30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Nyalandu: Hakuna majangili ambao hawajafikishwa kortini

Lazaro Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema hakuna majangili wanaojulikana na hawajafikishwa kwenye vyombo vya dola kama ambavyo watu wamekuwa wakimnukuu Rais Jakaya Kikwete.

Akiwa kwenye mkutano jijini London, Uingereza, Rais Kikwete alisema kuna majangili wakubwa 40 na wanafahamika.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi usiku baada ya kumalizika kwa mkutano wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulika na mambo ya Afrika, Mark Simmonds na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe, Nyalandu alisema watuhumiwa zaidi ya 2,000 wa ujangili wamefikishwa mahakamani.

“Najibu hilo swali kwa mara nyingine tena, hakuna majangili wanaojulikana ambao hawajafikishwa kwenye vyombo vya sheria, siyo hao 40 tu, watu zaidi ya 2,000 wamefikishwa mahakamani na wengine wakatoka kwa ushahidi kukosekana.

Kilichokuwa kinatokea mwanzo ilikuwa ni ugumu wa kuwakamata, kulikuwa na watu wanatembea mbugani wakiwa wamevaa rubega kama Wamasai, wanapita wanatembea wakiona tembo wanachukua simu wanapigia wengine na kuwaelekeza walipo tembo.

Wanaoelekezwa wanakuja wanapiga risasi moja na wanaua tembo na wao wanaondoka, anakuja mwingine anachomoa meno na kuyaweka pembeni na wengine wanakuja na pikipiki na kuyabeba, kwa hiyo ilikuwa vigumu kuwakamata,” alisema Nyalandu.

Alisema kuwa, kwa sasa serikali imejiimarisha kwa kununua silaha za kisasa, ikiwamo bunduki nyingi za AK45 na zana nyingine za kisasa.

Alisema pia kuwa Serikali ya Uingereza imekubali kutoa fedha za kujenga ghala la kisasa la kuhifadhi meno ya tembo yaliyo nchini, huku akisisitiza kuwa hayatateketezwa.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulika na mambo ya Afrika, Mark Simmonds, akizungumza jijini Dar es Salaam juzi usiku, alisema kuwa serikali yake itashirikiana na Tanzania katika kuendelea kuimarisha uhifadhi.

Alisema pia kuwa wanaendelea kuelimiza watu wanaojihusisha na kununua meno hayo ambao wengi wanatoka China juu ya athari ya biashara hiyo.

Aliipongeza pia Tanzania kwa juhudi zake za kutoa wanajeshi kwa ajili ya kulinda amani kwenye nchi mbalimbali.

Alisema vikosi vya Tanzania vinavyounda vikosi kadhaa vya Umoja wa Mataifa ni suala zuri kwa taifa.

Alisema kuwa amani kwenye nchi za mazima makuu ni muhimu ikadumishwa na vikosi vya uasi kwenye mataifa hayo ni vyema vikaweka silaha chini.

Naye Waziri Membe alisema kuwa Tanzania inazitaka nchi zinazotumia maji ya Mto Nile zielewe kuwa haziwezi kuwa na haki sawa na Misri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles