23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Nyumba yateketea kwa moto na kuua tisa wa familia moja

Pg 2NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MOTO ulioteketeza nyumba na kuua watu tisa wa familia moja, umeacha simanzi baada ya kuelezwa kwamba mmoja wa waliopoteza maisha ni bibi aliyefariki akiwa amekumbatia wajukuu zake watatu na mama aliyemkumbatia mwanawe.

Katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana eneo la Buguruni Malapa, Ilala jijini Dar es Salaam, baba mwenye nyumba hiyo, Masoud Mattar, ndiye aliyesalimika kwa sababu alikuwa kazini.

Moto huo unadaiwa kutokea saa 9 usiku wa kuamkia jana na unaelezwa kusababishwa na hitilafu ya umeme ambayo tangu juzi kuanzia saa 2 usiku ilikuwa imeanza kutokea kwenye nguzo ya umeme iliyopo nje ya nyumba hiyo.

MTANZANIA lilishuhudia miili hiyo ikitolewa kwenye nyumba hiyo ikiwa imeshikana mithili ya watu waliokumbatiana huku wakisali, kuonyesha kwamba walifariki dunia wakiwa wamekumbatiana.

Baba wa familia hiyo, Mattar, akiwa ameketi chini kwenye viwanja vya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), aliwaambia waandishi wa habari hana cha kusema zaidi ya kuomba asionyeshwe miili ya wanafamilia yake hao kwani na yeye anaweza kufariki.

“Ninachowaomba ndugu zangu mniache nipumzike…sina cha kusema zaidi ya kuomba nisionyeshwe maiti kwani na mimi naweza kufa, watoto wangu wamekufa bado wadogo, tena wamekumbatiana,” alisema Mattar huku akibubujikwa machozi.

Ofisa uhusiano wa hospitali hiyo, John Steven, alisema waliipokea miili ya watu hao juzi usiku ikiwa imeungana na kuihifadhi kwenye chumba cha maiti.

“Kwa kweli inasikitisha, watu wale walikuwa wameungua vibaya mno kiasi kwamba ilikuwa tabu kuwatambua kwa haraka,” alisema.

 

WALIOFARIKI KATIKA TUKIO HILO

Steven aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Samira Ibrahim (42) – mke wa Mattar na watoto wake Aisha Masoud (17), Ahmad Masoud (15), Abdilhah Masoud (10) na Ashiraf Masoud (5).

Wengine ni Bimdogo Masoud (72), ambaye ni mama mzazi wa Samira, msichana wa kazi Samira Haroub (17), Waadhat Swalleh (27) – mtoto wa kaka yake Samira, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msasani Islamic English Medium na mwanawe Fahir Fesal (2).

 

WAFARIKI DUNIA WAKIOMBA MSAADA

Wakati moto huo ukiendelea, MTANZANIA lilishuhudia mama mmoja akitokea katikati ya moto akiwa amemshika mtoto na kutupa funguo nje kupitia mlango uliokuwa wazi ili wasamaria wema wafungue mlango wa chuma uliokuwa umefungwa na kuwaokoa.

Baada ya kurusha funguo hizo nje, mama huyo alirudi ndani kwenye baadhi ya vyumba ambavyo vilikuwa havijaanza kushika moto kutokana na eneo hilo la mlango mkubwa kuwa na moto mkali.

Lakini kutokana na moto kuwa mkali, majirani waliokuwa wakihangaika kutaka kufungua mlango huo, hawakuweza kutumia funguo hizo kuwaokoa kutokana na kuzidiwa na moto.

Wakati wote huo, sauti zilizokuwa zikisikika kutoka ndani ya nyumba hiyo zilikuwa zikisema: “Majirani tusaidieni, tunakufa, tusaidieni.”

Wakati juhudi za kutaka kuwaokoa zikiendelea, mtungi wa gesi uliokuwa ndani ya nyumba hiyo ulilipuka na kung’oa mabati na kisha moto kusambaa nyumba nzima.

Kitendo hicho kiliwafanya majirani wakimbie kutokana na kishindo cha mtungi huo na ndipo ulipokuwa mwisho wa kelele kutoka ndani ya nyumba hiyo.

 

MLANGO WA CHUMA KIKWAZO

Baadhi ya majirani waliliambia MTANZANIA kuwa, mlango wa chuma ulioshindikana kufunguliwa, uliwekwa hivi karibuni baada ya wezi kuiba kwenye nyumba hiyo.

Walisema baada ya kuwekwa mlango huo, familia hiyo ilikuwa haitumii tena na badala yake walikuwa wanatumia wa uani.

 

ZIMAMOTO

Baada ya kikosi cha Zimamoto na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala kufika eneo hilo, utaratibu wa kubomoa mlango huo wa chuma ulianza na kufanikiwa, lakini tayari watu wote walikuwa wamepoteza maisha.

Mmoja wa majirani alilieleza MTANZANIA kuwa juzi jioni aliona wageni wawili waliofika katika nyumba hiyo wakiwa na mtoto mchanga, ambao anadhani kuwa nao waliteketea kwa moto huo.

Jirani mwingine, Mbarouk Mohamed, alisema mazingira ya nyumba hiyo yaliwapa shida watu hao kuweza kujiokoa kwakuwa sehemu ya sebule ilikuwa jirani na jiko, hivyo moto ulivyopamba walishindwa kujiokoa kwakuwa ndiyo ilikuwa njia ya wao kupita.

Alisema watu hao walikuwa wamelala katika baadhi ya vyumba vitano vilivyokuwa nyuma ambapo mlango mkubwa wa kutokea ndio uliokuwa umepamba moto tayari.

 

MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, alisema kamati ya ulinzi na usalama imepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na inatoa pole kwa familia ya marehemu.

Alisema tukio hilo limetokea kwa mapenzi ya Mungu kwakuwa jitihada zilifanyika, lakini ikashindikana kuokoa maisha ya watu hao.

“Mwenyezi Mungu alete subira katika kipindi hiki kigumu ambacho kimetokea katika familia hii… ila tunachoweza kusema kwa sisi tunaoamini dini, siku zao zilifika na Mungu awape pumziko kwani hatuna namna nyingine ya kuongea,” alisema Sadiki.

Alisema kwa taarifa alizozipata ni kuwa familia hiyo siku za hivi karibuni waliingiliwa na wezi hivyo wakalazimika kufunga mlango mmoja na kutumia mwingine ambao pia waliweka mlango wa chuma.

Sadiki alisema kutokana na hali hiyo, familia hiyo ilikuwa na mazoea ya kutumia mlango mmoja tu hali ambayo ilichangia jana kushindwa kujiokoa kwakuwa mlango mmoja ulikuwa haufunguki.

Alisema kutokana na ukubwa wa tukio hilo, Serikali itachangia sanda pamoja na chakula kwa wafiwa.

“ Tunaelewa mwenzetu (Mattar) alivyopata mshtuko kwa tukio hili, sisi kama Serikali tutaangalia namna ya kumsaidia ili ajiweke katika hali nzuri, hata kama ni mfanyakazi tunaamini tukio hili limemuweka katika hali ngumu,” alisema Sadiki.

 

KAMISHNA KOVA

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema ni vyema jamii  inapojenga nyumba na kuweka milango ya chuma ikaweka pia mlango wa dharura kwa sababu za kiusalama.

Kamishna Kova aliwataka wananchi kujenga mazoea ya kuweka filimbi ndani ya nyumba zao zitakazowasaidia kupeana taarifa pindi panapotokea dharura.

 

NENO LA SHUKRANI

Katibu wa Msikiti wa Ghuram uliopo Buguruni Malapa, Jamalidin  Ayoub alisema moto huo ulizimwa saa 10 alfajiri.

Alisema baba wa familia, Mattar, wakati tukio hilo likitokea alikuwa amekwenda kazini na muda huo alikuwa akirejea na ndipo alipokuta nyumba imeteketea yote na mali iliyokuwapo pamoja na familia yake.

Kutokana na hali hiyo, katibu huyo alisema walilazimika kumpeleka msikitini kwa ajili ya kumfariji na kuweka mambo sawa.

“Hali ya ndugu yetu ilikuwa mbaya, tulijitahidi sana kumfariji. Lakini hata hivyo tunaishukuru Serikali pamoja na watu mbalimbali ambao walijitokeza kumfariji na wananchi wamejitahidi kuchanga zaidi ya Sh 500,000 kwa ajili ya mwenzetu,” alisema.

Hadi MTANZANIA, familia ya marehemu pamoja na kamati ya ulinzi wakiondoka katika viwanja vya nyumba hiyo iliyopo jirani na kituo cha mabasi cha Buguruni Malapa saa 5:30 asubuhi, moto ulikuwa ukiendelea kuwaka, huku kuta zikiendelea kuporomoka hali ambayo iliwafanya polisi kuweka uzio maalumu ili wananchi wasipate madhara zaidi.

 HALI ILIVYOKUWA MUHIMBILI

Miili ya marehemu ilifikishwa hospitali ya Muhimbili jana saa 12 asubuhi na ilipofika saa 7:00 mchana umati wa watu ulikuwa umefurika kwa ajili ya kutoa salamu za mwisho kwa marehemu hao ambao walikuwa wanasomewa dua katika msikiti uliopo ndani ya hospitali hiyo.

Katika eneo lililoko karibu na chumba cha kuifadhia maiti kulikuwa na idadi kubwa ya waombolezaji walioonekana kuwa na nyuso zilizojawa na huzuni.

“Jamani wenzetu wana msiba mkubwa, watu tisa wote Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi awape faraja maana inatia huzuni,” alisikika mmoja wa waombolezaji hao akiwaeleza wenzake.

Maiti hizo ziliondoka saa 7:40 mchana baada ya dua na kuelekea katika makaburi ya Kisutu kwa ajili ya mazishi.

Miili hiyo ilipakiwa katika gari lenye namba za usajili T 963 BUJ Toyota Canter na T 224 BQJ Canter na kufuatiwa na msafara mkubwa kuelekea makaburi ya Kisutu kwa ajili ya maziko.

 

MADEREVA NA WANAFUNZI WALONGA

Mwanafunzi Mohamed Nassor wa darasa la sita katika Shule ya Msasani Islamic English Medium alisema wamepata pigo kutokana na kifo cha mwalimu wao, Waadhat aliyekuwa anawafundisha kompyuta.

Alisema watamkumbuka mwalimu huyo kwa ucheshi wake pamoja na uchapakazi.

Naye Ally Nassor ambaye ni dereva wa basi la shule hiyo, alisema watamkumbuka daima mwalimu huyo ambaye wamefanya naye kazi kwa muda wa miaka sita, kutokana na ucheshi, upole na ukarimu wake.

Alisema mwalimu huyo ambaye alikuwa akiishi maeneo ya Magomeni – Morocco Hotel, alikwenda Buguruni Malapa kumsalimia bibi yake akiwa na msichana wake wa kazi, Samira na mtoto wake mdogo, Fahir ambao wote wamefariki.

Habari hii imeandaliwa na VICTORIA PATRICK (TSJ), CHRISTINA GAULUHANGA, TUNNU NASSOR na VERONICA ROMWALD.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles