33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Lori lavamia msafara wa Magufuli

g3Na Bakari Kimwanga, Maswa

MSAFARA wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, umenusurika kupata ajali, baada ya lori la mizigo kuuvamia na kugonga magari matatu likiwamo lililokuwa limembeba mpiga debe wa chama hicho, Amon Mpanju.

Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika eneo la Njia Panda jirani  kilomita chache kabla ya kuingia Maswa mjini.

Akizungumza na MTANZANIA , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemin Mushi alikiri kutokea kwa tukio hilo.

Alisema wakati msafara huo ukitoka wilayani Meatu, askari polisi waliokuwa wakiuongoza msafara huo walimuaru dereva wa lori hilo lenye namba za usajili T 217 DDY kuegesha pembeni gari lake, lakini alikaidi.

“Msafara wa mgombea urais ulikuwa jirani kuingia Maswa, dereva wa lori aliamuriwa kuliweka pembeni akakaidi, tena kibaya akaongeza mwendo hali iliyosababisha ajali.

“Lori hili ni mali ya Kampuni ya Dilchadri Mill Ltd ya jijini Mwanza, liligonga magari matatu likiwamo gari lenye namba za usajili T 217 CYM aina ya Toyota Land Cruser ambayo iliharibika vibaya na kushindwa kuendelea na safari.

“…Baada ya tukio hili, dereva amekimbia na polisi wanamsaka ili  afikishwe mbele ya vyombo vya sheria,” alisema Kamanda Mushi.

Kutokana na ajali hiyo, Kamanda  Mushi amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Alisema hakuna mtu aliyeumia katika ajali hiyo.

Wakati huo huo, mgombea huyo aliendelea na mikutano yake katika wilaya za Maswa, Kishapu na Igunga.

Kwa nyakati tofauti katika mikutano hiyo, Dk. John Magufuli, aliwataka Watanzania kuchagua wabunge ambao watatetea masilahi yao badala ya wale wanaotoka bungeni kila zinapowasilishwa bajeti.

Alisema endapo atachaguliwa anataka kuona Bunge linalotimiza wajibu wake, ikiwemo kupigania  kero za waliowachagua.

“Haiwezekani wakati wa kujadili hoja za wananchi, wenzako wanatoka nje wanafanya hivi kwa kumkomoa nani?

“Maswa ninyi ni mashahidi kwa muda mrefu hamkuwa na mtu wa kuwasemea tatizo la maji, barabara na hata huduma za afya. Maana kila zinapopangwa bajeti wao wanatoka nje je waziri atajuaje kama kuna tatizo eneo husika.

“Hii si demokrasia hata kidogo ila ni kuwatesa wananchi, kwa hali hiyo sasa Watanzania wote chagueni wabunge wenye masilahi kwenu na watakaosemea shida zenu na si wale wanaotoka nje kila wakati (Ukawa),” alisema Dk. Magufuli

 

Aonya lugha chafu

Alisema ni vema viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kampeni za matusi, kwani hazina tija kwa Taifa.

“Matusi si hoja, ndiyo maana kila ninaposimama situkani mtu, najenga hoja. Tunahitaji kujenga nchi yetu iwe ya amani siku zote,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles