23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Masha atoka Segerea

mashaNA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

BAADA ya kuwa chini ya Jeshi la Magereza kwa saa 24, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Laurence Masha, ametimiza masharti ya dhamana na kuachiwa.

Masha aliingia katika Gereza la Segerea juzi alasiri na kuachiwa huru jana alasiri baada ya mahakama kujiridhisha.

Mshtakiwa huyo alipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Waliarwande Lema kwa ajili ya dhamana.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, aliifahamisha mahakama kwamba uhakiki wa masharti ya dhamana umefanyika na wanaodhamini ni watumishi katika ofisi ambazo barua zimetoka.

Hakimu Lema alikubali mshtakiwa huyo kudhaminiwa na Wilfred Mushi ambaye ni dereva wa Makao Makuu ya Chadema na Madala Masha ambaye ni mwanasheria kutoka Kampuni ya Oryx.

Masha aliyesindikizwa na msafara wa magari manane ya polisi pamoja na gari kubwa lenye maji ya kuwasha huku king’ora kikipigwa kuelekea gerezani juzi saa kumi alasiri, jana aliondoka akiwa huru.

Masha anashtakiwa kwa kutoa lugha ya matusi na vitisho kwa maofisa wa polisi katika Kituo cha Polisi Oysterbay.

Wakili wa Serikali Simon alimsomea Masha mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Lema.

Simon alidai mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja, kwamba Agosti 24, mwaka huu katika Kituo cha Polisi Oysterbay, alitumia lugha ya matusi na vitisho kwa Inspekta Msaidizi wa Polisi, Juma Mashaka na polisi wengine.

Inadaiwa aliwaambia polisi hao ni ‘stupid’, ni washenzi, waonevu, hawana shukurani, huruma wala dini, maneno ambayo yalisababisha uvunjifu wa amani.

Masha alikana mashtaka, upelelezi haujakamilika na Hakimu Lema alikubali mshtakiwa kudhaminiwa kwa dhamana ya Sh milioni moja, wadhamini wawili ambao watasaini dhamana ya Sh milioni moja.

Kesi itatajwa Septemba 7 mwaka huu. Wakati Masha akiachiwa kwa dhamana, wafuasi wa Ukawa ambao ni wanafunzi 10 na wafanyabiashara tisa waliovalia tisheti zilizoandikwa ‘Team Mabadiliko, mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCM yatapatikana nje ya CCM’ wanaendelea kusota rumande hadi Septemba 8, mwaka huu endapo hawatatimiza masharti ya dhamana.

Wafuasi hao wanadaiwa kwa pamoja Agosti 24, mwaka huu maeneo yasiyojulikana jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kukusanyika isivyo halali.

Shtaka la pili, washtakiwa wote kwa pamoja Agosti 24 mwaka huu maeneo ya Morocco, Dar es Salaam walikusanyika bila kibali kwa lengo ka kufanya maandamano na kusababisha watu wa maeneo hayo kuamini kungetokea uvunjifu wa amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles