaka na sadaka, ikiwa ni pamoja na  kuwasaidia watu wasiojiweza.

“Pia kila mzazi anatakiwa kuendelea kuwafundisha mema  watoto wetu  ili waendelee kukua vyema kiimani, kwani ndio tegemeo la kesho kwa Taifa letu,” alisema Bilal.

Dk. Bilal alisema nchi hii ina viongozi wema, hivyo amewataka kuendelea kudumisha amani tuliyonayo ili iweze kuendelea na kustawi.

Hata hivyo, aliwataka wananchi wote duniani kusherehekea sikukuu hii kwa kumtukuza Mtume Muhammad (S.A.W).

Kwa upande wa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema waumini wa dini ya  Kiislamu wametimiza nguzo ya nne kati ya tano za Uislamu na kuwataka kutotenda dhambi.

Alisema siku ya leo (jana) ni siku maalumu ya kuliombea Taifa kuwa na amani na kudumisha mahusiano na mshikamano.

Alisema vipo vitendo mbalimbali vya urushaji mabomu ambavyo vinaendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hivyo aliwataka watu wanaofanya uhalifu huo kuacha, kwani ni moja kati ya vitendo vibaya ambavyo vilikatazwa na Mtume Muhammad.

“Kitabu Kitakatifu cha Kuran kinatueleza kwamba tuishi na watu wa dini nyingine kwa upendo na amani tusifarakane baina yetu, kwani ni haramu kwa kuwa tumeumbwa kiakili na kwa ufahamu, hivyo si busara kufanya hivyo.

“Kilichobaki sisi Watanzania ni kumwomba Mungu atupe amani na kutuepusha na umwagaji damu kama ule unaoendelea, hasa katika mataifa mengine ya Kiarabu na mengineyo ambayo husababisha kupoteza uhai wa binadamu na mali nyingi kupotea, hivyo kusababisha uchumi kutikisika ndani ya nchi husika,” alisema.

Alisema pia kwamba katika sikukuu hii ya Eid watu wote wanatakiwa kusameheana pale walipokoseana, kupeana zawadi pamoja na mikono ya heri, kwani itaondoa chuki zilizopo miongoni mwa mtu na mtu na hatimaye jamii nzima, kwani hivyo ndivyo alivyofundisha Mtume Muhammad.

Naibu Kadhi wa Tanzania, Sheikh Ally Mkoyongore, ndiye aliyeongoza mamia ya Waislamu kuswalisha ibada hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles