27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kadi za kura zauzwa 100,000/-

voter*Wanaume wadaiwa kuiba za wake zao

 

NA ARODIA PETER, DAR ES SALAAM

ZIKIWA zimebaki siku 14 kabla ya Watanzania kupiga kura, baadhi ya watu katika Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera wanadaiwa kununua vitambulisho vya kupigia kura vilivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wakazi wa kisiwa hicho walipiga simu katika gazeti la MTANZANIA wakimtuhumu mmoja wa wagombea udiwani wa Kata ya Goziba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Masaba Nkunami, kuwa ndiye kinara wa ununuzi huo wa vitambulisho hivyo kinyume cha sheria.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Rogers Mutalemwa alisema mgombea huyo kwa kushirikiana na katibu wa chama chake (jina tunalo) wamekuwa wakiwarubuni baadhi ya wananchi kwa kununua kadi zao kwa gharama kati ya Sh 50,000 hadi 100,000 kila moja.

Mutalemwa alisema kadi hizo zimekuwa zikinunuliwa usiku kwa watu ambao hawana msimamo mkali wa kisiasa na wenye tamaa ya pesa.

Mkazi huyo alisema baada ya dau hilo kuwa kubwa baadhi ya wanaume wameamua kuiba vitambulisho vya wake zao kwa ajili ya kujipatia fedha.

“Mimi ni mmoja wao, nasikitika kitambulisho changu sikioni nyumbani, awali nilidhani nitakipata, lakini nilikuja kushtuliwa na wanawake wenzangu walionieleza kuwa nao wameibiwa vitambulisho hivyo na waume zao, ninaomba serikali itusaidie, tunaona haki yetu imepotea,” alisema mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Marygolethi.

“Tunasikia diwani kwa kushirikiana na viongozi wengine wananunua vitambulisho hivyo, tulisharipoti matukio hayo polisi, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kukomesha vitendo hivyo.

“Tulitoa taarifa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Msaidizi wa Goziba aitwaye Afande Jose, ambaye alipiga marufuku watu wasitembee usiku, lakini bado mgombea huyo na watu wake wanaendelea na zoezi hilo,” alisema Mutalemwa.

Mwananchi mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema baada ya vitendo hivyo kukithiri, walitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Goziba, Renald Mapesa, lakini hakutoa ushirikiano wowote.

Mwenyekiti huyo alipopigiwa simu alisema hawezi kuzungumzia suala hilo, kwani yuko Mjini Bukoba kwenye semina. “Sina taarifa ya suala hilo, sijawahi kulisikia, hata hivyo niko kwenye semina Mjini Bukoba,” alisema.

Katika hatua nyingine, Nkunami ambaye anatuhumiwa kununua vitambulisho vya kupigia kura alikamatwa na wananchi juzi saa nne usiku akidaiwa kuwa kwenye harakati za kutoa rushwa kwa kundi la kina mama.

Mgombea huyo anadaiwa kukamatwa katika eneo la Zahanati, Kitongoji cha Bwiminga, akiwa na kundi la wanawake na kusababisha taharuki na vurugu kubwa kisiwani humo.

Baada ya kukamatwa, Nkunami alipelekwa katika Kituo cha Polisi Goziba ambako alihojiwa na kuandikisha maelezo yake.

Akisimulia tukio hilo, Ndozi Maboko ambaye ni kati ya vijana walioshiriki kumkamata Nkunami, alisema walipata taarifa kutoka kwa mmoja wa akina mama ambao waliandaliwa kwenda kukutana na mgombea huyo wa CCM kwa lengo la kupewa pesa.

“Tulipopata taarifa hizo tuliwataarifu polisi ambao walitwambia twende katika eneo hilo tuweke mtego wa kumkamata Nkunami, tulifanya hivyo na tulifanikiwa kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi.

Hata hivyo, Maboko alisema yeye na wenzake wawili, James Dotto na Masha Pamba jana walikamatwa na kuhojiwa na polisi wakidaiwa kumvamia Nkunami akiwa katika shughuli zake za kampeni.

Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Nkunami alikiri kukamatwa na wananchi ambapo alidai kuvamiwa akiwa katika matembezi ya kawaida.

“Niko hapa polisi naandikisha maelezo, ni kweli kuna vijana walinivamia na kunikamata nikiwa eneo la Zahanati saa 2:30 usiku katika shughuli zangu za kawaida, na si kweli kwamba nilikuwa nagawa rushwa.

Kuhusu kununua vitambulisho vya kupigia kura, Nkunami alisema: “Siwezi kufanya hivyo, hayo ni maneno ya wanasiasa wanaonihofia baada ya kuona ninawashinda,” alisema Nkunami.

MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Olomi, ili azungumzie suala hilo, ambapo alisema alikuwa Dar es Salaam kuhudhuria semina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Niko nje ya kituo changu cha kazi, suala hilo siwezi kulitolea ufafanuzi kwa sababu silijui, hivyo nitakupa namba ya msaidizi wangu aliyeko huko ili uongee naye,” alisema Kamanda Olomi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles