33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Majimbo 12 yapendekezwa Dar

HALIMA MDEESHABANI MATUTU NA CHRISTINA GAULUHANGA, Dar es Salaam
KIKAO cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam (RCC)jana kilitawaliwa na vijembe kutoka kwa wajumbe walioshiriki katika mapendekezo ya ugawaji wa majimbo ya mkoa huo.
Vijembe hivyo viliibuka wakati wa mjadala wa mgawanyo wa majimbo hayo, kati ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Viongozi hao walianza kurushiana vijembe baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA)ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kutoa mapendekezo ya kutaka Wilaya ya Kinondoni igawanywe katika majimbo manne.
Hoja ya Mdee ilipingwa na Mbunge wa Viti Maalum, Zarina Madabida (CCM) ambaye alisema RCC haitakiwi kwenda kinyume na mapendekezo ya Baraza la Halmashauri ya Madiwani Kinondoni (DCC) lililoomba majimbo matano.
Madabida ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM)alimshutumu Mdee kwa kusema anatafuta njia ya kuingiza hoja ya ugawaji wa majimbo ambao una nia ya kuusaidia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Suala hilo lilifanya Mdee kuinuka na kumpinga kwa kusema CCM ndiyo inang’ang’ania majimbo mengi ili wawe na wawakilishi wengi katika uchaguzi ujao.
Wakati akichangia Mdee, mara kadhaa Madabida alikuwa akimkatisha kwa kumtupia vijembe vilivyokuwa vikisababisha kurushiana maneno.
Mvutano huo ulisababisha Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema),kuinuka na kupinga kufanyika mabadiliko katika majimbo ya Ilala.
Katika wilaya hiyo imependekezwa kuwapo jimbo jipya la Chanika, licha ya awali kupingwa na Baraza la Madiwani wa Ilala.
“Kwa nini Ilala imefanyiwa mabadiliko ya kuongeza jimbo moja wakati Kinondoni inazuiliwe kupunguza jimbo moja kwa kisingizio cha kanuni. Hapa cha kujiuliza ni kanuni gani zinaruhusu marekebisho Ilala na kuzuia marekebisho Kinondoni?” alihoji Mnyika.
Alisema CCM imekuwa ikipambana kupunguza gharama inakuwaje inakubali kuongezewa mzigo kwa kukubali kuwa na majimbo matano na kukataa wazo la kuwa na majimbo manne kwa Kinondoni.
Akijibu hoja hiyo, Madabida alisema suala la Kinondoni ni tofauti na Ilala kwa sababu uamuzi uliotolewa Kinondoni ukirejeshwa tena kwa Baraza la Madiwani utarudishwa kwa majibu hayo hayo.
“Kwa upande wa Ilala wanaweza kubadilisha kwa sababu kesi yao ni tofauti na Kinondoni ambayo tayari ilikuwa imejadili suala hili na kutoa uamuzi,” alisema Madabida.
Jibu hilo lilionekana kutomridhisha Mdee ambaye alisimama na kusema kikao hicho kina mamlaka ya kuamua jambo na kulitolea uamuzi.
Lakini Madabiba alimkatisha kwa kusema ‘haiwezekani kuondoa mapendekezo ya baraza la madiwani’ maneno yaliyomfanya Mdee kumtaka akae kimya ili amfundishe.
Baada ya majibu hayoMadabida alisikika akisema kwa sauti ya juu; ‘nani umfundishe’, huku Mdee naye akijibu ‘huniwezi’ na Madabida akimjibu ‘nani atakuweza’.
Mvutano huo ulimfanya Mwenyekiti wa mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadick Mecky Sadick kuwazuia na kumtaka Mdee kujielekeza kwenye hoja ya msingi huku akimtaka Madabida kunyamaza.
Akitoa mapendekezo ya majimbo, Sadick alisema Wilaya ya Temeke itakuwa na majimbo ya Mbagala,Kigamboni, Temeke Kijichi.
Wilaya ya Ilala ambayo ilipendekezwa kuwa na majimbo matatu imeongezewa jimbo la Chanika na yaliyopo ya Ukonga,Segerea na Ilala.
Kwa Wilaya ya Kinondoni yameongezwa majimbo mapya mawili ambayo ni Bunju,Kibamba yakiungana na Ubungo Kawe na Kinondoni.
Ongezeko la majimbo mawili Kinondoni yaliamsha hisia kwa wabunge wa Chadema waliohudhuria kikao hicho jambo lililosababisha kuomba kupigwa kura kuamua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles