30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wampa kibano Waziri Nyalandu

Lazaro-NyalanduNa Khamis Mkotya, Dodoma
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge wengi kushutumu utendaji wake wakisema umekuwa chanzo cha wizara hiyo kuzorota katika maendeleo.
Kwa mujibu wa wabunge hao, kitendo cha waziri huyo kushindwa kutekeleza agizo la mahakama kuhusu tozo mpya katika hoteli za utalii kimefanya Serikali kupoteza zaidi ya Sh bilioni 20 kila mwaka.
Wabunge hao pia walishangazwa na kitendo cha wizara hiyo kulazimisha mfumo wa ‘Double Entry’ (mtalii kulipa mara moja) unaosababisha hasara badala ya mfumo wa ‘Single Entry’ unaotaka mtalii kulipa ada ya kiingilio kila anapoingia hifadhini.
Waliyasema hayo walipojadili makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Akisoma maoni ya wabunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema licha ya kamati yake kutoa ushauri na Bunge kutoa maagizo, waziri huyo amegoma kuyatekeleza.
“Takwimu zinaonyesha kwa miezi 10 yaani Julai, 2014 hadi Machi, 2015 Hifadhi ya Serengeti na Hifadhi ya Ziwa Manyara zilipoteza zaidi ya Sh bilioni 1.4 kutokana na wizara kulazimisha mfumo wa ‘Double Entry’. Kamati inahoji kuna maslahi gani waziri kutetea mfumo ambao unaipotezea Serikali mapato?” alihoji Lembeli.
Lembeli alisema katika mkutano wa 18 wa Bunge, kamati ilishauri na Bunge likaazimia kwamba waziri huyo atekeleze hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliyomtaka Nyalandu kutangaza katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika hoteli za utalii nchini.
“Bunge lilimpa muda waziri wa maliasili na utalii awe ametoa tangazo hilo mwishoni mwa Februari, 2015, kutokana na kuchelewesha kuanza kutumika kwa tozo mpya hadi kufikia Machi 15 mwaka huu, Serikali imepoteza Sh bilioni 3.076.
Kambi ya upinzani
Akiwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema kinachoonekana ni wizara hiyo kukosa dira kufikia malengo yake.
Msigwa alisema changamoto ambazo zipo ni sawa na zile za kamati ya bunge, hivyo ni wajibu wa waziri kuweka wazi kuwa ana maslahi gani na migogoro mingine ambayo imefikiwa mwafaka hata ile ya uamuzi wa mahakama.
“Nashindwa kujua hivi hata hili la kuwa tumepoteza Sh bilioni 1.4 na Sh biloni 3 linakuwa gumu kufanyiwa uamuzi ni kwa maslahi ya nani au ndiyo mnajenga mazingira mazuri ya Ukawa kuchukua nchi,” alisema.
Katika mchango wake, Msigwa alisema ni wakati mwafaka Serikali kuweka bayana kuhusu suala la Ndege ya Kijeshi kutoka Qatar kuingia nchini na kuchukua wanyama kwa sababu uchunguzi wake umeshakamilika.
Nyalandu
Awali, akiwasilisha bajeti yake, Waziri Nyalandu alisema wizara yake imejipanga kuhakikisha inatatua migogoro yote baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa na kuhakikisha uhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili kwa maendeleo ya utalii yanalindwa kwa ukamilifu kwa mujibu wa sheria.
Alisema katika kuhakikisha migogoro ya mipaka na uvamizi na maeneo yaliyohifadhiwa inakomeshwa, wizara itaendelea kurekebisha na kuweka alama za kudumu za mipaka na kufanya doria za mara kwa mara na kuelimisha umma.
Pia alisema wizara itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wake kuhakikisha inadhibiti migogoro isiyokuwa na tija baina yao na wananchi waishio jirani na hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Nyalandu alisema tayari ameipatia ufumbuzi wa kudumu migogoro mbalimbali ya ardhi ukiwamo ule wa Mbarali, ambao umedumu kwa miaka saba bila kupatiwa suluhisho.
Kwa mujibu wa Nyalandu, Tanzania inafuatiwa na Botswana, Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Namibia, Uganda, na Zimbambwe.
Alisema kwa sasa idadi ya watalii wanaotembelea nchini imeongezeka kwa asilimia nne kutoka 1,095,884 hadi 1,140,156 mwaka jana huku mikakati mbalimbali ikiendelea kutekelezwa ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles