33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wawakilishi CUF wawasha moto

0D6A9345Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

WAKATI Jumuiya za kimataifa zikiendelea kushinikiza mgogoro wa kisiasa Zanzibar umalizwe, wawakilishi wateule 27 wa CUF Zanzibar, wamepigilia msumari wakisema wao ni wawakilishi halali na kwamba hawatambui kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.

Wawakilishi hao wamesema kuwa, sheria na Katiba ya Zanzibar haziruhusu mtu yeyote kufuta matokeo yao, kwa kuwa walishatangazwa na kupewa vyeti vya ushindi.

Wawakilishi hao 18 kutoka Pemba na tisa kutoka Unguja ambao ni kati ya wawakilishi 54 wa majimbo yote ya uchaguzi visiwani humo, waliyasema  hayo jana jijini Dar es Salaam.

Akisoma tamko kwa niaba ya wenzake, Mwakilishi wa Mgogogni, Abubakar Khamis Bakari alisema wawakilishi wote walishapigiwa kura, kutangazwa na kupewa vyeti vya kutambuliwa kwa ushindi wao na hakuna mtu yoyote aliyelalamika kuwa uchaguzi ulikuwa na dosari.

“Ni kutokana na kukamilika kwa hatua zote bila kuwepo malalamiko yoyote na kwa kufuata masharti ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka 1984, ndipo wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote ya Unguja na Pemba wakatutangaza washindi wa nafasi za uwakilishi na udiwani na pia kutupa taarifa za maandishi   wagombea tulioshinda,” alisema bakari ambaye katika Serikali iliyopita alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Alisema kifungu hicho cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kinaeleza kuhusu mamlaka ya msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.

Alinukuu kifungu kidogo (a) kinachosema. “Haraka atamtangaza mgombea aliyepata wingi wa kura halali zilizopigwa kuwa amechaguliwa; na (b) atapeleka taarifa ya maandishi kwa mgombea aliyeshinda; na (c), atatoa taarifa ya matokeo ya uchaguzi kwa tume ambayo itapeleka matokeo hayo, pamoja na idadi ya kura alizopata kila mgombea katika kila jimbo kutangazwa katika gazeti rasmi,” alisema.

Alisema, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka  1984, imetoa uwezo na mamlaka yote ya kusimamia na kuendesha uchaguzi wa wawakilishi na madiwani kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.

Alisema hakuna sehemu yoyote katika Katiba ya Zanzibar ya 1984 wala katika Sheria ya Uchaguzi inayotoa uwezo au mamlaka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa ujumla wake, kufuta uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi wa wawakilishi na madiwani.

Alisema kazi pekee iliyotajwa katika kifungu cha 88 (c), cha sheria ya uchaguzi ni kwa tume ya uchaguzi baada ya kupokea taarifa ya matokeo ya uchaguzi kutoka kwa  msimamizi wa uchaguzi wa jimbo na idadi ya kura alizopata kila mgombea katika kila jimbo, kutangaza matokeo hayo katika gazeti la serikali.

“Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kifungu cha 123, kimeweka bayana kwamba baada ya msimamizi wa uchaguzi kumtangaza mshindi, nafasi pekee ya mtu mwenye malalamiko kutaka matokeo hayo yatenguliwe ni kwa kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.

“Kwa hiyo si mwenyekiti wa tume wala tume yenyewe mwenye uwezo wa kutengua matokeo ya uchaguzi ya mwakilishi au diwani yaliyokwisha tangazwa na msimamizi wa uchaguzi. Uwezo na mamlaka hayo yamewekwa kwa Mahakama Kuu ya Zanzibar pekee,” alisema.

Bakari liitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kufuta uamuzi wa mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha na kuendelea na majumuisho ya kura za rais na kumtangaza mshindi.

Alisema ni vema wawakilishi wote kutoka vyama vyote, wakaapishwa ili waanze kuwatumikia wananchi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mtopepo, Nassor Ahmed Mazrui, alikanusha taarifa kuhusu mgombea urais wa chama hicho Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kukutana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mamunyange kama ilivyopendekezwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.

Mazrui ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar) aliulizwa iwapo kuzungumza kwao na waandishi wa habari, kunatoka na mazungumzo ya Rais mstaafu Kikwete na Maalim Seif kutozaa matunda.

“Maalim Seif ataendelea kufanya mazungunzo na watu wa ngazi yake na sisi tutaendelea kusema yetu, sisi hapa leo tumekuja na suala la wawakilishi,” alisema Bakari.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa chama hicho, Jussa Ismail Ladhu, alisema inashangaza kuona uchaguzi wa wawakilishi kubatilishwa hali ya kuwa ule wa wabunge wa Muungano ukionekana ni halali.

“Uchaguzi huo ulifanywa kupitia daftari moja la wapiga kura, kitambulisho kimoja. Hicho hicho ndiyo kilitumika kupiga kura tano ikiwa ni pamoja na za wabunge wa Zanzibar, wawakilishi, madiwani na wabunge wa Bunge la Muungano,” alisema Jussa ambaye ni Mwakilishi mteule wa Jimbo la Malindi.

Novemba 5, mwaka huu aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alisema CUF inaendelea kutafuta haki ya Wazanzibari kutaka ZEC iendelee kutangaza matokeo ya uchaguzi, ili mshindi ajulikane na hatimaye kuapishwa.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika makao makuu ya CUF Mtendeni, baada ya kurejea visiwani humo katika safari yake ambayo alikutana na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

FATMA KARUME

Katika kile kinachooneka kuibuka kwa mgogoro wa kikatiba, Mwanasheria wa visiwani Zanzibar Fatma Karume, hivi karibuni, alisema Mwenyekiti wa ZEC amevunja Katiba ya Zanzibar akisema uamuzi wa kufuta uchaguzi ni wake binafsi na si tamko la kisheria.

“Tuseme ukweli si Jecha, kwa sababu Jecha hana jeshi. Jecha hana Polisi. Wazanzibari tumenyimwa haki yetu si na Jecha. Tumenyimwa haki yetu na wale watu waliotuma Jeshi pale na kutuma polisi pale,” alisema Fatma.

Akizungumza  katika mahojiano na Redio Ujerumani (DW), Fatma, aliwatupia lawama wenye mamlaka na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Polisi, kwa kuzuia kutangazwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar.

“Kama ni kusema, Jecha kasema tu, lakini hana mamlaka na kama ni kulaumiwa Jecha atalaumiwa kwa kutumiwa dhidi ya masilahi na haki ya Wazanzibari,” alisema.

Akizungumzia suala hilo kikatiba na kisheria, Fatma Karume alisema Serikali imezuia kutangazwa matokeo ya uchaguzi na wala si kufuta uchaguzi, kwa sababu si Jecha wala serikali iliyo na mamlaka ya kufuta uchaguzi.

Mawaziri waachia ngazi

Wakati hali ikiendelea hivyo, juzi mawaziri sita kutoka chama cha CUF waliopo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo walitangaza kuacha ngazi kwa kile walichodai kuwa ni kumalizika kwa muda wa serikali hiyo inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.

Akitoa taarifa hiyo juzi visiwani Zanzibar katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, Bakari alisema mawaziri wote wa chama hicho pamoja na manaibu watatu wamekwisharudisha magari ya Serikali katika mamlaka husika.

Bakari alisema kwa mujibu wa kifungu cha 28 (2) cha Katiba ya Zanzibar kipindi cha Dk. Shein pamoja na baraza la mawaziri kuendelea kubaki madarakani kimekwisha tangu Novemba 2, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles