24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Yametimia *Dk. Slaa awashambulia Ukawa, *Asema maaskofu Katoliki wamehongwa, Walutheri wana udini

IMG_5657NA FREDY AZZAH, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ametangaza kuachana na siasa huku akiwatuhumu viongozi wa chama chake, maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuwa wamehongwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Dk. Slaa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena, zikiwa zimepita siku 36 tangu aliposusia mkutano wa kumpokea Lowassa anayegombea urais kupitia Chadema, chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), uliofanyika Julai 28.

Katika mkutano wa jana, Dk. Slaa ambaye pia alikejeli ahadi ya Lowassa kushughulikia suala la masheikh walioko rumande, alisema hana chuki wala hasira na mtu yeyote ndani ya Chadema, ila kwenye taifa kuna misingi inayoongoza siasa ambayo ni lazima ifuatwe.

“Inapofika mahali siasa inaongozwa na misingi ya propaganda, upotoshwaji, mwisho wake ni vurugu, mimi sikuwa likizo kama ilivyosemwa na viongozi wangu, sikupewa likizo na mtu yeyote.

“Ndugu zangu niliamua kuachana na siasa tarehe 28 mwezi wa saba, majira ya saa tatu usiku baada ya kuona yale yanayofanyika ndani ya chama changu hayakuniridhisha na sikukubaliana nayo.

“Ni kweli nilihusika na nilishiriki kuanzia dakika ya kwanza kumpokea Lowassa, na niliweka msingi na msimamo toka dakika ya kwanza, na mwendelezo unavyoendelea, wengine wanashinda kwa wingi wao,” alisema.

Alisema  baada ya jina la Lowassa kukatwa kwenye orodha ya wagombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, alimpigia simu akamshawishi juu ya kutaka kiongozi huyo ajiunge na Chadema.

Dk. Slaa ambaye alikuwa akimtaja Gwajima kama mshenga, alisema baada ya kuzungumza naye, alimshauri asubiri kwanza waonane pamoja na Mbowe.

Alisema baada ya kikao hicho, alitaka Lowassa kwanza atangaze kuondoka CCM na ajisafishe juu ya tuhuma zilizokuwa zimeelekezwa kwake.

Dk. Slaa aliongeza kuwa sharti lake jingine kwa Lowassa alitaka kujua kama akiingia kwenye chama hicho atakuwa na mtaji ama mzigo.

“Tangu siku ya kwanza nilitaka tujue anakuja na nani, peke yake ama ana wafuasi? Ni watu gani, vijana wa bodaboda wanaofuata mkumbo, wa mitaani, ama viongozi makini watakaoweza kuambatana na makamanda?

“Jibu la kwanza tuliambiwa wabunge wasiopungua 50, wenyeviti wa mikoa 22, wa wilaya 88, nikakiri kama ni hivyo kutakuwa na tetemeko la nchi,” alisema Dk. Slaa.

Alisema wakati akiendelea na suala hilo, kuna kamati ndogo iliyokuwa imeundwa kushughulikia ujio wa Lowassa ndani ya chama hicho ambayo Julai 25 ilimtaka aitishe kikao cha Kamati Kuu ya dharura Julai 27.

“Wenzangu walikuwa na haraka sijui walinielewa ama vipi, tarehe 27 mwenyekiti akanipigia simu akasema anaambiwa kuwa sijaridhika, akataka tuongee ili tuingie kwenye mkutano na msimamo mmoja,” alisema Dk. Slaa.

Alisema kwenye kikao hicho hawakuafikiana na baadaye wakaingia kwenye kikao, huku Mbowe akitaka iundwe kamati ndogo ya kuendelea kumshawishi.

“Nikaandika barua ya kujiuzulu nikiwa huko huko kwenye Kamati Kuu, barua ya kwanza nilimpatia Profesa Safari (Abdallah, Makamu Mwenyekiti wa Chadema), akaichukua na kuichanachana, pili nikaandika kwa Makamu Katibu Mkuu Zanzibar (Salum Mwalimu), akaiweka mfukoni akaandika kikaratasi ‘haya mambo yamepangwa, usijisumbue, funga mdomo wako’,” alisema Dk. Slaa.

 

AMTETEA MKEWE

Aidha alisema katika uamuzi wake huo hakushinikizwa na mke wake kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakisema.

“Dk. Slaa na Josephine Watanzania wanawajua, leo hii huyo ni mwanaharakati ana uchungu kwa sababu alitokwa damu kwa ajili ya ukombozi wa nchi hii, ana haki zake, sisi katika familia yetu tumezoea hayo maneno,” alisema Dk. Slaa.

Alisema amekuwa akila mihogo ili Josephine aweze kupata fedha za kuzunguka nchi nzima kuandaa na  kuendeleza harakati.

 

AWASHAMBULIA SUMAYE, LOWASSA

Dk. Slaa alisema Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, siyo mwadilifu kwakuwa ana tuhuma mbalimbali.

Alisema kiongozi huyo ana kashfa mbalimbali ikiwamo kupokonya ardhi na kujimilikisha.

Akimzungumzia Lowassa, alisema: “Ni dhambi kupotosha watu, unahalalisha uovu kwa masilahi yako binafsi, dhambi haihalalishwi na dhambi, CCM hawana ujasiri wa kukemea dhambi, Lowassa alipofika ni kwa sababu ya CCM.

“Tumeng’ang’ania mambo ya Richmond, mimi na Lowassa tuna ugomvi, tangu 2008 nilimwambia acha kulalamika, nikamwambia sema Richmond ni ya nani? Leo anatoka anasema alishinikizwa na mkubwa, ni nani huyo?”

Alisema ripoti ya Bunge dhidi ya Richmond, ilionyesha namna suala hilo lilivyoanza tangu Serikali ya awamu ya tatu hadi zabuni ilivyotangazwa na mzabuni kupatikana.

“Baadaye miezi mitatu baada ya mzabuni kupatikana, Lowassa aliandika barua akieleza hofu yake juu ya Richmond na namna vyombo vya habari vinavyoripoti,” alisema.

Pamoja na barua hiyo, Dk. Slaa alihoji kwanini Lowassa aliiandika kwa wakati huo na kwanini mzabuni alitakiwa kupatikana ndani ya siku 10 badala ya 40.

“Chadema ilikuwa ni tumaini jipya, lililojengeka kwahiyo vijana wengi wakisikia jina la Chadema wanajitokeza, sitaki vijana wangu mfike baadaye muanze kujilaumu kama  mwaka 2010 mlivyoambiwa maisha bora kwa kila Mtanzania.

“Tulihamasika baada ya kuambiwa maisha bora, matokeo yake tukajikwaa kwa sababu ya maneno mazuri kwenye tisheti, 2005, sukari ilikuwa 500 leo sh ngapi? Mnayajua.

“Juzi Mwakyembe  (Dk. Harison, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza Richmond) kasema kesi ya jinai haina mwisho, itaamka wakati wowote,” alisema.

Alisema baada ya mkutano wake wa jana, baadhi ya watu watasema ameichana Chadema na kuitetea CCM, lakini imebidi iwe hivyo kwa sababu ndiyo ukweli.

“Niko tayari kushusha heshima yangu hata dunia nzima ili kuridhisha nafsi yangu,” alisema.

 

TUHUMA KWA MAASKOFU

Alisema katika mazungumzo yake na Askofu Gwajima, kiongozi huyo wa dini alimwambia kwamba Lowassa anaungwa mkono na watu wote wakiwamo viongozi wa Kilutheri kwa sababu ndiyo dhehebu lake na wale wa Kanisa Katoliki amewapa fedha.

“Yule mshenga aliniambia Walutheri wanamuunga mkono kwa sababu ni dhehebu lake na kati ya maaskofu 34 wa Katoliki, 30 wamehongwa kati ya Sh milioni 50 mpaka 60.

“Kama hivyo ni kweli, maaskofu pigeni magoti, mmoja, huyo mshenga haoni kwamba ni ukweli, kama kuna wale mashetani walisema, tutajiunga hata na shetani ili tuitoe CCM, mimi sipo tayari, huyu mshenga naye akili yake imepumbazwa,” alisema.

 

AMTUHUMU ROSTAM AZIZ

Katika mkutano wake, Dk. Slaa pia alimtuhumu aliyewahi kuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kwamba wakati alipotaja orodha ya mafisadi katika viwanja vya Mwembeyanga, alimpigia simu na kumwambia ana dakika tano za kuishi na kumtaka asali.

Kabla ya Dk. Slaa kutoa kauli hiyo, aliuliza waandaaji wa mkutano huo kama kwenye eneo hilo wapo askari na kisha ndipo alipotoa kauli yake hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu tuhuma hizo, Rostam alisema ni za uongo kwa sababu hajawahi kuzungumza hayo na Dk. Slaa hata mara moja.

“Sijawahi kuzungumza na Dk. Slaa masuala haya hata mara moja,” alisema.

 

MAKAPI YA CCM

Waandishi walipotaka kujua kwanini Dk. Slaa anaita watu waliohama CCM kwenda Chadema makapi ili hali na yeye alihama kutoka kwenye chama hicho baada ya jina lake kukatwa, alisema yeye hakuwa na kashfa kwa hiyo siyo kapi.

Alipotakiwa kusema endapo hamtaki Lowassa anataka nani awe rais, alisema: “Mimi sina chama, simpigii kampeni mtu yeyote. Nimesema taifa linaweza kupata madhara gani.”

 

WALIOMWANDALIA MKUTANO

Jana baada ya matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni kufungwa, MTANZANIA lilimtaka Dk. Slaa aeleze nani ameandaa mkutano wake pamoja na gharama zake.

Katika majibu yake, Dk. Slaa alisema: “Unaijua hii kampuni (akinyoosha mkono kwenye ubao wa kampuni iliyoandaa mkutano huo), unajua ukitaka mkutano unaomba watu wakuandalie.”

Alipoulizwa endapo kauli yake hiyo inamaanisha kwamba hajui walioandaa mkutano, na kwamba ni kiasi gani kililipwa kwa ukumbi na televisheni zilizorusha mkutano huo moja kwa moja, walinzi waliokuwa wakimwongoza walimvuta na kumpitisha mlango wa nyuma akiwa hajajibu swali hilo.

 

TUNDU LISSU

Akihojiwa katika Redio Sauti ya Amerika (VOA) jana, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu,  alihoji sababu za Dk. Slaa kuibuka sasa na kusema Lowassa hakuweka wazi masuala ya kashfa ya Richmond kabla ya kujiunga rasmi na chama hicho.

“Mbona huo ushahidi aliokuja nao leo hakunishirikisha mimi kama mwanasheria mkuu wa chama? Kwanini kaibuka leo? Na hizo gharama za mkutano wake zimebebwa na nani?

“Tulizungumza kwenye Kamati Kuu na kabla ya Kamati Kuu ya chama, na Lowassa akatwambia aliyeruhusu mkataba huo kuendelea ni Rais Kikwete, Dk. Slaa alikuwepo, imeandikwa wapi kwamba lazima Lowassa alete vijana, viongozi wangapi kutoka CCM?” alisema Lissu.

Habari zilizopatikana baadaye kutoka ndani ya Chadema zilisema licha ya kiongozi huyo kusema aliandika barua ya kujiuzulu Julai 28 mwaka huu, chama hicho kimeendelea kumlipa mshahara ukiwamo wa mwezi uliopita.

“Hata gari alilonunuliwa na chama ameendelea kulitumia hadi leo (jana) ambako aliamua kulirudisha saa chache kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari,” kilisema chanzo hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles